1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

EU inalenga kurekebisha mahusiano Kusini mashariki mwa Asia

10 Oktoba 2024

EU inawekeza mabilioni ya pesa kusini mashariki mwa Asia, na maafisa wa Ulaya wanashinikiza kuwepo kwa uhusiano wa kina katika mkutano wa kilelele wa kila mwaka wa Jumuia ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, huko Laos.

Viongozi wa mataifa ya jumuiya ya ASEAN katika mkutani wa kilele nchini Laos, Alhamisi Oktoba10, 2024
Viongozi wa mataifa ya jumuiya ya ASEANPicha: Dita Alangkara/AP/picture alliance

Muungano wa ASEAN wa wanachama 10 unafanya mkutano wake wa kila mwaka huko Laos. Wanachama wa jumuiya hiyo wanaichukulia mikutano hiyo kama jukwaa muhimu la kushirikiana na washirika wa kigeni katika masuala makuu kuhusu siasa, uchumi na usalama.

Umoja wa Ulaya utawakilishwa nchini Laos na rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel. Michel pia amealikwa kuhudhuria mkutano ujao wa kilele wa Asia Mashariki, unaotazamiwa kuanza Ijumaa, ambapo viongozi wa kimataifa wanatarajiwa kujadili masuala mapana yanayoliathiri bara hilo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya kwa ASEANSujiro Seam, ameiambia DW kwamba mualiko huo unauwezesha Umoja huo kujumuika na jumuiya ya ASEAN katika ngazi ya uongozi.

Jumuiya hiyo ya ASEAN inazozijumuisha nchi za Brunei, Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, the Philippines, Singapore, Thailand na Vietnam ni makazi ya takriban watu milioni 685 na inazidi kuwa mhusika muhimu katika uchumi wa dunia.

Biden na Xi hawatahudhuria mkutano wa Laos

Laos, nchi inayoongozwa na wakomunisti, imejitahidi kuepusha mvutano wowote wakati wa uongozi wake kama mwenyekiti wa ASEAN, ikilenga umoja wa kikanda badala ya mizozo ya kijiografia.

Baadhi ya masuala nyeti hata hivyo, yaliibuliwa siku ya Alhamisi, huku Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr akiishutumu Beijing kwa unyanyasaji na vitisho katika Bahari ya China Kusini na kushinikiza kuwepo kwa mfumo wa kanuni za maadili katika eneo hilo linalozozaniwa.

Rais wa China Xi JinpingPicha: Xie Huanchi/Xinhua/picture alliance

Rais wa China Xi Jinping hatahudhuria mkutano huo unaofanyika Laos, huku waziri mkuu Li Qiang akiiwakilisha China. Rais wa Marekani Joe Biden pia hatahudhuria mkutano huo na badala yake anamtuma waziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken. Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer pia hatakuwepo, lakini mwenzake wa Australia Anthony Albanese anashiriki, pamoja na waziri mkuu mpya wa Japan Shigeru Ishiba. Viongozi wa Korea Kusini na Canada pia wako Laos.

Utawala wa kijeshi Myanmar wawakilishwa katika mkutano wa ASEAN

Wachambuzi hawatarajii maazimio yoyote makubwa kuhusu masuala muhimu ya kikanda, kama vile mizozo kuhusu Bahari ya China Kusini au mzozo unaoendelea nchini Myanmar.

Utawala wa kijeshi wa Myanmar utawakilishwa nchini Laos, kwa kumtuma afisa mkuu kutoka wizara yake ya mambo ya nje kwenye mkutano huo. Hata hivyo, uamuzi wa kumwalika, umesababisha mataifa mengine ya ASEAN kuikosoa Laos.

Katibu mkuu wa ASEAN Kao Kim Hourn, amesema jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na Myanmar. Hourn ameliambia shirika la habari la reuters kwamba wanahitaji muda na subira kwasababu suala la Myanmar ni tata na kwamba hawapaswi kutarajia suluhisho la haraka.

Indonesia, ambayo imeshinikiza hatua kali zaidi kwa mzozo wa Myanmar, ilifanya mazungumzo yake wiki iliyopita. Mazungumzo hayo yaliwajumuisha wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayopinga utawala wa kijeshi.

Biashara ya Umoja wa Ulaya barani Afrika

Pembezoni mwa mkutano huo, maafisa wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuzungumza na viongozi wa Kusini Mashariki mwa Asia kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya biashara na uwekezaji.

Rais wa Baraza la Ulaya Charles MichelPicha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Mapema mwezi huu, Umoja wa Ulaya na ASEAN zilifanya kongamano la Mazungumzo ya Washirika huko Jakarta, huku mazungumzo ya kisekta kuhusu masuala kama vile usimamizi wa teknolojia ikiwa imefanyika katika wiki za hivi karibuni.

Wataalamu wanasema mwaka wa 2024 unaelekea kuwa mwaka muhimu kwa uhusiano wa Umoja wa Ulaya na ASEAN.

Mvutano ulipungua baada ya kuchelewa kwa sheria ya EU dhidi ya ukataji miti

Mara kwa mara, serikali za Kusini Mashariki mwa Asia zimezozana na Umoja wa Ulaya kuhusu mapendekezo ya sheria ya Umoja wa Ulaya ya kupinga ukataji miti. Mpango huo unalenga kuzuia uagizaji wa bidhaa kama vile kakao, kahawa, mafuta ya mawese na nyingine nyingi iwapo zitahusishwa na uharibifu wa misitu.

Sheria hiyo ilipangwa kuanza kutumika mwishoni mwa 2024, lakini sasa, imeahirishwa hadi Desemba 2025 kwa kampuni kubwa na Juni 2026 kwa kampuni ndogo.

Malaysia kuchukua uongozi

Malaysia inatarajiwa kuchukua rasmi nafasi ya uenyekiti wa ASEAN mnamo Januari 2025. Katika muda wa miezi 12 ijayo, mojawapo ya vipaumbele vya Malaysia itakuwa kukamilisha ruwaza ya Jumuiya ya ASEANya mwaka 2045, huu ukiwa mpangilio wa masuala ya kikanda katika miongo miwili ijayo.

Hata hivyo, wachambuzi wanaona kuingia kwa Malaysia katika uongozi huo kutaibua changamoto nyingi.