EU yaikosoa Hungary kuhusu sheria ya mashoga
8 Julai 2021Kiongozi huyo wa nchi anayetokea kambi ya mrengo wa kulia nchini Hungary amesema hayo leo siku ambapo sheria hiyo imeanza kutumika. Sheria hiyo inazipiga marufuku shule kutumia vifaa vinayoonekana kuhamasisha kuhusu ushoga na kusema watoto wa chini ya umri wa miaka 18 hawawezi kuoneshwa maudhui ya kingono. Sheria hiyo pia inapendekeza kuanzisha orodha ya vikundi vinavyoruhusiwa kuendesha elimu ya ngono shuleni.
Orban amewakosoa viongozi wa Umoja huo wa Ulaya kwa kuwa na tabia kama za wakoloni wanaotaka kuyatolea amri mataifa mengine na kukanusha kwamba sheria hiyo ni ya uonevu dhidi ya mashoga huku akitaja shtuma za Von der Leyen kuwa aibu. Orban ameongeza kusema kwamba bunge la Ulaya na halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya zinawataka kuruhusu wanaharakati wanaopigania haki za mashoga na wasagaji katika shule za chekechea, za msingi na upili lakini hivi sivyo inavyotaka Hungary.
Wakati huo huo rais wa Czech Milos Zeman ameongeza sauti yake katika suala hilo akisema kwamba anadhani kuingilia masuala ya taifa lingine mwanachama wa Umoja wa Ulaya ni kosa kubwa sana la kisiasa na kwamba kila taifa lina kitu linaloshtumiwa nalo, hivyo basi hampingi orban anaposema kuwa hawapingi mashoga lakini anapinga hujuma sio tu kwa wazazi lakini pia kwa watoto wanaofunzwa elimu ya ngono.
Wabunge wa Umoja wa Ulaya kuidhinisha azimio la pamoja
Wakati huo huo, viongozi wengi wa Umoja wa Ulaya wanataka kuondolewa kwa sheria hiyo na kusema inakiuka maadili ya Umoja huo. Hapo jana Von der Leyen ameliambia bunge la Umoja huo mjini Strasbourg kwamba sheria hiyo ni fedheha. Wabunge wa Umoja huo wa Ulaya leo wanatarajiwa kuidhinisha azimio la pamoja la kuishtumu sheria hiyo na kuihimiza halmashauri kuu ya Umoja huo kuchukuwa hatua dhidi ya Hungary iwapo haitabadilisha msimamo wake.
Azimio hilo linasema kuwa sheria hiyo itazuia vikali na kwa maksudi haki na uhuru wa mashoga pamoja na haki za watoto na kuihimiza halmashauri hiyo kuwasilisha suala hilo kwa mahakama ya haki ya Umoja wa Ulaya. Hii leo, mashirika yasio ya kiserikali ya Amnesty International na Hatter, yalipeperusha puto moja kubwa la muundo wa moyo lenye rangi ya upinde wa mvua juu ya bunge la Hungary kulalamika dhidi ya sheria hiyo. Mkurugenzi wa shirika hilo la Amnesty nchini Hungary David Vigh amewaambia wanahabari kwamba lengo la sheria hiyo ni kuwaondoa mashoga katika jamii. Amesema kuwa hawatazingatia sheria hiyo ama kubadilisha mipango yao ya elimu.