1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhamiajiPoland

EU, Ujerumani zaitaka Poland kujieleza kuhusu rushwa ya visa

20 Septemba 2023

Umoja wa Ulaya pamoja na Ujerumani zimeishinikiza serikali ya Poland kutoa ufafanuzi kuhusu kashfa kubwa katika suala la utoaji wa visa, ambalo linaweza kuathiri majirani zake.

Europa-Schengen-Visum im Reisepass
Picha: Nikolai Sorokin/Zoonar/picture alliance

Ripoti za vyombo vya habari vya Poland zimebaini kuwepo kwa mfumo wa rushwa unaoendeshwa na balozi za Poland kwa watu kutoka barani Afrika na Mashariki ya Kati wanaohitaji kuingia katika eneo linajumuisha mataifa 26 ya Ulaya maarufu kama "Schengen".

Katika wakati ambapo mvutano umekuwa ukiongezeka ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu suala la uhamiaji, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser alimpigia simu mwenzake wa Poland Mariusz Kaminski siku ya Jumanne huku Balozi wa Warsaw mjini Berlin akiitwa mara moja kuelezea mkasa huo.

Soma pia: Wahamiaji wanaotafuta ajira waongezeka Ulaya Mashariki

Wakati wa mazungumzo hayo, Ujerumani imeitaka Poland kutoa "ufafanuzi wa haraka na uliokamilika" kuhusu tuhuma hizo. Ripoti zimebaini kuwa Balozi za Poland na mashirika kadhaa yaliyopo katika eneo hilo, yamekuwa na mfumo wa rushwa katika utoaji visa kwa watu wa Afrika na Mashariki ya Kati.

Waziri wa mambo ya Ndani wa Poland, Mariusz Kaminski Picha: Wojciech Olkusnik/PAP/picture alliance

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani Mehmet Ata ameelezea hasa kilichozungumzwa: " Majadiliano hayo yalilenga kufahamu muda na idadi ya visa zilizotolewa na uraia wa wale waliopewa visa, pamoja na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Poland."

Maswali ya Berlin yamesababisha ghadhabu kutoka kwa Waziri Kaminski, ambaye ametupilia mbali madai hayo na kuyaita "ya kipuuzi", na kusema kwa bahati mbaya, vyombo vya habari vya Ujerumani vimejikita katika suala hilo alilosema ni kampeni ya upinzani na kwamba wanalishughulikia.

Huenda idadi kubwa ya watu walipewa visa kuingia Poland

Mamlaka ya Warsaw inasema mkasa huo huenda umehusisha utoaji wa mamia ya visa kwa watu waliodhamiria  kufanya kazi nchini Poland, huku upinzani nchini humo ukidai kuwa idadi halisi inaweza kufikia karibu watu 250,000 waliopewa visa kwa njia ya udanganyifu baada ya kutoa rushwa.

Soma pia: Poland kuandaa kura ya maoni Oktoba kuhusu sera ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya

Siku ya Jumatano, Tume ya Ulaya imeipa Poland muda wa wiki mbili kutoa "ufafanuzi" kuhusu tuhuma hizo, ambazo imesema zinaibua "wasiwasi mkubwa".

Vyombo vya habari vya Poland vimeripoti kuwa wizara ya mambo ya nje ilihusika katika mpango huo, ambao chama cha upinzani cha "Civic Platform" kimeitaja kuwa "kashfa kubwa zaidi nchini Poland katika karne ya 21".

Uzio wa chuma wa kuwazuia wahamiaji huko Nomiki nchini Poland: 18.11.2022Picha: Maciek Luczniewski/AP Photo/picture alliance

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland Piotr Wawrzyk alijiuzulu wiki iliyopita kutokana na kashfa hiyo, ingawa sababu rasmi iliyotajwa ni "kutokuwepo kwa ushirikiano wa kutosha".

Idara ya Ujasusi ya Poland ilisema wiki iliyopita kuwa watu saba walikamatwa kuhusiana na kashfa hiyo. Hayo yameelezwa wakati nchi hiyo inatarajia kufanya uchaguzi Oktoba 15, na chama tawala kinachojinadi kuwa cha Haki na Sheria (PiS) kinajaribu kutumia suala la kupambana na uhamiaji kwa manufaa ya kisiasa, hasa ikizingatiwa kuwa ndio ajenda iliyowapa ushindi katika uchaguzi wa Bunge wa mwaka 2015.

Soma pia: Walinzi wa mpaka wa Poland waomba nyogeza ya askari 1,000

Polisi wa Ujerumani walikuwa tayari wameimarisha ukaguzi katika mpaka wake na Poland hata kabla ya kashfa hiyo kuibuka, kutokana na ongezeko la wahamiaji. Mwaka jana Poland ilikamilisha uzio wa chuma kuwazuia wahamiaji na imekuwa ikizishitumu Urusi na mshirika wake Belarus kuchochea mtiririko wa wahamiaji wanaoingia Ulaya, ikiwa kama mbinu inayotumiwa na mataifa hayo ili kuyumbisha eneo hilo.

(Chanzo: AFPE)