1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU: Mapigano ya kuwania Karabakh yasitishwe

2 Oktoba 2020

Viongozi wakuu wa nchi na serikali za Umoja wa Ulaya wametowa mwito leo Ijumaa wa kusitishwa mara moja mapigano na vurugu ambazo zimekuwa zikishuhudiwa hivi karibuni kati ya majirani wawili,Azerbaijan na Armenia.

Brüssel EU Sondergipfel Merkel Orban
Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wakihudhuria mkutano wa kilele mjini BrusselsPicha: Johanna Geron/dpa/picture-alliance

Nchi hizo mbili Azerbaijan na Armenia zinagombania eneo lililojitenga linalofahamika kama Nargono Karabakh.

Na katika kipindi cha siku za karibuni zimeonekana kuongeza mapambano kila upande wa kuliwania jimbo hilo ambalo kwa miongo linadhibitiwa na vikosi vya Armenia nchi ambayo inahodhiwa na wakristo lakini jumuiya ya Kimataifa inalitazama jimbo hilo kama sehemu ya Azerbaijan nchi ambayo idadi kubwa ya wakaazi wake ni Waislamu.

Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, Baraza la Jumuiya hiyo mjini Brussels limetowa taarifa likisema kuangamia kwa maisha ya watu na athari kubwa kwa raia wa kawaida ni kitu kisichokubalika.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya pia imeweka wazi kwamba hakuna suluhisho la kijeshi katika mgogoro huu wa Azerbaijan na Armenia bali nchi hizo zinapaswa kuingia kwenye mazungumzo ya dhati bila ya kutowa masharti.

Kadhalika kwa mujibu wa taarifa hiyo,mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell ataangalia uwezekano wa njia ya Umoja wa Ulaya kutowa msaada katika suala hili.

Putin, Trump na Macron walishatoa wito wa kuwepo utulivu 

Ufaransa, Marekani na Urusi nazo zimetowa taarifa ya pamoja jana Alhamisi na kutowa mwito wa kutaka vita visitishwe na kulaani kuongezeka kwa vurugu.

Picha: Armenian unified info centre/Reuters

Ofisi ya rais Putin wa Urusi na Macron wa Ufaransa zimesema zinawasiwasi juu ya ripoti za Uturuki kuwapelekwa  wapiganaji wakisyria huko Karabakh.

Kwa upande mwingine Uturuki imesema itafanya kila juhudi kusiadia mshirika wake wa jadi Azerbaijan ingawa imekanusha taarifa kwamba imepeleka mamluki kuisadia nchi hiyo.

Ikumbukwe kwamba hadi sasa inaripotiwa kwamba watu 100 ikiwemo raia wengi wameuwawa katika mapigano hayo yaliyoanza siku ya Jumapili.

Hayo ni mapigano yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka minne iliyopita,kati ya majirani hao wawili waliowahi kuwa chini ya muungano wa kisovieti.

Jeshi la Armenia limesema limezidungua ndege nne zisizo na rubani zilizokuwa zikizunguuka anga yake karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Yerevan,jana usiku katika wakati ambapo mapigano yalikuwa yameingia siku yake ya tano.

Viongozi wa pande mbili bado wanapuuza miito ya kufanya mazungumzo 

Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan ameandika kwenye Twitta ujumbe akisema ndege hizo zilidunguliwa katika mikoa ya Gegharkunik na Kotayak na zote kuangushwa.

Picha: Azerbaijan Defence Ministry/Anadolu Agency/picture alliance

Ndege hizo zimedaiwa kuwa za Azerbaijan.Lakini pia shirika la habari la Urusi Interfax limeripoti kwamba wizara ya ulinzi ya jimbo la Nargono-Karabakh imesema wanajeshi 54 wameuwawa leo ijumaa na kuifanya idadi ya waliuuliwa kuwa 158.

Licha ya viongozi wa jumuiya ya Kimataifa kutowa mwito kwa pande zote mbili kuacha vita na kuingia kwenye mazungumzo,waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan na kiongozi wa Azerbaijana Ilham Aliyev wote wamekataa pendekezo la kufanya mazungumzo huku waziri mkuu huyo wa Armenia akisema Jimbo la Nagorno Karabakh haliwezi kuweka chini silaha kwasababu hatua hiyo itasababisha maangamizi makubwa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Gakuba, Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW