1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kumimina mabilioni ya Yuro Afrika

11 Februari 2022

Umoja wa Ulaya watangaza mpango wa uwekezaji duniani ikiwemo nchi za bara la Afrika utakaojikita katika ujenzi wa miundo mbinu

Senegal Ursula von der Leyen und Präsident Macky Sall
Picha: Seyllou/Getty Images/AFP

Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa na mpango wa kuwekeza yuro bilioni 150 barani Afrika. Mpango huu umewekwa wazi katika wakati ambapo wiki ijayo kuna mkutano wa kilele kati ya viongozi wa bara hilo la Afrika na Ulaya mjini  Brussels.

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen baada ya kukutana jana na rais wa Senegal Macky Sally mjini Dakar aliweka wazi kwamba Umoja huo unataka kukusanya zaidi ya yuro bilioni 150 kwa ajili ya kuwekeza barani Afrika kupitia mpango wake maalum wa kimataifa wenye lengo la kuiunganisha jumuiya hiyo na nchi za Ulimwengu na mpango wa China wa ujenzi wa barabara.

Mpango wa ujenzi wa miundo mbinu wa China tayari umeshamwaga mabilioni ya dola katika miradi mbali mbali ya miundo mbinu duniani ikiwemo katika bara la Afrika.

Hivi sasa Umoja wa Ulaya kupitia mpango wake unalenga kusaidia kutowa mabilioni ya dola kufadhili miradi, ingawa kiwango kinachotolewa na Umoja huo nu thuluthi ya kile ambacho China imepania kukitowa kwenye mpango wake. Hata hivyo pia mpango huo mpya wa Umoja wa Ulaya haukutolewa maelezo zaidi ya kina lakini inatarajiwa ufafanuzi utatolewa katika mkutano wa Brussels kati ya viongozi wa Afrika na Ulaya utakaoanza tarehe 17 hadi 18.

Huu ni mradi wa kwanza wa kikanda wa  jumuiya hiyo ya Umoja wa Ulaya utakaogusa nchi mbali mbali za ulimwengu ikitarajiwa kukusanywa yuro bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya binafsi na ya umma kufikia mwaka 2027. 

Ukionekana kama wenye lengo la kuiga mradi wa China, mkakati hasa wa mradi huo wa Umoja wa Ulaya utakuwa ni kutumia fedha kutoka taasisi za jumuiya hiyo na kutoka  nchi wanachama kusimamia uwekezaji wa sekta binafsi.

Picha: Tony Karumba/AFP

Aidha Umoja wa Ulaya mjini Brussels umeweka lengo la mwaka 2030 kuwa muda wa kufikia mpango wake wa kufadhili miradi ya barani Afrika kwa mujibu wa nyaraka zilizotoka kwenye Halmashauri ya Umoja huo.

Pamoja na hilo tovuti ya Umoja wa Ulaya imeweka taarifa inayobaini kwamba sekta zitakazomulikiwa ni zile za usafiri pamoja na afya,elimu, utafiti,nishati isiyoharibu mazingira ili kuepusha kitisho cha majanga ya asili sambamba na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya internet. 

Akizungumza na shirika la habari la AFP von der Leyen aliweka wazi kwamba mkutano kati ya Afrika na Umoja huo utajikita zaidi kwenye suala la uwekezaji kwasababu eneo hilo hasa Bara la Afrika ndio mshirika wake wa kutegemea  lakini cha muhimu zaidi ni kwamba pande zote mbili zinathaminiana katika masuala ya uwazi,utawala bora, maendeleo endelevu pamoja na ustawi wa watu wananchi wao,huku pia  akitahadharisha kwamba mara nyingi uwekezaji wa kigeni barani Afrka  huambatana na gharama zilizojificha.

Ikumbukwe kwamba wakosoaji mara nyingi huitumu China na wawekezaji wengine wakubwa barani Afrika kama Urusi kwamba hazishughuliki kujali ulinzi wa mazingira au hata haki za binadamu zinapijiingiza katika bara hilo.

Na hasa China inakosolewa sana ikishutumiwa kuzitumbukiza nchi nyingi za bara hilo kwenye mitego ya kuogelea kwenye madeni makubwa wasioweza kuyarudisha.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW