1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaidhinisha mpango wa uokozi kukabiliana na COVID-19

14 Julai 2021

Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha mpango wa kuufufua uchumi uliowasilishwa na nchi 12 wanachama wa umoja huo, kutokana na athari za janga la virusi vya corona.

Belgien Brüssel | EU-Gipfel, Sitzungssaal
Picha: EU Council/Anadolu Agency/picture alliance

Baraza la Ulaya limesema mpango huo wa uokozi wenye thamani ya Euro bilioni 672.5 unalenga kuufufua uchumi wa Ulaya kwa kuunga mkono mageuzi na miradi ya uwekezaji ya nchi wanachama. Nchi zitakazonufaika na mpango huo uliopitishwa jana ni pamoja na Ujerumani, Austria, Ubelgiji, Denmark, Ufaransa, Ugiriki, Italia, Latvia, Luxembourg, Ureno, Slovakia na Uhispania.

Waziri wa Fedha wa Slovenia, Andrej Sircelj ambaye nchi yake ndiyo rais wa Umoja wa Ulaya kwa sasa, amesema hiyo ni hatua muhimu kwa umoja huo na amesisitiza haja ya kuidhinisha mipango hiyo vizuri kwa ajili ya malengo ya pamoja ya Umoja wa Ulaya wenye nchi 27.

Tukio la kihistoria

''Nadhani leo ni siku ya kihistoria kwa sababu ni mara ya kwanza Umoja wa Ulaya na Halmashauri ya Ulaya zinazisaidia nchi kwa njia hiyo. Kwa mfano wameenda sokoni, wakanunua hati fungani na sasa wanatoa misaada na mikopo kwa kila nchi,'' alifafanua Sircelj.

Uhispania na Italia zitanufaika zaidi na mpango huo, huku zikiwa na jumla ya takriban Euro bilioni 70 ya ruzuku katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwa mbele ya Ufaransa yenye Euro bilioni 40. Aidha, Makamu wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Valdis Dombrovskis amesema hatua hiyo ni habari njema kwani wameuandaa mpango huo kabambe kwa muda mrefu.

Makamu wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Valdis DombrovskisPicha: Reuters/E. Vidal

Hata hivyo, pendekezo la Hungary limegeuka kuwa mkwamo wa kisiasa na bado halijasainiwa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya kutokana na wasiwasi wa nchi hiyo kujizatiti katika kupambana na rushwa na utawala bora. Ni nchi mbili tu kati ya 27, Bulgaria na Uholanzi ambazo hazijawasilisha mapendekezo yao.

Ama kwa upande mwingine serikali ya Ufaransa imeutetea uamuzi wake wa kuwataka wananchi ambao hawajachoma chanjo ya virusi vya corona, wapime kubaini iwapo wameambukizwa virusi hivyo au la ili kuruhusiwa kula kwenye mikahawa au kufanya safari za mbali. Hatua hiyo imesababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotaka kuchoma chanjo.

Ujerumani kutofuata njia ya Ufaransa

Ujerumani kwa upande wake imesema haina mpango wa kufuata nyayo za Ufaransa na nchi nyingine kuwalazimisha watu kuchoma chanjo ya COVID-19. Aidha, China leo imerekodi visa vipya 24 vya virusi vya corona, idadi hiyo ikiwa imeshuka kutoka 29 siku moja kabla.

Nalo bara la Afrika limerekodi visa 6,009,854 vya COVID-19, tangu ugonjwa huo ulipozuka nchini China, Desemba mwaka 2019. Tunisia inapambana kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona ambavyo vimemuambukiza pia Spika wa Bunge Rached Ghannouchi. Morocco nayo inapanga kupeleka vitanda 100 kwenye wodi za wagonjwa mahututi na idadi kama hiyo ya mashine za kuwasaidia wagonjwa kupumua ili kupambana na janga hilo.

Wakati huo huo nchi za Jumuiya ya Madola zimepoteza dola bilioni 345 katika biashara mwaka uliopita kutokana na janga la virusi vya corona lililosababisha kudorora kwa uchumi ulimwenguni.

(DPA, AFP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW