1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kutoa Euro bilioni 37 kukabiliana na COVID-19

13 Machi 2020

Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa Euro bilioni 37 kama sehemu ya mpango wa kusaidia juhudi za kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona.

Brüssel PK Ursula von der Leyen
Picha: Reuters/J. Geron

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema fedha hizo zitatolewa kwa nchi wanachama wa umoja huo ili kuchukua hatua kukabiliana na athari za kiuchumi kutokana na mripuko wa virusi vya corona.

Fedha hizo zitakuwa kwa ajili ya kusaidia katika uchumi na huduma za umma zinazotolewa kwenye ngazi ya kitaifa. Akizungumza na waandishi habari, Von der Leyen amesema kuwa Umoja wa Ulaya utatoa mkopo wa Euro bilioni nane kwa kampuni 100,000 ili kuiunga mkono sekta ya ushirika.

Aidha, Von der Leyen ameonya kuhusu kuweka vikwazo vya kusafiri katika kukabiliana na virusi vya corona, kama ambavyo baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo zimefanya. Kauli hiyo ameitoa baada ya Jamhuri ya Czech kutangaza kwamba itapiga marufuku raia kutoka nchi 15 ambazo zimeathirika zaidi na virusi vya corona kuingia nchini humo.

''Katika saa chache zilizopita, tumeona marufuku ya kusafiri na udhibiti wa mipaka ikitangazwa miongoni mwa nchi wanachama. Ni kweli tunataka kuwalinda raia wetu na kuzuia kuenea kwa virusi. Lakini tuangalie namna tunaweza kushirikiana pamoja kwa ufanisi mkubwa. Udhibiti wa aina hiyo unaweza kuwa sawa, lakini Shirika la Afya Duniani, halioni marufuku ya kusafiri kama njia bora zaidi,'' alisisitiza Von der Leyen.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Olaf Scholz Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Serikali ya Ujerumani imeahidi kutoa mkopo usio na kikomo kwa biashara ambazo zimeathirika na mripuko wa virusi vya corona. Mkopo huo ni sehemu ya Euro bilioni 460 ambazo iliahidi kusaidia kukabiliana na athari za kiuchumi kutokana na janga hilo la kimataifa. Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema hakutakuwa na kikomo cha kiwango ambacho serikali itatoa ili kuwasaidia watu binafsi pamoja na kampuni ili kukabiliana na athari za kiuchumi zitokanazo na virusi vya corona.

Wakati huo huo, jimbo la North Rhine Westphalia nchini Ujerumani limetangaza kuwa shule zake zote zinapaswa kufungwa ifikapo Jumatano ijayo hadi mwishoni mwa likizo ya Pasaka, katikati ya Aprili.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Ujerumani ya Afya, Robert Koch, jimbo hilo lenye idadi kubwa ya watu nchini Ujerumani lina visa vingi vya COVID-19 ambako hadi sasa zaidi ya wagonjwa 680 wamethibitishwa, huku watu watatu wakiwa wamefariki.

Uhispania imeamuru leo kufungwa kwa lazima shughuli zote za umma katika manispaa nne za jimbo la Catalonia ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Huduma katika manispaa hizo zenye jumla ya watu 60,000, zimefungwa kwa wiki mbili.

Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani, ZMD limeiamuru misikiti yote kusitisha huduma za sala ya Ijumaa. Nalo shirika la reli nchini Ujerumani limesema litasitisha usafiri wa moja kwa moja wa treni kwenda Italia. Njia inayotumika kutoka Frankfurt kupitia kusini magharibi mwa Ujerumani na Uswisi hadi Milan, itasitishwa hadi Aprili 13.

(DPA, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/2U0rFmB)