EU kuzindua mfumo wa pamoja wa usimamizi wa fedha
19 Juni 2009Viongozi hao wameziunga mkono juhudi za Jose Manuel Barosso kuwania muhula wa pili wa miaka mitano wa urais wa Kamisheni ya Umoja huo.Kwa upande mwengine kikao cha Umoja huo cha leo kinajadili mbinu za kuuidhinisha mkataba wa Lisbon uliopingwa vikali na Ireland mwaka uliopita.Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kikao cha Umoja huo kilichomalizika kuchelewa jana usiku.Uingereza kwa upande wake inaripotiwa kuwa ilikuwa inatiwa shaka na mpango huo mpya wa kuwateua wasimamizi maalum katika sekta ya fedha.
Kwa mujibu wa rasimu ya taarifa hiyo iliyochapishwa na Shirika la habari la Reuters Baraza la Umoja wa Ulaya lilipitisha maamuzi kadhaa yaliyo na azma ya kuulinda mfumo mzima wa fedha barani Ulaya ili kulilinda kutoaathiriwa tena na mitikisiko katika sekta hiyo.Mapendekezo hayo yanajumuisha uzinduzi mwaka ujao wa taasisi tatu za uangalizi zitakazoanzisha sheria mpya za usimamizi wa taasisi za fedha pamoja na kuteuliwa kwa Bodi maalum itakayotathmini uwezekano wa hasara kutokea.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya Marekani kutangaza mabadiliko makubwa ya usimamizi wa yake ya fedha ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika miaka ya thelathini
''Napendekeza kwamba benki kuu ya Marekani iwe na mamlaka makubwa zaidi na iwajibike kuzisimamia taasisi za benki na fedha ambazo huenda zikakabiliwa na tishio la kufilisika na kuuvuruga uchumi mzima.Kadhalika tutaziimarisha ili tupunguze uwezekano wa kufilisika.'' alieleza Rais Obama
Rasimu hiyo inaeleza bayana kuwa maamuzi yatakayopitishwa na taasisi hizo mpya sharti yasiilazimishe nchi yoyote mwanachama kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuyaokoa mabenki yanayokabiliwa na hatari ya kufilisika.Uingereza ilihofia kwamba taasisi zake za usimamizi wa kitaifa wa sekta hiyo huenda zikashindwa kuutimiza wajibu wake ndiposa ilipinga mpango wa kuiidhinisha Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya kuisimamia bodi maalum ya tathmini.Waziri Mkuu Gordon Brown anaeleza kuwa ''Tulilazimika kuchukua hatua kwa pamoja na mabenki ya Scotland ,Lloyds TSB na Northern Rock kwasababu ni pesa zetu za umma za Uingereza ndio maana tukafanya hivyo.Kwahiyo uamuzi wowote wa kifedha kwa maoni yangu sharti upitishwe na taasisi iliyo na uwezo wa kufanya hivyo.''
Rasimu hiyo kadhalika imeeleza kuwa wanachama wa Baraza la Benki ya Umoja wa Ulaya ECB ndiwo watakaomteua mwenyikiti wa Bodi maalum ya tathmini.Hata hivyo rasimu hiyo inaweza kubadilishwa tena hii leo ikihitajika watakapokutana viongozi hao.Wakati huohuo Umoja wa Ulaya uko katika harakati za mwisho za kuandaa mikakati itakayowashawishi wapiga kura wa Ireland kuuidhinisha mkataba wa Lisbon uliokwama.Ireland iliupinga mkataba huo mwaka uliopita.Kwa mujibu wa rasimu ya wanadiploamasia wa Umoja huo kikao hicho kitawapa wapiga kura wa Ireland hakikisho la kisheria kuwa masuala wanayopa kipa umbele hayatoathiriwa na utekelezaji wa mkataba wa Lisbon.Hii ni kwasababu mkataba huo unaenda sambamba na mkataba uliopo wa Umoja wa Ulaya kwahiyo hakutakuwa na haja ya kuuidhinisha tena uamuzi wa kutekeleza mkataba wa Lisbon.Suala linalozua utata ni utekelezaji wenyewe wa hakikisho hilo la kisheria.Ireland inawataka viongozi wa Umoja wa Ulaya kuiunga mkono rasimu hiyo kama uamuzi rasmi wa kikao hicho utakaoidhinishwa rasmi kama itifaki ya mikataba ya msingi ya Umoja huo.Kimsingi hatua hiyo inaiidhinisha kisheria rasimu ya mkataba huo.Hata hivyo mataifa mengi wanachama wa Umoja huo hawajaridhia hatua hiyo ambayo huenda ikaufungua mpya mjadala kuhusu mkataba wa Lisbon uliozua mitazamo tofauti.Suala hilo bado linaendelea kujadiliwa hii leo na viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Kwa upande mwengine viongozi wa Umoja huo wamemuunga mkono Jose Manuel Barosso anayewania muhula wa pili wa miaka mitano wa urais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya.Bwana Barosso aliye na umri wa miaka 53 anasubiri ridhaa ya Bunge la Umoja wa Ulaya litakalokutana mwezi ujao.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya RTRE/AFPE
Mhariri:Josephat Charo