Ethiopia yasitisha kurusha Boeing chapa 737 Max
11 Machi 2019Ethiopia imeitangaza siku ya leo Jumatatu kuwa siku ya maombolezi huku juhudi za kusaka mabaki na miili ya wahanga wa ajali hiyo zikiendelea.
Ingawa sababu halisi ya kuanguka ndege hiyo ambayo ni mpya bado haijuliKni,shirika la ndege la Ethiopia limeamua kutozirusha ndege nne zilizosalia za chapa hiyo hiyo hadi ufafanuzi zaidi utakapotolewa.
Akitangaza uamuzi huo meneja wa shirika la ndege la Ethiopia nchini Kenya Yilma Goshu amesema;
"Ninapendelea kukuarifuni mapya .Tumeamua kutozirusha ndege zote za Boeing chapa 737 Max 8 Max zilizokuwa zikitumiwa na shirika la ndege la Ethiopia na ambazo zinahusika na ajali ya jana-hiyo ikiwa ni hatua mojawapo ya usalama. Lakini haimaanishi kwamba ajali hiyo ina mafungamano ya aina yoyote na ndege hizo.Tumeamua kuchukua hatua hizo ziada za tahadhari ili utafiti uweze kuendelea."
Shirika la ndege la Ethiopia limekuwa likitumia ndege tano za chama ya Boeing 737 Max 8 na limekuwa likisubiri nyengine 25 ambazo tayari zimeshaagiziwa.
Mashirika mengine yachukua hatua kama hiyo
Mashirika mengine pia ya kimataifa yameamua pia kutozirusha andege zao chama Boeing 737 Max nane, mfano wa shirika la ndege la China na Caribbean Cayman Airways.
Juhudi za kuyatafuta mabaki na miili ya wahanga zinaendelea.Tangu juwa lilipochomoza watumishi wa shirika la msalaba mwekundu wamekuwa wakidondowa mabaki hayo karibu na mahala ndege hiyo ilipoangukia.
Wataalam kutoka Israel wameshawasili kusaidia kujua chanzo cha ajali hiyo. Maafisa wa Ethiopia ndio wanaoongoza uchunguzi huo wakisaidiwa na Mmarekani,wakenya na wengine. Shughuli kama hizi zinahitaji muda" amesema waziri wa usafiri wa Kenya James Macharia.
Majonzi ni makubwa
Watu 157 kutoka mataifa 35 wamefariki kutokana na ajali hiyo ya ndege iliyoanguka dakika sita tu baada ya kuruka toka kiwanja cha ndege cha kimataifa mjini Addis Abeba.Ndege hiyo ilikuwa inaelekea Nairobi nchini Kenya.
Kenya ndio iliyopoteza watu wengi zaidi; watu 32. Kwa mujibu wa waziri wa usafiri James Macharia hadi wakati huu maafisa wa serikali wanawasiliana pamoja na familia za wahanga 25 kati ya hao.
Canada,Ethiopia,Marekani,China,Italia,Ufaransa,Uingereza,Misri,Ujerumani,India na Slovakia kila moja imepoteza kati ya raia mmoja hadi wanne.
Ajali ya ndege ya shirika la ndege la Ethiopia inalingana moja kwa moja na ajali kama hiyo ya shirika la ndege la Indonesia iliyotokea mwaka jana ambapo jumla ya watu 189 waliuwawa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/
Mhariri: Gakuba, Daniel