1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yaudhibiti mji wa pili kwa ukubwa Tigray

Grace Kabogo
21 Novemba 2020

Serikali ya Ethiopia imesema kwamba imeudhibiti mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Tigray ambao umekuwa ukigombaniwa tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba.

Tigray-Konflikt | Äthiopisches Militär
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Siku ya Jumamosi ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ilitangaza kupitia televisheni ya taifa kwamba vikosi vya usalama vimechukua udhibiti wa mji wa Adigrat na vilikuwa vinaelekea katika mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele, ambao una takriban watu nusu milioni.

Hatua ya serikali ya Ethiopia kuendeleza mashambulizi Tigray inaonesha kuwa hakuna dalili zozote za Abiy, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019, kukubaliana na shinikizo la kimataifa la kusitisha mapigano katika mzozo huo unaosababisha hofu ya kuzuka kwa janga la kibinaadamu.

Jeshi la serikali lapongezwa

Katika taarifa yake ya Jumamosi, Abiy alilipongeza jeshi kwa kusonga mbele, akisema sasa vikosi vyao vimeikomboa Adigrat kutoka kwenye mikono ya vikosi vya chama cha Ukombozi wa Watu wa tigray, TPLF. Amesema kwa kushirikiana na Ethiopia yote watahakikisha kwamba mahitaji yote ya kibinaadamu yanashughulikiwa.

''Usalama na ustawi wa jumla wa watu wa Tigray ni muhimu sana kwa serikali ya shirikisho na tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha utulivu unapatikana kwenye mkoa wa Tigray na kwamba raia wetu hawapati madhara yoyote,'' alisisitiza Abiy.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy AhmedPicha: Minasse Wondimu Hailu/picture alliance/AA

Wakati huo huo, Umoja wa Afrika umetangaza kuwa utapeleka wajumbe maalum kuipatanisha serikali ya shirikisho ya Ethiopia na chama cha TPLF kinachotawala jimboni humo, ambacho kwa sasa kinachukuliwa kama kundi la waasi.

Umoja huo umeandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba jukumu la msingi la wajumbe hao litakuwa kuzishirikisha pande zote zinazohusika katika mzozo huo kuonesha nia ya kumaliza uhasama, kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya kitaifa ya kutatua masuala yote yaliyosababisha kutuka kwa mzozo pamoja na kurejesha amani na utulivu Ethiopia.

Serikali yakanusha

Hata hivyo, serikali ya Ethiopia imekanusha kuhusu ziara ya wajumbe hao. Ofisi ya Abiy imesema taarifa zinazosambaa kwamba wajumbe wa Umoja wa Afrika wanaelekea Ethiopia kupatanisha mzozo huo ni za uongo. Abiy amesema anataka kuwaondoa kwanza viongozi wa TPLF kabla ya mazungumzo hayo. Wajumbe walioteuliwa na Umoja wa Afrika ni rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano, Ellen Johnson-Sirleaf rais wa zamani wa Liberia pamoja na aliyekuwa raisi wa Afika Kusini, Kgalema Montlanthe.

Waethiopia waliokimbia Tigray wakiwa kwenye mpaka wa Ethiopia na SudanPicha: Mohamed N. Abdallah/REUTERS

Ama kwa upande mwingine, waasi wa Tigray wamesema raia tisa wameuawa huku watu wengi wakiwa wamajeruhiwa vibaya baada ya vikosi vya serikali ya shirikisho kufanya mashambulizi kwenye mji wa Adigrat. Hata hivyo, shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha taarifa hizo za Adigrat, mji ulioko umbali wa kilomita 116 kutoka Mekele. Serikali na jeshi hawakupatikana mara moja kujibu madai hayo, ingawa awali walikanusha kuwalenga raia.

Taarifa zinazotolewa na pande zote mbili haziwezi kuthibitishwa kiurahisi kutokana na kukatwa kwa mawasiliano ya intaneti na simu kwenye jimbo hilo la kaskazini.

Mzozo kati ya serikali ya Ethiopia na serikali ya jimbo la Tigray ulianza mwanzoni mwa Novemba baada ya Waziri Mkuu Abiy kuyapeleka majeshi yake jimboni humo kuumaliza uasi na kutuliza ghasia zinazofanywa na TPLF. Mzozo huo tayari umesababisha maelfu ya Waethiopia kukimbilia nchi jirani ya Sudan. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, limesema linajiandaa kuwapokea Sudan wakimbizi 200,000 wanaotoka Ethiopia. Hadi sasa wakimbizi 33,000 wameshaingia Sudan.

(DPA, AFP, Reuters)