1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yasikitishwa kwa kuondolewa katika mpango wa AGOA

28 Desemba 2021

 Ethiopia imesema imesikitishwa na uamuzi wa Marekani kufutilia mbali mpango unaoruhusu bidhaa zinazoagizwa kutoka taifa hilo kuelekea Marekani kutotozwa ushuru.

Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Taarifa hiyo kutoka katika wizara ya biashara ya Ethiopia siku ya Jumatatu, imejiri baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuiondoa Ethiopia miongoni mwa mataifa yanayonufaika na mpango wa kibiashara wa Marekani na Afrika maarufu kama AGOA.

Biden alifanya uamuzi huo mnamo Disemba 23, akisema imetokana na Marekani kupinga vita vinavyoendelea vya jimbo la Tigray.

Wanajeshi wa Ethiopia waamriwa kutokuingia Tigray

Katika taarifa yake, Wizara ya Biashara ya Ethiopia imesema serikali ya nchi hiyo imesikitishwa na uamuzi huo na imeiomba Marekani kuubatilisha.

Wizara hiyo imesema Ethiopia inashughulikia miradi mbalimbali inayolenga kuleta amani na utulivu, maridhiano ya kisiasa na maendeleo ya kiuchumi, kando na kutekeleza mageuzi kuendana  na mahusiano kati ya mataifa hayo mawili, Ethiopia na Marekani.

Marekani ilisitisha manufaa ya kibiashara kwa Ethiopia, licha ya rai kutoka kwa wabunge wachache wa Marekani pamoja na makundi ya kiraia ya Ethiopia yaliyousihi utawala wa Biden kuipa Ethiopia muda zaidi kuhakikisha inatimiza masharti ya Marekani.

Mnamo mwezi Septemba, Biden alionya kwamba utawala wake utaweka vikwazo vikali ikiwa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed hatachukua hatua madhubuti kumaliza vita katika jimbo la Tigray na majimbo mengine.Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Ethiopia yadai kuchukua udhibiti wa Alamata

Uamuzi dhidi ya Ethiopia ulifikiwa kufuatia kushindwa kwake kumaliza vita vya jimbo la Tigray ambavyo vimedumu kwa takriban mwaka mmoja sasa.

Biden alisema kupitia tarifa kuwa vita hivyo vimesababisha "ukiukwaji mkubwa” wa haki za binadamu.

Lakini si Ethiopia pekee iliyofutiwa manufaa hayo, bali pia Guinea na Mali ambazo hazitanufaika kutokana na na mpango huo kuanzia Januari Mosi.

Umoja wa Mataifa waagiza uchunguzi wa kimataifa Ethiopia

Mpango wa kimaendeleo na kibiashara AGOA, unaziruhusu nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara, kuuza bidhaa zao katika masoko ya Marekani bila ya kutozwa ushuru, lakini kwa masharti kwamba zinatimiza baadhi ya matakwa mfano; kuondoa visiki vya kibiashara na uwekezaji kwa Marekani na kupiga hatua katika kukuza demokrasia kisiasa.

Maafisa wa Ethiopia walizuia malori ya misaada?

Vita vya jimbo la Tigray kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho Ethiopia na wapiganaji wa TPLF vimedumu kwa takriban mwaka mmoja sasa.Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa zimesema maafisa wa Ethiopia walizuia malori ya misaada kuwasilisha misaada kwa watu waliokuwa na mahitaji makubwa katika jimbo la Tigray. Watu kadhaa wamekufa kutokana na njaa. Hayo ni kulingana na ripoti ya shirika la habari la Associated Press.

UN yasema Ethiopia imewakamata madereva wake 70

Mnamo Novemba 3, wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia iliitaja tahadhari hiyo ya Marekani kama iliyokosa mwelekeo na onyo lisilokuwa na uthibibitisho.

Aidha, wizara hiyo ilisema hatua kama hiyo inaweza kuathiri zaidi ya watu 200,000 wenye kipato cha chini nchini Ethiopia wanaofanya kazi kwenye kampuni zinazonufaika kutokana na mpango wa AGOA.

Baadhi ya kampuni za Ethiopia tayari zinaonyesha ishara za kudidimia kwa kuzingatia bidhaa zinazosafirisha.

"Kampuni kadhaa tayari zimeanza kufunga milango na hatujui nini kitafuata,” mfanyakazi mmoja wa kiwanda cha nguo eneo la Hawassa - yapata kilomita 270 kutoka mji mkuu Addis Ababa ameliambia shirika la habari la Associated Press kwa njia ya simu lakini kwa sharti la kutotambulishwa jina.

Katika miaka ya hivi karibuni, Ethiopia ilikuwa miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyokuwa na kasi kubwa ya ukuaji kiuchumi, lakini vita vya Tigray vimesababisha kasi hiyo kufifia.
(APE)