1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

EU, Marekani: Tutajibu ikiwa Iran inapeleka makombora Urusi

10 Septemba 2024

Umoja wa Ulaya umesema umepokea taarifa za kuaminika za kiintelejensia kutoka washirika wake zinazoonesha kwamba Iran imeipatia Urusi makombora ya masafa.

Moja ya makombora ya masafa yanayoundwa na Iran
Moja ya makombora ya masafa yanayoundwa na Iran.Picha: Vahid Reza Alaei/Iranian Defense Ministry/AP Photo/picture alliance

Hayo yameelezwa na msemaji wa Umoja wa Ulaya Peter Stano. "Tunazo habari juu ya taarifa za kuaminika zilizotolewa na washirika wetu za kupelekwa kwa makombora ya masafa marefu ya Iran nchini Urusi," amesema afisa huyo.

Ameongeza kusema kwamba viongozi mjini Brussels wanazifuatilia kwa karibu taarifa hizo na iwapo itathibitika umoja huo utachukua hatua kali na za pamoja za kuiadhibu Iran.

Washington nayo imetoa matamshi sawa na hayo ikisema imejiandaa kuchukua hatua zitakazoiathiri Iran.

Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani viliripoti wiki iliyopita kwamba Washington inaamini Iran imeipelekea Urusi silaha za kutumia kwenye vita dhidi ya Ukraine.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya na Marekani wamesema ikiwa taarifa hizo ni sahihi itakuwa ni kutanuka pakubwa kwa msaada wa Tehran kuelekea Urusi katika uvamizi wake wa kijeshi nchini Ukraine.

Iran yakanusha madai ya kupeleka silaha Urusi huku Moscow ikijizuia kutoa jibu la moja kwa moja

Iran tayari inasambaza droni chapa Shahed kwa Urusi.Picha: Middle East Images/picture alliance

Iran imekanusha taarifa hizo lakini Urusi bado haijatoa matamshi ya wazi ya kupinga madai hayo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Iran Nasser Kanani amesema kwenye mkutano wa kila wiki na waandishi habari: "Tunakanusha vikali madai ya kuihusisha Iran na upelekaji silaha upande mmoja wa vita."

Kwa upande wake Urusi haikutoa tamko lolote la kukanusha madai hayo siku ya Jumatatu hata pale msemaji wa ikulu ya nchi hiyo alipoulizwa moja kwa moja juu ya ripoti za jarida la Wall Street kwamba Iran imeipatia Moscow makombora.

"Tumeiona hiyo ripoti, siyo kila wakati aina hii ya taarifa huwa za kweli," amesema msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov.

"Iran ni mshirika wetu muhimu, tunaimarisha mahusiano yetu ya kibiashara na kiuchumi, tunatanua ushirikiano wetu na mashauriano kwenye maeneo yote yanayowezekana, ikiwemo yale yaliyo nyeti kabisa."

Ukraine yaionya Iran juu ya "kupwaya mahusiano" iwapo taarifa za kupeleka makombora Urusi ni za kweli

Rais Volodomymyr Zelensky wa Ukraine.Picha: Heiko Becker/REUTERS

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya kigeni ya Ukraine imesema imemwita mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran kumwonya kuhusu "taathira kubwa na zisizorekebishika" katika mahusiano baina ya nchi hizo mbili iwapo ripoti kwamba Tehran imeipatia Urusi makombora ya masafa zitakuwa za kweli.

Wizara imeandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba imemwita mkuu wa kituo cha uwakilishi wa ubalozi wa Iran Shahriar Amouzegar kumtahadhirisha kwa matamshi makali juu ya athari katika mahusiano ya mataifa hayo iwapo habari hizo zitathibitika.

Kwa miezi kadhaa sasa mataifa ya magharibi yamekuwa yakiionya Iran dhidi ya kupeleka makombora nchini Urusi, na Umoja wa Ulaya tayari ulikwisha iadhibu nchi hiyo kwa vikwazo kutokana na uamuzi wake wa kuipatia Moscow ndege zisizo na rubani kuzitumia katika vita vya Ukraine.

"Upelekaji wowote wa makombora ya masafa ya Iran nchini Urusi utadhihirisha kutanuka kwa uungaji mkono wa Iran katika vita vya Urusi nchini Ukraine," amesema msemaji wa wizara ya mambo nje ya Marekani Vedant Patel alipozungumza na waandishi habari.

"Tumeweka bayana kabisa ... kwamba tumejitayarisha kutoa adhabu inayostahili."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW