EU, Marekani zashitushwa na uvunjaji wa haki Madagascar
17 Oktoba 2023Upinzani unapinga mpango wowote wa kusalia madarakani kwa rais anayeondoka, Andry Rajoelina.
Katika taarifa ya pamoja, wawakilishi wa Umoja wa Ulaya, mashirika ya kimataifa pamoja na nchi nyingine saba zikiwemo Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Japan, wameelezea wasiwasi wao kufuatia hali ya mvutano wa kisiasa nchini Madagascar, huku wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa kujieleza na kukusanyika na kutoa wito kwa pande zote kushiriki katika mazungumzo.
Soma zaidi: Rais wa Madagascar ajiuzulu ili kugombea muhula wa pili
Wiki iliyopita, Mahakama ya juu nchini humo iliahirisha uchaguzi huo kwa wiki moja hadi Novemba 16, baada ya mgombea urais kujeruhiwa katika moja ya maandamano ya karibu kila siku katika kipindi cha wiki mbili, ambayo yamekitikisa kisiwa hicho kilichopo katika Bahari ya Hindi.