Etienne Tshisekedi kuzikwa Juni Mosi
22 Mei 2019Tshisekedi, baba wa rais wa sasa wa Kongo, Felix Tshisekedi alifariki dunia mjini Brussels, Ubelgiji miaka miwili iliyopita na alikuwa bado hajazikwa kutokana na tofauti za kisiasa nchini Kongo.
Familia ya Tshisekedi na chama cha UDPS vinaelezea kwamba mwili wa Etienne Tshisekedi utazikwa Jumamosi ya Juni 1, huku maombolezo yanatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha siku mbili mjini Kinshasa.
Askofu aliestaafu na mdogo wa marehemu Tshisekedi, ambae ni kiongozi wa kamati ya maandalizi ya mazishi, Gerard Mulumba amesema kila kitu kinaendelea vizuri kwa ajili ya mazishi ya kaka yake.
''Kwa sasa tunawatangazia wananchi kwamba Tshisekedi atazikwa katika masharti ambayo tulitegemea, na mipango inaendelea vyema kwa ajili ya kuurejesha mwili wake Alhamisi ya tarehe 30 Mei na mazishi yatafanyika Jumamosi ya Juni mosi. Atazikwa kwenye kaburi la kipekee kwenye mashamba ya familia'', alifafanua Mulumba.
Ndege maalumu imekodishwa kwa ajili ya kuurejesha nyumbani mwili huo ambao ulibaki kwenye chumba cha kuhifadhi maiti mjini Brussels kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Wizara ya mambo ya nje ya Kongo imeelezea kwamba takriban marais 20 wameelezea nia yao ya kuhudhuria mazishi ya Etienne Tshisekedi, lakini haijulikani ni wangapi watakaowasili mjini Kinshasa.
Mwili utawasili Mei 31
Ijumaa ya tarehe 31 Mei, mwili wa Tshisekedi utawekwa kwenye uwanja mkuu wa kandanda wa Stade des Martyrs, ambako maombolezo ya wananchi na wafuasi wa chama chake yatafanyika na siku moja baadae itakuwa ni heshima za mwisho za viongozi wa serikali kabla ya mazishi nje ya jiji la Kinshasa.
Toka kufariki kwake Februari 2017, chama cha UDPS na familia vilikuwa havijakubaliana na serikali ya wakati huo ya Rais Joseph Kabila kuhusu mazishi ya Tshisekedi.
Serikali ilikuwa ikihofia kwamba kurejeshwa kwa mwili wake huenda kukazusha vurugu nchini Kongo, huku chama cha UDPS na familia vikishikilia kwamba Etienne Tshisekedi anatakiwa kuzikwa mjini kati.
Serikali imetangaza kwamba Tshisekedi atazikwa na kupewa heshima kama waziri mkuu wa zamani. Tayari kuna wale wanaodai kwamba ni lazima atangazwe kuwa ''shujaa wa demokrasia '' nchini humo.
Wakati huo huo, Rais Felix Tshisekedi amewateua viongozi wapya jeshini na kwenye ofisi yake ikulu, akiwemo mkuu wa jeshi Luteni Jenerali Celestin Mbala. Mbala ameshikilia wadhifa huo toka Julai mwaka jana alipoteuliwa na rais aliestaafu Joseph kabila.
Jenerali Francois Kabamba ametajwa kuwa mshauri wa masuala ya kijeshi wa Rais Tshisekedi. Baba yake mdogo, Gerard Mulumba ameteuliwa kuwa mshauri wa rais anayehusikana na masuala ya kijamii.