Ethiopia yaunga mkono kikosi kipya cha kulinda amani Somalia
3 Januari 2025Awali, Somalia ilisema kuwa wanajeshi wa Ethiopia hawatoshiriki kutokana na uhusiano mbaya baina ya nchi hizo mbili, baada ya serikali ya Ethiopia kusaini makubaliano na jimbo la Somaliland lenye utawala wake wa ndani, kuiruhusu Ethiopia kutumia sehemu yake ya bahari.
Lakini baada ya miezi kadhaa ya malumbano, mwezi uliopita nchi hizo mbili zilikubaliana kumaliza mvutano, katika mapatano yaliyosimamiwa na Uturuki.
Alhamisi Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia, Aisha Mohammed aliongoza ujumbe wa ngazi ya juu kuizuru Somalia, kukutana na Rais Hassan Sheikh Mohamud, na aliwasilisha ujumbe wa Waziri Mkuu, Abiy Ahmed. Nchi hizo mbili zilikubaliana kushirikiana na Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Kufanikisha Utulivu Somalia, AUSSOM, na kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.