EU kukaza masharti ya kuuza chanjo za COVID-19
24 Machi 2021Kulingana na rasimu ambayo shirika la habari la AFP limeipata, Umoja wa Ulaya umeghadhabishwa na hatua ya Uingereza kudai kwamba tayari imeshanunua dozi za chanjo ya AstraZeneca ambazo zimetengenezwa katika kiwanda cha kampuni hiyo kilichoko Uholanzi, ilhali kiwanda cha kampuni hiyo kilichoko Uingereza kimeshindwa kutimiza ahadi yake ya kuwasilisha dozi kamili ambazo Umoja wa Ulaya uliagiza.
Huku mazungumzo yakiendelea nyuma ya pazia kati ya Umoja wa Ulaya na serikali ya Uingereza, kuepusha kitisho cha kupiga marufuku kabisa uuzaji wa chanjo zilizotengenezwa ndani ya Umoja wa Ulaya nje ya umoja huo, tayari halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeamua kukaza sheria za uuzaji nje wa chanjo.
Soma pia:
- Ujerumani kufunga kabisa shughuli wakati wa Pasaka
- Pasi ya chanjo ya EU: Changamoto ya kimaadili na kisheri?
- Waziri wa afya wa Ujerumani kuchunguzwa kashfa ya barakoa
Uhaba wa chanjo wasababisha mvutano
Sheria hiyo inayolenga kufuatilia chanjo zinazotolewa ndani ya Umoja wa Ulaya kuuzwa nje na ikibidi kuzuia uuzaji huo, imeshawahi kutumiwa mara moja wakati dozi za AstraZeneca zilizokusudiwa kutolewa Italia na kuuziwa Australia zilizuiwa.
Hata hivyo rasimu hiyo ya sheria iliyosahihishwa, pia inalalamikia nchi zinazozuia chanjo kusafirishwa kuingia Umoja wa Ulaya, kutokana na sheria au kutokana na mikataba waliyonayo na kampuni za kutengeneza chanjo.
Kampuni ya AstraZeneca imesema mkataba wake na serikali ya Uingereza unaipa Uingereza kipaumbele kupokea chanjo zake zaidi.
Ursula von Der Leyen atoa onyo kwa AstraZeneca
Akiungwa mkono na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya akiwemo kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von Der Leyen, ametaka kuwe na kile alichokitaja kuwa utimizaji wa makubaliano katika uuzaji wa chanjo huku akionya kwamba huenda kampuni ya AstraZeneca ikapigwa marufuku kuuza chanjo nje ya Umoja wa Ulaya.
Rasimu hiyo imeonya pia kwamba baadhi ya nchi ambazo kwa sasa hazina sheria za kudhibiti uuzaji wa bidhaa nje ya mipaka yao zina kiwango cha juu cha utoaji chanjo hata kushinda Umoja wa Ulaya, ama hazijaathiriwa zaidi na janga la virusi vya corona.
Kufuatia hali hiyo rasimu imesema usafirishaji wa chanjo kuelekea nchi hizo huweza kuathiri upatikanaji wa chanjo ndani ya Umoja wa Ulaya.
Boris Johnson aingiwa wasiwasi na fikra za EU
Mnamo Jumanne, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alielezea wasiwasi wake kuhusu hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya, lakini alielezea matumaini kwamba mazungungumzo yao yataleta suluhisho.
Hayo yanajiri mnamo wakati mkuu wa vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi katika hospitali ya Paris nchini Ufaransa Jean-Francois [Janfranswaa] Timsit akisema mwezi ujao utakuwa kile alichokitaja kuwa ‘maafa makubwa' kufuatia kulemewa kwa mfumo wa afya kwa sababu ya wimbi la tatu la maambukizi ya COVID-19.