EU na Japan kuzidisha mbinyo dhidi ya Urusi
12 Mei 2022Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida, amefanya mazungumzo hii leo mjini Tokyo na rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pamoja na rais wa Tume ya Ulaya Charles Michel. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Kishida amesema kuwa Japan inaunga mkono vikwazo vikali dhidi ya Urusi na kuongeza kuwa "usalama wa ulaya na kanda ya bahari ya Hindi-Pasifiki hauwezi kutenganishwa"Kansela Scholz wa Ujerumani asifu msaada wa Japan kwa Ukraine
"Uvamizi wa Urusi kwa Ukraine unatikisa misingi ya utulivu wa kimataifa, sio tu Ulaya lakini pia Asia, na hii haikubaliki kabisa. Kwa ushirikiano na G7 pamoja na Umoja wa Ulaya, Japan itatekeleza vikwazo vikali dhidi ya Urusi na kuimarisha uungaji mkono kwa Ukraine."
Naye rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema wanataka kuwajibika zaidi katika eneo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa Ulaya. Ameongeza kuwa "vita vya kikatili" dhidi ya Ukraine vimeibua wasiwasi juu ya kuongezeka kwa ushawishi na matarajio ya China.
"Indo-Pacific ni eneo linalostawi. Pia ni eneo la mivutano. Ukichukulia hali ya Mashariki na Kusini mwa Bahari ya China au tishio la mara kwa mara la Korea Kaskazini. Kama tulivyojadili Waziri Mkuu Kishida, Umoja wa Ulaya unataka kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kanda ya Indo-Pacific," alisema von der Leyen.
Tokyo iliungana na Umoja wa Ulaya na kundi la nchi saba tajiri duniani kutangaza vikwazo vya kibiashara dhidi ya Urusi, vikwazo ambavyo vimebana uwezo wa Urusi kuuza nje mafuta na gesi yake. Hata hivyo Japan inategemea zaidi uagizaji wa nishati ikiwemo ununuzi kutoka Urusi. Wiki iliyopita waziri Mkuu Kishida alisema kwamba Japan, itapiga marufuku mafuta ya Urusi lakini imekuwa ikisita zaidi kuachana na baadhi ya miradi.EU na Japan zafikia makubaliano makubwa ya biashara
Mbali na suala hilo la Ukraine, pande hizo mbili zimekubaliana pia kuongezea ushirikiano katika masuala ya dijitali na teknolojia, usalama wa mtandaoni na teknolojia ya akili bandia. Ushirikiano wa kidijitali baina ya Umoja wa Ulaya na Tokyo ni wa kwanza na wa aina yake baina ya muungano huo na nchi nyingine.