1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaendelea kuyafanyia kazi makubaliano mapya ya Brexit

16 Oktoba 2020

Umoja wa Ulaya umesema unaendelea kufanyia kazi makubaliano mapya ya Brexit, na kutupilia mbali kauli ya waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson, kuwa wako tayari kuondoka bila makubaliano, ukiitaja kama upuuzi

Belgien EU-Gipfel Von der Leyen und Antonio Costa
Picha: Olivier Hoslet/Reuters

Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema baada ya kauli ya Johnson kwamba umoja huo unaendelea kufanyia kazi makubaliano, na kusisitiza hata hivyo kwamba hilo halifanyiki kwa gharama yoyote. Katika ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, von der Leyen amesema timu yao ya majadiliano itakwenda mjini London wiki ijayo kuongeza nguvu majadiliano hayo. Soma pia: Viongozi wa EU wakubaliana ushirikiano wa wazi na Uingereza

Naye rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, ambaye ndiye mwenyekiti wa vikao vya wakuu wa mataifa ya kanda hiyo, amerudia maneno hayo wakati wa kuhitimisha mkutano wa siku mbili wa kilele wa viongozi wakuu wa serikali na mataifa ya Umoja wa Ulaya, akisema wameungana na wamedhamiria kuwezesha kufikiwa kwa makubaliano.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson Picha: Downing Street/PA/dpa/picture-alliance

Tumeungana kikamilifu na tumedhamiria kufanyakazi ili kufanikisha makubaliano, lakini si kwa gharama yoyote. Na tulichosema jana kinabakia kuwa sahihi leo. Na unajua Michel Barnier amejifunga kujadiliana, tuko tayari kujadiliana na natumai hili litawezekana kupiga hatua mbeleni. Lakini narudia: Tumedharia kufikia makubaliano, lakini si kwa gharama yoyote.

Waziri mkuu Boris Johnson alisema mapema Ijumaa kwamba kama Umoja wa Ulaya hautabadili mwelekeo, hakutakuwa na makubaliano yanayoziruhusu biashara za Uingereza kuendelea kuingia soko kubwa la pamoja la Umoja wa Ulaya. Hii ilifuatia hatua ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya siku ya Alhamisi, kusema Uingereza ndiyo inapaswa kusogea katika mazungumzo au kuwa tayari kwa uvurugaji mkubwa wa kibiashara kuanzia mwaka 2021. Soma pia: Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Tangia mwanzo tuliweka wazi kabisaa kwamba tulitaka mfumo wa uhusiano kama wa Canada, wenye msingi wa urafiki na biashara huru. Kwa kuzingatia maazimio ya mkutano wa karibuni wa kilele wa wakuu wa mataifa ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, hilo halitofanya kazi kwa washirika wetu wa EU. Wanataka kuendelea kuwa na uwezo wa kudhibiti uhuru wetu wa kisheria, uvuvi wetu katika namna ambayo haikubaliki kabisaa kwa taifa huru.

Merkel amezitaka pande zote kuendelea kuzungumzaPicha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amewaambia waandishi habari mjini Berlin baada ya mkutano wa kilele, kwamba muda ulikuwa unayoyoma na ingekuwa vyema wakafikia makubaliano, lakini pia emesistiza kwamba hili halitakuwa kwa gharama yoyote.

Kwa upande wake rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema ni Uingereza iliojiondoa katika umoja huo na hivyo wao ndiyo wanahitaji makubaliano zaidi ya Umoja wa Ulaya, huku akikanusha kwamba suala la uvuvi ndiyo limesababisha mkwano kati ya pande mbili.

Pande zote zimeelezea kuvunjwa moyo na maendeleo ya mazungumzo katika siku za karibuni, huku kila upande ukiushutumu mwingine kwa ubishi. Johnson hata hivyo aliacha mlango wazi kwa majadiliano zaidi, lakini msemaji wake amesema hivi sasa kwamba wanayachukulia mazungumzo hayo kuwa yamefungwa, isipokuwa tu kama umoja wa Ulaya uko tayari kubadili msimamo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW