EU na mataifa ya Ghuba zazungumzia migogoro na ushirikiano
16 Oktoba 2024Viongozi wamataifa ya Ghuba akiwemo Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman wanakutana na wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels hii leo Jumatano kwenye mkutano unaolenga kuepusha balaa katika Mashariki ya Kati.
Mkutano huo pia unalenga kuuongeza nguvu uhusiano wa pande hizo mbili ili uwe wa kimkakati zaidi na hatua hiyo ni kwa sababu Umoja wa Ulaya unatambua ushawishi wa nchi hizo hasa katika migogoro ya Mashariki ya Kati na Ukraine.
Nchi hizo ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia and the Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Soma Zaidi: Mawaziri wa EU wagawika kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen atashiriki katika mkutano huo wa kilele utakaoongozwa na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, na Amiri wa Qatar Sheik Tamim bin Hamad Al-Thani.
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema mkutano huu wa pande mbili unnaonyesha na unathibitisha dhamira ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano mwema na ushirikiano wa kimkakati.
Borrell amesema ushirikiano wa nchi za Umoja wa Ulaya na nchi za Kiarabu utazingatia pia maswala ya uwekezaji, nishati mbadala, usalama wa kikanda na masuala ya viza kwa raia wa nchi husika.
Umoja wa Ulaya unawataka washirika wa nchi za Kiarabu kukubaliana kwa sauti moja ingawa hautarajii nchi hizo kutoa tamko sawa na la Umoja wa Ulaya la kuilaumu Urusi kutokana na mashambulio yake ya kijeshi nchini Ukraine. Kambi hizo mbili hata hivyo zinakaribiana kimtazamo katika swala la Mashariki ya Kati.
Soma Zaidi: Hofu yatanda Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya Iran
Umoja wa Ulaya katika jitihada zake za kuwasogeza karibu washirika wake wa kikanda, umeshafanya mikutano na nchi za kambi ya ASEAN, Jumuiya ya Karibiki na nchi za Amerika Kusini (CELAC).
Vyanzo: RTRE/AFP