EU kujadili suala tete la kikomo cha bei ya nishati
13 Desemba 2022Hii ni baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo ambayo yamefeli kusuluhisha mkwamo uliopo kati ya serikali zinazotofautiana ikiwa hatua hiyo itapunguza mgogoro wa nishati unaoikumba Ulaya kwa sasa.
Mawaziri wa nishati kutoka nchi 27 wanakutana mjini Brussels kujaribu kuboresha pendekezo la kikomo cha bei lililowasilishwa na kamisheni ya umoja huo mwezi uliopita.
Pendekezo hilo ni jibu la hivi karibuni la Umoja wa Ulaya dhidi ya mgogoro wa nishati ambao umesababishwa na hatua ya Urusi kupunguza usambazaji wa gesi kwenda Ulaya hivyo kusababisha bei ya nishati kupanda.
Nchi kama Ubelgiji, Poland na Italia zimesema kikomo hicho kinahitajika kukinga chumi zao dhidi ya bei za juu za gesi. Lakini nchi kama Ujerumani, Uholanzi na Austria zinahofia hatua hiyo inaweza kusababisha shehena za gesi zilizokusudiwa kuja Ulaya, kupelekwa kwingineko.