EU yaeleza mipango, mazungumzo ya Brexit
3 Aprili 2017Muongozo wa rasimu ambayo Shirika la habari la AFP liliipata, unataka kuwepo kwa mazungumzo ya awamu ambayo yataweka vipaumbele muhimu katika mchakato wa kujitoa, na kuongeza kwamba viongozi wataamua wakati ambapo kuna hatua iliofikiwa ili kuruhusu kuendelezwa kwa mazungumzo katika hatua nyingine. Aidha hatua hiyo itapunguza usumbufu utakaosababishwa na mchakato wa BREXIT ifikapo mwezi Machi mwaka 2019.
Rasimu hiyo imeongeza kwamba, Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya itakuwa ikifuatilia kwa karibu mwendelezo wa mazungumzo hayo, na kuamua kama kutakuwepo na hatua mahsusi zilizofikiwa ili kuruhusu mazungumzo hayo kuendelea katika aawamu inayofuata kuhusiana na mustkabali wa kimahusiano hususan ya biashara.
Rasimu hiyo ambayo pia imelifikia Shirika la habari la Associate Press, inasema, kwamba kwanza Umoja huo na Uingereza wanatakiwa kukamilisha makubaliano ya kujiondoa, na kuongeza kwamba makubaliano jumla kuhusu mfumo wa mustakabali wa kimahusiano unaweza kuelezwa katika awamu ya pili ya mazungumzo chini ya kifungu cha 50 cha mkataba wa Lisbon.
Miongozo hiyo ya rasimu, ambayo itatumwa kwa viongozi wa mataifa wanachama wote 27 wa Umoja wa Ulaya, inakuja ikiwa ni siku mbili baada ya waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May alipouarifu rasmi Umoja wa Ulaya kuhusu nia ya Uingereza kujiondoa kutoka Jumuiya hiyo ndani ya kipindi cha miwili.
Umoja huo kupitia muongozo wa rasimu umesema hakuna makubaliano yoyote kuhusu mustakabali wa kimahusiano na Uingereza utkaosainiwa kabla ya kuondoka ifikapo mwaka 2019, lakini mazungumzo kuhusu mfumo wa mashirikiano mapya yanaweza kuanza mara baada ya kukubaliana kuhusu talaka kati yao. Tusk anatarajiwa kukutana na May kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya utakaofanyika Aprili 29.
Katika hatua nyingine, waziri kiongozi wa Scotland, Nicola Sturgeon leo anatarajiwa kuwasilisha waraka kwa waziri mkuu Theresa May ya kuomba ruhusa ya kufanyika kwa awamu ya pili ya kura ya maoni juu ya uhuru wa nchi hiyo, chombo kimoja cha habari kimeripoti.
Mapema wiki hii, bunge la Scotland lilipiga kura kumuunga mkono mpango wa Sturgeon wa awamu ya pili ya kura hiyo. Sturgeon anasisitiza kuwepo kwa awamu hiyo ya pili, kwa kuwa BREXIT, na hususa mpango wa May wa kuiondoa Uingereza kutoka soko la pamoja la Ulaya, kutaathiri mahusiano na Uingereza na Umoja wa Ulaya, tofauti na matakwa yao.
Mwandishi: Lilian Mtono/EAP/AFPE/ECA.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman