1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaikalia kooni serikali ya Uganda

Lubega Emmanuel21 Aprili 2016

Ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya umeitaka Uganda kuifanyia mageuzi tume ya uchaguzi na ukikosoa serikali ya nchi hiyo kutotilia maanani mapendekezo ambayo ujumbe huo huyatoa kila mara baada ya uchaguzi

Uganda PK EU-Delegation in Kampala
Picha: DW/L. Emmanuel

Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wake kuhusiana na mchakato wote wa shughuli za uchaguzi uliofanyika tarehe 18 mwezi Februari, ujumbe wa wangalizi wa umoja wa Ulaya umetoa angalizo kuwa Uganda inahitaji kurekebisha mbinu zake za kuendesha zoezi hilo ambalo ni nyeti kwa kujenga demokrasia.

Akiwasilisha ripoti ya hatma kuhusu jukumu lao, mkuu wa ujumbe huo Eduard Kukan aliyeandamana na mabalozi wa mataifa hayo pamoja na yule wa Marekani aliorodhesha baadhi ya masuala yaliyopelekea uchaguzi huo kutofikia viwango vya kutajwa kuwa wa haki na huru.

"Tume ya uchaguzi ilikosa uhuru na uwazi, vyombo vya dola vilijenga mazingira ya vitisho dhidi ya wapinzani na wapigakura, huku polisi wakitumia nguvu ya kupindukia, dhidi ya wapinzani, wanahabari na wapigakura," alisema Kukan katika ripoti hiyo alioisoma mbele ya waandishi wa habari mjini Kampala.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: picture alliance/Kyodo

Serikali yaonywa kutoheshimu ushauri

Mara nyingi baadhi ya wananchi wamelezea kutorishishwa kwao na ripoti zinazotolewa na wangalizi wakisema hazizingatiwi na serikali. "Hizo ripoti zao hazitusaidii, kwa sababu serikali haichukuwi hatua," alisema Siama Sadi mkaazi wa kitongoji cha Naguru.

Mkuu wa ujumbe huo hata hivyo ameonya kwamba tabia ya serikali ya Uganda kupuuza mapendekezo yake kuhusiana na uchaguzi ni ishara kwamba haiheshimu ushirikiano wake na wabia wake wa maendeleo. "Sisi Umoja wa Ulaya tulikuwa na bado tunaichukulia Uganda kuwa mshirika muhimu na tunaraji ushauri wetu kutiliwa maanani," alisema balozi Kukan.

Miongoni mwa mapendekezo muhimu ambayo ujumbe huo umeitaka Uganda kuzingatia ni pamoja na kuifuta sheria ya kudhibiti shughuli za umma ambayo inadai polisi hutumia kuwanyanyasa wananchi na upinzani kwa jumla.

Mpinzani mkuu wa Museveni kwenye uchaguzi uliyopita kanali mstafu Dk. Kizza Besigye.Picha: Getty Images/AFP/STRINGER

Museveni, Spika Kadaga wahusishwa

Ujumbe huo umefahamisha kwamba kabla ya ripoti hiyo kuwasambazwa, wameijadili na rais Museveni, spika wa bunge la Uganda, tume ya uchaguzi, wakuu wa jeshi la polisi. Kwa hiyo wanataraji kwamba wadau hao wote watazingatia mapendezo 30 yaliyomo katika ripoti hiyo.

Ujumbe huo aidha umezisifu asasi za kiraia kwa kufuatilia kwa ukaribu mchakato wa uchaguzi pamoja na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki chini ya kauli mbiu ya Topowa ambalo ni neno la lugha ya mitaani iliyokuwa na ujumbe wa usife moyo bali thamini kura yako kuleta mageuzi.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.

Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW