EU yachukua hatua kuzuwia njaa Afrika, Yemen
6 Aprili 2017Mkutano huo uliopendekezwa na Ujerumani, kuhusu kuwasadia watu waliokumbwa na mgororo katika kanda ya Afrika Mashariki na Yemen uliandaliwa haraka na Kamishna wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, na uliendeshwa sambamba na mkutano wa siku mbili juu ya Syria ulioyashirikisha mataifa 70 mjini Brussels.
Baada ya mkutano huo kuhusu mgogoro wa njaa, Ujerumani na Umoja wa Ulaya zilifanya mkutano mfupi na waandishi habari ambako Mogherini aliishukuru Ujerumani kwa kupendekeza mkutano huo. Mogherini aliutaja mkutano huo kuwa mfupi lakini muhimu sana, kujenga ufahamu kuhusu haja ya kuyasaidia maeneo yaliokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na ukame, kama vile Somalia, Sudan Kusini, kaskazini mwa Nigeria, Kenya na Ethiopia.
"Lakini tunatakiwa kuboresha mawasiliano," alisema Mogherini na kuongeza kuwa janga linalotabiriwa haliwezi kuruhusiwa kutukia. "Tunatoa mwito kwa washirika zaidi duniani kutoa msaada wa kibinadamu unaohitajika zaidi kwa ajili ya mamilioni ambao tayari wamekumbwa na ukame, au walio katika hatari ya kukumbwa na janga hilo."
Aibu kwa jumuiya ya kimataifa
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Sigmar Gabriel alishinikiza mkutano huu wa dakika za mwisho kuhusu Afrika kufuatia ziara ya eneo linalokumbwa na mgogoro, na waziri mwenzi wake anaehusika na maendeleo Gerd Müller mapema wiki hii. Müller aliuelezea muitikio wa jumuiya ya kimataifa kwa mgogoro huo kuwa ni kashfa kwa sababu hakuna aliyekuwa anajitokeza kuwasaidia wanaokumbwa na njaa Afrika.
"Hivi sasa tunafahamu kwamba maafa yanatunyemelea na hakuna anayeweza kusema hana alijualo kuhusu kinachawanyemelea watu katika maeneo yalioathirika. Ndiyo sababu sisi tumechukuwa hatua ya kwanza kuyaomba mataifa yashiriki katika utoaji wa misaada," alisema Gabriel.
Msaada zaidi
Umoja wa Mataifa unasema karibu watu milioni 20 katika kanda ya Afrika Mashariki na nchi ilioharibiwa kwa vita ya Yemen, wanakabiliwa na hatari ya kufa kwa njaa. Mkuu wa shughuli za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien aliutaja mgogoro huo mwezi Machi kuwa janga kubwa kabisaa la kibindamu tangu kuasisiwa kwa Umoja wa Mataifa.
Anaamini majanga kama hayo mara nyingin husababishwa na binadamu wenyewe. Nchini Yemen vita ndiyo vya kulaumiwa na Sudan Kusini, panade zinazihasimiana ndiyo zinawajibika kwa mavuno duni
Ujerumani na Umoja wa Ulaya zimeongeza msaada wao kwa mataifa yanayokabiliwa na njaa kwa mamilioni ya euro kabla ya kuanza kwa mkutano huo ulioandaliwa haraka. Mogherini aliseme Umoja wa Ulaya utatoa fedha za ziada kiasi cha takribani euro milioni 183, na Ujerumani kwa mujibu wa waziri Müller, inaogeza msaada wake kwa euro milioni 100 na kufikisha jumla ya euro milioni 300.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu euro bilioni moja zitahitajika kufikia katikati mwa mwaka huu ikiwa maeneo yalioathirika yatapata msaada yanayouhitaji. Upatikanaji ni mgumu hasa nchini Somalia kutokana na ukweli kwamba baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yanadhibitiwa na wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab. UN inachukulia kwamba mamia kwa maelfu ya watu watasafiri kwenda vituo vya dharura vya maji na kambi zilizoundwa na mashirika ya misaada ya kimataifa.
Mkutano wa wafadhili wa London
Gabriel amesema jumuiya ya kimataifa itakutana mjini Geneva Aprili 25 kujadili hali nchini Yemen, ambko Saudi Arabia na Iran zinapigana vita vya uwakala. Theluthi mbili ya Wayemen hivi sasa wanategemea msaada, inasema UN. Kulingana na O'Brien, hali nchini Yemen ni mbaya kuliko kokote kwingine.
Inatazamiwa kwamba mkutano wa Geneva utafuatiwa na mkutano kamili wa wafadhili mjini London May 11. "Hapo ndiyo tunataka kuanza kukusanya michango ya kweli," alisema Gabriel. Alisema atazingatia uwezekano wa iwapo ufadhili zaidi utakuwepo kutoka katika bajeti ya taifa ya Ujerumani.
Mwandishi: Bernd Riegert
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba