1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yahimiza muafaka kuhusu uhamiaji

27 Januari 2017

Chini ya sheria za sasa za Dublin, wanaotafuta hifadhi katika nchi za Umoja wa Ulaya, wanapaswa kurejeshwa katika nchi ambazo walifikia kwanza.

Afghanistan abgeschobene Flüchtlinge aus Deutschland kommen in Kabul an
Picha: Getty Images/AFP/W. Kohsar

Mawaziri wa ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya siku ya Alhamisi walipiga hatua katika kupata suluhisho la mkwamo kuhusu namna ya kugawana mzigo wa wakimbizi wanaotafuta hifadhi, ambao wengi wao wako Italia na Ugiriki. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa.

Huku bara la Ulaya likikabiliwa na idadi kubwa zaidi ya wahamiaji ambayo haijawahi kutokea tangu vita vikuu vya pili vya Dunia, mawaziri hao wanaokutana mjini Valetta nchini Malta, wameandika mapendekezo yanayoitwa sheria za Dublin, ambazo zitawahitaji watafutao uhifadhi kuwasilisha maombi yao kwanza katika nchi wanazofikia ambazo mara nyingi huwa ni Italia na Ugiriki.

Akizungumza na wanahabari baada ya kukamilika  mkutano huo wa kila baada ya miezi sita,waziri wa mambo ya  ndani wa Malta Camelo Abela ambaye ndiye mwenyeji wa awamu ya sasa ya mkutano huo amesema "Leo tumepiga hatua mbele na ni vyema kwa mustakabali"

Naye kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos ambaye pia alizungumza na wanahabari hao, amewahimiza wanachama 28 wa umoja huo kumaliza mkwamo wa kufanyia mabadiliko sheria za Dublin ambao umedumu kwa muda wa miezi 18. "Kwa mara ya kwanza nimeona dalili ya maendeleo kuwa hatuko mbali kufikia suluhisho la pamoja na ushirikiano unaodhihirika": Amesema Avramopoulos.

Kuwatengea maeneo salama nje ya Umoja wa Ulaya

Waziri wa ndani nchini Ujerumani Thomas de MazierePicha: DW/B. Riegert

Chini ya sheria za sasa za Dublin, wanaotafuta hifadhi katika nchi za Umoja wa Ulaya, wanapaswa kurejeshwa katika nchi ambazo walifikia kwanza. Mawaziri walijadili hatua tatu kuu kuhusu sheria za Dublin, huku msisitizo ukiwekwa kuwa watu waombe hifadhi katika nchi waloyowasili kwanza wakati wa uhamiaji wa ''kawaida''. Ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani ya Ujerumani Thomas de Maiziere. Hata hivyo, bila ya kufafanua zaidi, de Maiziere amesema kuwa ikiwa mhamiaji atahitimisha kiwango fulani, basi mbinu nyingine itatumika ambapo nchi nyingine zitatwikwa mizigo zaidi ya kuwapa hifadhi watu hao. Ameongeza kuwa, ikiwa kweli kuna ongezeko kubwa la wahamiaji, basi nchi wanachama zinaweza kupeleka wahamiaji hao katika "maeneo salama nje ya Umoja wa Ulaya".

Duru za Umoja wa  Ulaya zimesema mashirika kama UNHCR linaloshughulikia wakimbizi na lile la Kimataifa la Uhamiaji, yanaweza kusaidia nchi zilizopo Kaskazini mwa Afrika au zile zilizo kusini, kutenga vituo ambavyo vinatimiza matakwa ya kimataifa kuwezesha kuwapokea wahamiaji ili kuwawezesha kurejea katika nchi zao za awali.

Makubaliano?

Avramopoulos amesema japo vipengee zaidi vingali vinahitaji kuainishwa, wote walikubali hatua zote tatu ambazo zilijadiliwa. Amesema kuwa Umoja wa Ulaya bado itaheshimu kanuni ya kimataifa ya ulinzi dhidi ya kutoshitakiwa ambayo inazuia kumrudisha mkimbizi katika nchi ambayo anaweza kuteswa au maisha yake yanaweza kuwa hatarini.

Picha: DW/B. Riegert

Nchi wanachama hazijakubaliana kuhusu namna ya kugawana mzigo wa kuwapa hifadhi wanaotafuta hifadhi. Nchi za  Ulaya Mashariki kama vile Hungary, Slovakia na Poland, ni kati ya zile ambazo zimekuwa zikichelea kuwapokea  wahamiaji wanaotafuta hifadhi, huku wakisema wanaweza tu kutoa usaidizi wa kifedha.

Mawaziri walikuwa wakizungumza baada ya Waziri Mkuu wa Malta Joseph Muscat kuuonya Umoja wa Ulaya dhidi ya uwezekano wa kutokea mmiminiko wa wahamiaji kutoka Libya kuelekea Italia msimu wa jua uanzapo. Uhamiaji haramu unaendelea na zaidi ya wahamiaji 180,000 walifika Italia mwaka jana, tofauti na rekodi ya mwaka 2014 ambapo kulikuwa na wahamiaji 170,100.

Mkataba wa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya ulioafikiwa nchini Uturuki mnamo mwezi Machi mwaka jana, umepunguza pakubwa idadi ya wanaotafuta hifadhi wanaofika nchini Ugiriki, ambayo ni njia ya mwanzo iliyotumiwa na wahamiaji kuingia Ulaya.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema wengi wa wanaosafiri maeneo ya kati ya Mediterrania ni wahamiaji wanaotafuta kazi wala sio wanaotoroka mapigano au kuteswa. Wengi wa walioingia Ugiriki walitoka Syria na nchi nyingine zinazokumbwa na mapigano.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu