1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaishutumu Urusi kwa kufunga ofisi ya DW nchini mwake

4 Februari 2022

Umoja wa Ulaya umeulaani uamuzi wa Urusi kufunga ofisi za shirika la utangazaji la Ujerumani, Deutsche Welle, na kusema hatua hiyo haikubaliki na ni mbaya kwa ustawi.

DW Studio in Moskau, Schließung
Picha: Alexander Zemlianichenko Jr/AP Photo/picture alliance/dpa

Msemaji wa Umoja wa Ulaya Peter Stano amewaambia waandishi wa habari kwamba uamuzi wa Urusi unasikitisha na kwa mara nyingine unadhihirisha mwendelezo wa nchi hiyo kukiuka uhuru wa habari na kutoheshimu uhuru wa kujieleza.

Stano amesema Umoja wa Ulaya unasimama na Deutsche Welle pamoja na wafanyakazi wake walioko Urusi na umoja huo utaendelea kufuatilia hali hiyo kwa ukaribu.

Urusi yawapokonya vibali waandishi habari wa DW Moscow

Urusi ilisema hatua yake ni ya kulipiza kisasi dhidi ya mamlaka za vyombo vya habari Ujerumani kupiga marufuku Idhaa yake ya Russia Today (RT) inayotangaza kwa lugha ya Kijerumani,

Wakati huo huo- msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema uamuzi wa Urusi dhidi ya shirika la DW ni wa kisiasa tu.

Ameongeza kwamba uamuzi uliochukuliwa na mamlaka za Ujerumani dhidi ya idhaa ya Urusi Russia Today (RT) haulingani kwa vyovyote vile na huo uliochukuliwa na Urusi dhidi ya shirika la kimataifa la habari linalomilikiwa na umma wa Ujerumani Deutsche Welle.

Urusi imesitisha operesheni ya ofisi ya DW mjini Moscow kuanzia Ijumaa na kufuta vibali vya kazi vya waandishi Habari wa DW walioko Urusi.

Mkurugenzi Mtendaji wa DW Peter Limbourg amesema uamuzi wa Urusi ni wa kusikitisha na kwamba DW itachukua hatua za kisheria dhidi ya uamuzi huo.Picha: DW

Shirika la DW ambalo limekuwa na leseni ya kutangaza nchini Urusi tangu mwaka 2005, limesema litachukua hatua za kisheria dhidi ya uamuzi wa Urusi.

Urusi yaifungia Deutsche Welle kulipiza kisasi dhidi ya Ujerumani

Mamlaka inayosimamia utoaji leseni ya vyombo vya habari nchini Ujerumani, ZAK, kukipiga marufuku kituo cha televisheni cha Urusi, Russia Today (RT DE), kutangaza nchini Ujerumani kwa sababu hakina leseni.

ZAK iliongeza kwamba televisheni ya RT DE haiwezi kutangaza kwa kutumia leseni ya Serbia.

Stano amesema uamuzi huo wa marufuku kutokana na kukosa leseni haiwezi kulinganishwa na DW ambayo ina leseni kuendesha shughuli zake nchini Urusi.

Waandishi habari wa DW walioko Urusi walitarajiwa kurudisha vibali vyao vya kazi katika wizara ya mambo ya nje ya Urusi leo Ijumaa.

Lakini hatua hiyo ya Urusi ikiendelea kuibua mjadala, Urusi imesema leo Ijumaa kwamba itakuwa na jibu la kipekee ikiwa Ujerumani itamaliza mvutano kuhusu operesheni ya vyombo hivyo viwili. Lakini vilevile itaendeleza mvutano huo ikiwa Ujerumani itachagua njia ya mvutano.

Mamlaka inayosimamia utoaji leseni ya vyombo vya habari nchini Ujerumani, ZAK, kukipiga marufuku kituo cha televisheni cha Urusi, Russia Today (RT DE), kutangaza nchini Ujerumani kwa sababu hakina leseni.Picha: Andre M. Chang/ZUMA/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Urusi Maria Zakharova amewaambia waandishi wa habari hivyo akiongeza kuwa kwa sasa uamuzi ni wa Ujerumani.

Mvutano huo kuhusu vyombo vya habari umezidi kudhoofisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili ambayo tayari yanakabiliwa na mzozo wa bomba la kusafirisha gesi la Nord Stream 2.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anatarajiwa kuizuru Urusi Februari 15 kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin.

Naibu spika wa Urusi Konstantin Kosachyov wa baraza la juu la bunge la Urusi amesema Putin na Scholz wataujadili mzozo huo watakapokutana, na kwamba Urusi itakuwa tayari kubatilisha uamuzi wake dhidi ya Deutsche Welle ikiwa Ujerumani itabadili msimamo wake dhidi ya kituo cha Urusi RT DE.

(AFPE, RTRE, DPAE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW