1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yataka usitishaji mara moja wa vita vya Israel-Hezbollah

25 Novemba 2024

Mwanadiplomasia mkuu wa EU, Josep Borrell ametoa wito wa usitishaji vita wa haraka kati ya Israel na Hezbollah na kusisitiza utekelezaji wa Azimio 1701 la Umoja wa Mataifa linalotaka wanajeshi wa Israel kuondoka Lebanon.

Lebanon | Josep Borrell mjibi Beirut
Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel akiwa katika mazungumzo na Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati mjini Beirut, Lebanon, Novemba 24, 2024.Picha: Mohamed Azakir/REUTERS

Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ametoa wito wa usitishaji vita wa haraka katika mzozo wa Israel na Hezbollah wakati wa ziara yake nchini Lebanon Jumapili, wakati kundi hilo la wanamgambo likidai kufanya mashambulizi kadhaa ya kuvuka mpaka.

Mapema wiki hii, mjumbe maalum wa Marekani, Amos Hochstein, alisema nchiniLebanon kwamba makubaliano ya kusitisha vita yalikuwa "katika uwezo wetu," kabla ya kuelekea Israel kwa mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo.

Vita kati ya Israel na Hezbollah vilipamba moto mwishoni mwa Septemba, karibu mwaka mmoja baada ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran kuanzisha mashambulizi ya kumuunga mkono mshirika wake wa Kipalestina, Hamas, kufuatia shambulizi lake la Oktoba 7.

Mgogoro huo umesababisha vifo vya watu wasiopungua 3,670 nchini Lebanon tangu Oktoba 2023, kulingana na wizara ya afya, wengi wao tangu Septemba.

Katika mji mkuu wa Lebanon, Borrell alifanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, ambaye ameongoza juhudi za upatanishi kwa niaba ya mshirika wake Hezbollah.

"Tunaona njia moja tu inayowezekana: kusitisha vita mara moja na utekelezaji kamili wa Azimio 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," alisema Borrell baada ya mkutano wake na Berri.

Soma pia: Hezbollah yavurumisha makombora na kuua askari 4 wa Israel

Chini ya Azimio nambari 1701, ambalo lilimaliza vita vya mwisho kati ya Hezbollah na Israel mwaka 2006, wanajeshi wa Lebanon na walinda amani wa Umoja wa Mataifa pekee ndio wanapaswa kuruhusiwa kuwepo kusini mwa nchi, ambapo Hezbollah ina nguvu.

Pia liliitaka Israel iondoe wanajeshi wake kutoka Lebanon. "Mwezi Septemba nilikuja na nilikuwa na matumaini kwamba tunaweza kuzuia vita kamili vya Israel kuivamia Lebanon.

Israel yashambulia katikati mwa Beirut

01:03

This browser does not support the video element.

Miezi miwili baadaye Lebanon iko ukingoni kuporomoka," alisema Borrell. Alisema Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa euro milioni 200 kusaidia kuimarisha vikosi vya jeshi la Lebanon.

Hezbollah: Kundi lenye nguvu kuliko jeshi la Lebanon

Hezbollah ni moja ya makundi ya wapiganaji wasio wa kiserikali yalio na silaha bora duniani, na ndiyo kundi pekee nchini Lebanon lililokataa kukabidhi silaha zake baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1975-1990.

Jeshi la Lebanon linahakikisha uwepo wake kote nchini, lakini Hezbollah ndio ina nguvu katika maeneo muhimu kando ya mpaka na Israel. Ingawa jeshi la Lebanon halishiriki moja kwa moja katika vita vya Israel na Hezbollah, limepoteza wanajeshi kadhaa.

Jumapili, jeshi lilisema shambulizi la anga la Israeli kwenye kituo cha jeshi lilimuua mwanajeshi mmoja na kuwajeruhi wengine 18.

Pia Jumapili, Hezbollah ilisema ilifanya mashambulizi kwa kutumia makombora na droni kwenye kambi ya jeshi la majini ya kusini mwa Israel na shabaha nyingine ya kijeshi mjini Tel Aviv.

Kundi hilo lilisema lilifanya "kwa mara ya kwanza, shambulizi la anga kwa kutumia kundi la droni kwenye kituo cha jeshi la majini cha Ashdod."

Soma pia: Vita vyaendelea kurindima Palestina na Lebanon

Pia lilidai kufanya operesheni dhidi ya "shabaha ya kijeshi" mjini Tel Aviv kwa kutumia "mashambulizi ya makombora ya hali ya juu na kundi la droni."

Jeshi la Israeli lilisema mizinga ya tahadhari ya mifumo ya ulinzi wa anga iliwashwa katika maeneo kadhaa ya katikati na kaskazini mwa Israel, na kuongeza kuwa lilizuia makombora yaliyofyatuliwa kutoka Lebanon.

Wanawake wa Lebanon wakabiliwa na kitisho cha uzazi salama

02:07

This browser does not support the video element.

Idara ya huduma ya matibabu ya dharura ya Israel, Magen David Adom, ilisema iliwahudumia watu wawili wakiwemo mwanamke wa miaka 70 aliyejeruhiwa kidogo.

Jumamosi, Lebanon ilisema mashambulizi ya Israeli kote nchini humo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 55, wengi wao wakiwa katikati mwa mji wa Beirut.

Shambulizi moja kwenye kitongoji cha watu wa kipato cha chini cha Basta mjini Beirut liliua watu wasiopungua 20 na kuwajeruhi wengine 66, wizara ya afya ya Lebanon ilisema.

"Tuliona watu wawili wakiwa wamekufa chini... Watoto walianza kulia na mama yao akalia zaidi," alisema Samir, mwenye umri wa miaka 60, ambaye anaishi kwenye jengo lililo mkabala na lile lililoharibiwa.

Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Israeli, Israel Katz, Jumamosi, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin "alisisitiza dhamira ya Marekani ya kupata suluhisho la kidiplomasia" katika vita vya Lebanon, msemaji wa Pentagon alisema.

Soma pia: 

Msemaji wa Katz alisema anapongeza juhudi za Marekani kuelekea utulivu nchini Lebanon, lakini alisema Israel itaendelea "kuchukua hatua kali kujibu mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya raia wa Israel."

Mateka wa Israel auawa Gaza

Katika upande wa Gaza, tawi la kijeshi la Hamas limesema Jumamosi kwamba mateka wa Israeli aliyekamatwa wakati wa shambulizi la Oktoba 7 ameuawa. Jeshi la Israeli lilisema haliwezi "kuthibitisha wala kukanusha" madai hayo.

Waandamanaji wa Israeli walifanya maandamano yao ya kawaida Jumamosi mjini Tel Aviv kudai serikali yao ifikie makubaliano ya kuwaachilia mateka waliobaki.

Jumapili, shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza lilisema shambulizi la droni lilimjeruhi vibaya mkuu wa hospitali katika shambulizi kwenye kituo cha afya, wakati mashambulizi ya anga ya Israeli yakiua watu 11 kote katika eneo hilo la Palestina.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

01:04

This browser does not support the video element.

Hossam Abu Safiya anaongoza hospitali ya Kamal Adwan, moja ya hospitali mbili pekee zinazoendesha huduma kwa sehemu kaskazini mwa Gaza, wakati eneo hilo likiwa katika hali mbaya ya kibinadamu.

Shambulizi la Hamas la Oktoba 7 dhidi ya Israel ambalo lilizua vita vya Gaza lilipelekea vifo vya watu 1,206, wengi wao wakiwa raia, kulingana na taarifa ya AFP kutoka kwa maafisa wa Israeli.

Soma pia: Shambulio la Israel kwenye shule huko Gaza lalaaniwa kimataifa

Kampeni ya kujibu mashambulizi ya Israel huko Gaza imeua watu wasiopungua 44,211, wengi wao wakiwa raia, kulingana na takwimu za wizara ya afya ya eneo hilo linaloongozwa na Hamas, ambazo Umoja wa Mataifa unazichukulia kuwa za kuaminika.

Ukosoaji dhidi ya Israel umeongezeka kutokana na mwenendo wake wa vita hivyo, na wiki hii Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant.

Pia ilitoa hati ya kukamatwa kwa mkuu wa kijeshi wa Hamas, Mohammed Deif, ingawa haijulikani ikiwa bado yuko hai.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW