1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

EU kutuma mjumbe kuzungumza na viongozi wapya wa Syria

16 Desemba 2024

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema mjumbe maalum wa umoja huo anaelekea Damascus kuzungumza na watawala wapya wa Syria.

Kaja Kallas | Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya
Kaja Kallas asisitiza kwamba wanachotaka kuona zaidi kama Umoja wa Ulaya "si maneno ambayo watawala wapya wa Syria wanasema bali ni matendo yanayofuata mwelekeo sahihi”Picha: Alaa Al Sukhni/REUTERS

Nchi za Magharibi zimeimarisha mazungumzo na taifa hilo tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad alipoondolewa mamlakani.

Juhudi za mazungumzo za Umoja wa Ulaya na Syria, zinajiri baada ya Marekani na Uingereza pia kusema wamewasiliana na mamlaka mpya huko Damascus, inayoongozwa na kundi la waasi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS).

Mataifa yenye nguvu ya kikanda na kimataifa yako mbioni kuimarisha ushawishi nchini Syria baada ya Assad kupinduliwa katika mashambulizi yaliyofanywa kwa kasi, na yaliyomaliza miongo mitano ya utawala wa familia yake nchini Syria.

Kama mataifa mengine ya Magharibi, mataifa ya Umoja wa Ulaya yana wasiwasi na uongozi mpya mjini Damascus, ikizingatiwa kwamba kundi la waasi wa Hayat Tahrir al-Sham (HTS) ina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda na serikali nyingi pia zimeliorodhesha kama kundi la kigaidi.

EU kujadili mahusiano yao na uongozi mpya wa Syria

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels-Ubelgiji, katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas amesema watajadili jinsi mahusiano yao yatakavyokuwa na uongozi mpya wa Syria na katika kiwango gani.

Soma pia: Mjumbe wa UN Syria ataka vikwazo viondolewe baada ya Assad

Kallas aliyechukua wadhifa wake mwezi huu amesema hawawezi kuacha "ombwe” nchini Syria. Ameongeza kuwa "Syria inakabiliwa na mchanganyiko wa mustakabali wenye matumaini, lakini pia usiokuwa wa hakika. Inabidi tuhakikishe kuwa taifa hilo linakwenda katika mwelekeo sahihi."

Umoja wa Ulaya ulivunja uhusiano wake na utawala wa Assad katika kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, lakini umoja huo umesalia kuwa mfadhili wa misaada ya kiutu kuwasaidia raia.

Jumuiya ya kimataifa imeelezea mustakabali wa matumaini nchini Syria lakini kwa tahadhari, mnamo wakati utawala changa wa Damascus ukiapa kuyalinda makundi ya walio wachache na kuunda serikali shirikishi.

Ahmed al-Sharaa, kiongozi wa kundi la waasi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) nchini SyriaPicha: Aref Tammawi/AFP/Getty Images

Uongozi mpya Syria kuyapokonya silaha makundi yote

Mnamo Jumapili, Ahmed al-Sharaa, kiongozi wa waasi wa Syria aliahidi kuyapokonya silaha makundi yote yenye nchini humo na kuupa ujenzi upya wa Syria kipaumbele.

Unaweza pia kusoma: Blinken asema raia wa Syria wanahitaji kulindwa

Wanadiplomasia wanasema baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zinataka ushirikiano na Syria baada ya Assad kuondolewa madarakani lakini nyingine zina tahadhari zaidi.

Kallas amesisitiza kwamba wanachotaka kuona zaidi kama Umoja wa Ulaya "si maneno ambayo watawala wapya wanayasema bali ni matendo yanayofuata mwelekeo sahihi”.

Kulingana na Kallas, wiki au miezi ijayo itatoa taswira kamili ikiwa Syria imechukua mwelekeo sahihi au la.

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

01:45

This browser does not support the video element.

Mashambulizi ya Israel yapiga "maghala ya silaha" Syria

Hayo yakijiri shirika la haki za binadamu lenye makao yake Uingereza limesema mashambulizi ya anga ya Israel mapema Jumatatu yamelenga maghala ya makombora nchini Syria na kuyaita "mashambulizi makali zaidi" tangu 2012.

Unaweza kusoma pia: Iran yazishutumu Israel, Marekani kwa anguko la Assad

Israel imekuwa ikipiga "maeneo ya kijeshi nchini Syria" baada ya kuporomoka kwa utawala wa Rais Bashar Assad.

Katika tukio jingine, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Geir Pedersen, amesema umoja wake unakusudia kutoa kila aina ya msaada kwa watu wa Syria. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Pedersen siku ya Jumatatu.

(APE; AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW