EU: Msimamo kuhusu makaazi ya walowezi hautobadilika
19 Novemba 2019Washington imesema haizingatii tena kuwa ujenzi huo unakiuka sheria za kimataifa.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema msimamo wa umoja huo kuhusu sera ya maakazi ya Israel hautobadilika kwa kuwa inakwenda kinyume na sheria za kimataifa.
Mogherini amesema sera hiyo ya Israel inaweka kizingiti juu ya uwezekano wa kupatikana suluhisho la mataifa mawili pamoja na amani ya kudumu kwenye mzozo kati ya taifa hilo na Palestina.
Matamshi yake yamekuja baada ya Marekani kutangaza jana kuunga mkono haki ya Israeli ya kujenga makazi ya wayahudi kwenye eneo inalolikalia kwa nguvu la ukingo wa magharibi.
Tangazo hilo lililotolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo lilisema Marekani imefikia hitimisho kwamba sera ya Israel kuhusu makaazi ya walowezi haiendi kinyume na sheria za kimataifa.
Wakati wa mkutano wake na waandishi habari mjini Washington Pompeo amesema utawala wa Donald Trump unabadili sera ya utawala wa Barack Obama kuelekea suala la makaazi ya walowezi wa Israel.
"Hatushughulikii wala kutoa uamuzi wa mapema kuhusu hatma ya ukingo wa magharibi. Hilo ni kwa waisraeli na wapelestina kujadiliana. Sheria ya kimataifa hailazimishi matokeo wala haiweki kizingiti cha kisheria kwa suluhuisho lililofikiwa baada ya majadiliano" Alisema Pompeo.
Kulingana na Pompeo matamshi ya Marekani kuhusu suala la makaazi ya walowezi yamekuwa yakitofautiana.
Amesema mwaka 1978 rais wa zamani Jimmy Carter alihitimisha kuwa ujenzi huo ni kinyume cha sheria ya kimataifa lakini rais Ronald Reagan alisema mwaka 1981 kuwa makaazi hayo hayakiuki sheria.
Marekani imeipa kisogo sera yake ya miongo kadhaa
Kwa uamuzi huo, Marekani imeipa kisogo sera yake ya karibu miongo minne iliyobainisha kuwa ujenzi wa makaazi kwenye eneo hilo unakiuka masharti ya sheria ya kimataifa.
Kadhalika tangazo hilo limefikisha idadi ya maamuzi matatu makubwa chini ya utawala wa Rais Donald Trump ambapo Marekani imeegemea na kuipendelea Israel na kupuuza misimamo ya Palestina na mataifa ya kiarabu.
Uamuzi huo wa Marekani ni ushindi kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anayehangaika kusalia madarakani baada ya chaguzi mbili zilizoshindwa kumwezesha kuunda serikali.
Netanyahu aliusifu msimamo huo mpya wa Marekani ambao hata hivyo umewakasirisha wapalestina wanaozingatia ujenzi wa makaazi kwenye ardhi ya ukingo wa magharibi ni kinyume na sheria.
Mpatanishi mkuu wa Palestina kwenye mazungumzo ya amani Saeb Erekat ameitaja hatua hiyo ya Marekani kuwa inayorudisha nyuma kanuni za kimataifa za kutatua mizozo kwa njia za amani.