1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU inatamatarajio yapi kwenye uchaguzi wa Marekani?

4 Novemba 2024

Uchaguzi wa Rais wa Marekani unafanyika mnamo Novemba 5, iwapo mgombea wa chama cha Republican Donald Trump ataibuka mshindi, kurejea kwake madarakani kunaweza kusababisha matatizo makubwa barani Ulaya.

Marekani, Washington | Uchaguzi Mkuu 2024 | Kamala Harris
Mgombea Urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Kamala Harris akiwa katika kampeni za uchaguzi.Picha: SAUL LOEB/AFP

Usalama na biashara huria huenda vikawa hatarini. Je, bara hilo kongwe linatarajia nini kutoka katika uchaguzi wa Marekani? 

Ikiwa watu wa Ulaya wangeweza kumchagua mkuu wa taifa la Marekani Novemba 5, matokeo yangekuwa wazi. Katika nchi za Ulaya Magharibi, asilimia 69 wangempigia kura Kamala Harris, na Ulaya Mashariki, asilimia 46.

Donald Trump angepata tu asilimia 16 ya wapiga kura Ulaya Magharibi na asilimia 36, Ulaya Mashariki.

Hayo yalikuwa matokeo ya utafiti wa uwakilishi uliofanywa na taasisi za utafiti wa maoni ya wananchi za Novus na Gallup International mwezi Oktoba.

Mgombea wa chama cha Democratic alipata alama za juu zaidi nchini Denmark ambako ilikuwa asilimia 85, na Finland asilimia 82. Nchi zilizoongoza kumchagua Trump Ulaya ni Serbia asilimia 59, na Hungary asilimia 49. Nchi zote hizo mbili zinatawaliwa kimabavu.

Soma pia:Wafahamu wagombea urais Marekani na sera zao

Andras Laszlo, mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Hungary, anasema ingekuwa bora kama Trump atashinda katika uchaguzi.  Laszlo anatokea chama cha Fidesz, cha Waziri Mkuu Viktor Orban, rafiki wa Urusi.

"Wamarekani wanataka mabadiliko katika siasa za nchi hiyo. Wamechoshwa na hali iliyopo. Ni Trump tu ndiye anaweza kufanya hivyo."

Laszlo ameiambia DW kuwa mabadiliko hayo yanahitajika pia mjini Brussels. Mbunge huyo anajiuliza ikiwa Wanaweza kuzuia migogoro iliyopo isiongezeke kuwa mibaya zaidi.

Anabainisha kuwa sio tu Ukraine, lakini pia Mashariki ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.

Anaamini kuwa Trump mwenye uzoefu, anaweza kuonesha uongozi wa kimataifa na kuichukua Ulaya pamoja naye.

Hungary: Trump anaweza kuleta utulivu

Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, anaamini kwamba Trump anaweza kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine ndani ya siku chache.

Ni akina nani wengine hupigiwa kura Marekani?

01:17

This browser does not support the video element.

Steven Blockmans kutoka Kituo cha Mafunzo ya Sera za Ulaya kilichoko mjini Brussels, anasema wanasiasa wengi wa siasa kali za mrengo wa kulia na kizalendo kutoka Uholanzi hadi Ujerumani na Italia wanakubaliana na Orban.

Kulingana na Blockmans, wanaweza kuhisi kutiwa moyo na ushindi wa Trump. Mwezi Oktoba, Orban alisema katika Bunge la Ulaya, kuwa iwapo Trump atarejea madarakani, watafungua chupa kadhaa za vimnyo kusherehekea.

Hata hivyo, wakuu wengi wa nchi za Umoja wa Ulaya wanamuunga mkono Kamala Harris.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz alisema anamfahamu vyema Harris, na kwamba bila shaka atakuwa rais mzuri. Sholz alimsifu Harris katika mahojiano ya televisheni.

Blockmans anabainisha kuwa iwapo Harris atashinda kutakuwa na afueni kubwa Ulaya.

Soma pia:Uchaguzi Marekani: Harris na Trump katika kampeni za mwisho

Katika suala la usalama, Marekani iko tayari kufanya maamuzi ya kuiunga mkono Ukraine, na katika kujilinda dhidi ya vita vya Urusi.

Tineke Strik, mbunge wa Bunge la Ulaya wa chama cha Kijani kutoka Uholanzi, ameiambia DW kuwa Harris ana uwezekano mkubwa wa kuwapa watu matumaini kuliko Trump.

"Itakuwa ni ushindi mkubwa kuimarisha nguvu za kidemokrasia nchini Marekani na Ulaya."

Strik anasema kwa upande mwingine Trump, yuko na watawala wa serikali za kimabavu kote ulimwenguni. Wataimarishwa naye.

Hiyo itakuwa habari mbaya kwa demokrasi, haki za binaadamu, na ulimwengu ambao wanataka kuishi ndani yake.

Mambo ya Nje EU: Msitarajie mambo makubwa 

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Bunge la Ulaya, David McAllister kutoka Ujerumani wa chama cha CDU, ameonya dhidi ya kutarajia mambo makubwa kupita kiasi.

Amesema kama ilivyo kwa Trump, Harris pia atakuwa na matakwa ya Ulaya, kama vile kujitoa zaidi Ulaya katika usalama na ulinzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Biashara ya Bunge la Ulaya, Bernd Lange, anasema hawako tayari kuacha maslahi yao bila kupambana.

Soma pia:Putin asema Marekani itaamua yenyewe uhusiano baina yao

Lange, wa chama cha SPD kutoka Ujerumani, anasema ana uhakika baada ya uchaguzi, watatumia nyenzo zao kupambana na masuala ambayo tayari hayako sawa, kama vile ushuru usio halali katika chuma au ruzuku kutoka katika Sheria ya Marekebisho ya Mfumuko wa Bei, IRA.

Hali ya uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani

01:11

This browser does not support the video element.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Norbert Pistorius pia ana utabiri sawa na huo katika sera ya mambo ya nje na usalama.

Pistorius anasema bila shaka Ulaya itabidi kufanya zaidi, kwani vyovyote vile matokeo yatakavyokuwa, Marekani haitafanya vya kutosha kuhusu Ulaya katika siku zijazo.