1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kuwazuia wasafiri wa kigeni ili kukabiliana na COVID-19

18 Machi 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuweka mara moja marufuku ya kusafiri kwa raia wa kigeni wanaoingia Ulaya kwa muda wa siku 30 ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Deutschland Grenze zu Frankreich in Saarbrücken | Coronavirus | Grenzschließung
Picha: Reuters/R. Orlowski

Umoja huo pia umeanzisha usafiri wa haraka kwa ajili ya kusafirisha vifaa muhimu vya matibabu, chakula na bidhaa nyingine, ili kurahisisha usambazaji wake ndani ya nchi wanachama.

Wakati ambapo visa vya COVID-19 vikiwa vimeongezeka barani Ulaya hadi kufikia zaidi ya wagonjwa 60,000 na zaidi ya vifo 2,700 viongozi wa nchi hizo wamechukua hatua mbalimbali kama vile kuifunga mipaka yao. Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano wao uliofanyika kwa njia ya video na kudumu kwa zaidi ya saa tatu na kuungana pamoja katika juhudi za kuvidhibiti virusi hivyo ambavyo vimesababisha hasara za kiuchumi.

Umuhimu wa kuungana

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema viongozi hao wameelezea umuhimu wa kushirikiana kufanya kila linalowezakana kukabiliana na janga la virusi vya corona pamoja na athari zake. Amesema nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuweka vizuizi vya mpakani haraka iwezekanavyo katika sekta ya utalii na biashara nyingine zisizo muhimu. Amesema mpango huo hautowahusisha wakaazi wa muda mrefu wa Umoja wa Ulaya, wanadiplomasia pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa afya na usafiri.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema pendekezo lake la kuweka vikwazo vya kuingia kwenye nchi za umoja huo limepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa nchi wanachama. Amesema sasa ni jukumu la nchi hizo kulitekeleza na kwamba wameahidi kufanya hivyo mara moja.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel Picha: Reuters/J. Geron

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema baada ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kukubaliana kuhusu kuweka marufuku ya kusafiri kwa raia wasio wa Ulaya, nchi yake itaanza kulitekeleza hilo haraka iwezekanavyo. Merkel amesema raia wa Uswisi, Liechtenstein, Uingereza na Norway hawatohusika katika marufuku hiyo.

Kwa mujibu wa Merkel, viongozi hao pia wamekubaliana kuratibu zoezi la kuwarejesha nyumbani raia wa Umoja wa Ulaya ambao wamekwama kwenye nchi zilizo nje ya umoja huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema operesheni ya kuwaondoa raia wa Ujerumani waliokwama nje ya nchi imeanza. Akizungumza na DW, Maas amesema maelfu ya Wajerumani wanatarajia kurejeshwa nyumbani kutokana na hoteli kufungwa na mashirika ya ndege kufuta safari zake.

Ndege 40 kuwachukua watalii wa Kijerumani

Maas amesema Euro milioni 50 zimetengwa kwa ajili ya operesheni hiyo itakayochukua siku kadhaa. Amesema kuwa watalii wa Kijerumani wapatao 35,000 wako nchini Misri, 4,000 hadi 5,000 wako Morocco na maelfu wengine wako kwenye nchi kadhaa kama vile Ufilipino, Argentina na Maldives. Tayari ndege 40 zimeelekea katika maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya kuwachukua watalii hao na kuwarejesha nyumbani.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na nchi tisa duniani ikiwemo Ujerumani imezitolea wito pande zinazohasimiana katika mzozo wa Libya kusitisha mapigano mara moja ili kuwaruhusu maafisa wa afya kukabiliana na virusi vya corona. Taarifa hiyo imeeleza kuwa kumalizwa kwa uadui kutasaidia pia makamanda kurejea nyumbani na kuwahudumia ndugu zao ambao huenda wakawa katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko MaasPicha: Imago Images/photothek

Uturuki imetangaza kifo cha kwanza kilichotokana na virusi vya corona. Waziri wa Afya wa Uturuki, Fahrettin Koca amesema mgonjwa aliyefariki alikuwa na umri wa miaka 89. Ubelgiji imeamua kutangaza kusimamisha shughuli zote za kijamii kwa muda wa wiki tatu ili kuwazuia watu kuondoka majumbani mwao. Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Sophie Wilmes amesema wananchi watakaoruhusiwa kutoka nje ni wanaokwenda kununua mahitaji muhimu, kupata huduma za afya, wanaokwenda kazini na katika biashara muhimu kama vile maduka ya vyakula na dawa.

G20 kukutana

Wakati hayo yakijiri, wakuu wa mataifa yenye nguvu kiuchumi, G20 wanatarajia kukutana wiki ijayo kuzungumzia jinsi ya kukabiliana na janga la virusi vya corona. Saudi Arabia, ambayo inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo, imesema kwamba wanasiasa watajadiliana kuhusu hatua za kuchukua kuwalinda raia wao na kusaidia uchumi.

Uingereza kwa upande wake imetenga Pauni bilioni 330 za mkopo, ukiwa ni mpango mkubwa wa nchi hiyo katika kuukoa uchumi wake tangu mwaka 2008 wakati wa mzozo wa kiuchumi. Nia ya kutenga fedha hizo ni kuzisaidia biashara zilizoathirika kutokana na virusi vya corona.

Jimbo la West Virginia nchini Marekani limethibitisha kisa cha kwanza cha COVID-19. Kisa hicho kinamaanisha kuwa majimbo yote 50 ya Marekani yameathirika kwa virusi vya corona.

Watu 197,168 ulimwenguni wamethibitika kuambukizwa virusi hivyo, huku vikiripotiwa vifo 7,905. Watu wengine 80,840 wamepona ugonjwa huo.

(DPA, AP, DW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW