1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kupitisha sheria ya nishati rafiki kwa mazingira

Hawa Bihoga
2 Februari 2022

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya hii leo inatarajiwa kupitisha sheria iliyopingwa vikali ambayo inaziainisha nishati za gesi asilia na nyuklia kuwa rafiki kwa mazingira chini ya mazingira fulani.

Belgien Kernkraftwerk Doel
Picha: W. Pattyn/blickwinkel/picture alliance

Rasimu ya sheria hiyo inayopendekezwa na halmashauri kuu iliyokabidhiwa kwa mataifa wanachama mnamo mwezi Desemba, imeugawa Umoja wa Ulaya, na kusababisha upinzani kutoka makundi ya mazingira na ukosoaji kutoka kwa wataalamu wa tabianchi walioshauriwa katika kutunga sheira hiyo. 

Sheria hiyo ni sasisho la uainishaji wa mfumo wa uwekezaji uliopewa jina la taxonomy, ambao unalenga kuelekeza uwekezaji binafsi katika kuusaidia Umoja wa Ulaya kufikia malengo yake ya tabianchi ya mwaka 2050, kupunguza utoaji wa gesi inayochafua mazingira kwa hadi sifuri.

Halmashauri Kuu imetetea ujumuishaji wa nyuklia na gesi kama uamuzi yakinifu ili kusaiidia mabadiliko kulekea vyanzo jadidifu vya nishati. Chini ya rasimu hiyo ya taxonomy, uwekezaji katika mimea mipya ya nishati ya gesi kabla ya mwaka 2030 unaainishwa kama rafiki wa mazingira ikiwa jumla ya gesi inayotolewa iko chini ya gramu 270 za kaboni dioksidi kwa saa ya kilowatt.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Michel Euler/Pool/REUTERS

Kwa uwekezaji katika nishati ya nyuklia kujumuishwa, mtanmbo wa umeme unapaswa kuwa na viwango vya kisasa zaidi vya teknolojia na kuwa na mpango ulioidhinishwa wa utupaji wa taka za atomiki unaofanya kazi kufikia mwaka 2050. Wakosoaji wanadai hata hivyo, kwamba hatari za muda mrefu za taka za mionzi na uharibifu wa mazingira vinazidi ukosefu wa uzalishaji wa kaboni na wanahoji kwamba nishati kama gesi hazina nafasi kabisaa katika mfumo wa taxonomy. Upinzani kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya dhidi ya taxonomu unaakisi vipaumbele vinavyotofautiana na namna mataifa yanavyozalisha nishati, ambapo serikali tofauti zimegawika kati ya kuunga mkono nyuklia, gesi au nishati jadidifu. Ufaransa ambayo ni moja ya wazalishaji wakuu wa nishati ya nyuklia duniani, ilishinikiza pakubwa mfumo wa taxonomy kujumuisha nishati ya nyuklia kwa kuungwa mkono na Poland na Hungary.

Ujerumani kwa upande mwingine ina msimamo imara wa kuunga mkono gesi lakini inapinga nyuklia na serikali mjini Berlin imesisitiza juu ya kuvifanya vigezo vya uwekezaji katika gesi kuwa vyepesi zaidi, jambo ambalo limekuwa na mafanikio fulani. Muda wa mwisho wa mwaka 2026 uliotolewa kwa viwanda vya nishati kuonyesha mabadiliko kuelekea vyanzo rafiki zaidi kwa mazingira, uliokuwepo katika rasimu ya awali ya taxonomy, hivi sasa umeondolewa.

Viwanda vipya vya gesi vinavyochukuwa nafasi ya mitambo ya zamani, havitakabiliwa na ukomo mkali wa viwango cha uchafuzi pia kulinga na rasimu hiyo. Siku ya Jumanne, Sweden ilituma barua kwa halmashauri kuu ambayo shirika la habari la Ujerumani dpa limepata nakala yake, ikipinga ujumuishaji wa shughuli zinazotokana na gesi ya kuchimbwa.

Sheria ya taxonomu itaanza kutekelezwa, isipokuwa tu kama bunge la Ulaya au Baraza la Ulaya, linalowakilisha mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, yatazawia sheria za uwekezaji katika kipindi cha miezi minne au sita ijayo. Ili kufanikisha hili, wingi wa mataifa 20 kati ya 27 wanachama, au wabunge 353 unahitajika, kihunzi kikubwa ambacho siyo rahisi kufikiwa.

Vyanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW