Hungary yatuhumiwa kuipelekea taarifa za EU, Urusi
23 Machi 2026
Umoja wa UIaya umesema umeingiwa na wasiwasi kuhusu ripoti zinazoonesha kwamba Hungary imekuwa ikitoa taarifa za Umoja huo kwa Urusi.
Umoja wa Ulaya umesema unatarajia kupata maelezo ya ufafanuzi wa kina kutoka kwa Hungary, baada ya gazeti la Marekani la Washington Post mnamo siku ya Jumamosi kuripoti kwamba waziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter Szijjarto alikuwa mara kwa mara kwenye simu wakati wa mikutano ya Umoja wa Ulaya, akipitisha taarifa kwa mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kuhusu mazungumzo ya Umoja huo na maamuzi yao.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walumbana na Orban kuhusu mkopo wa Ukraine
Washington Post limedai,Hungary kwa miaka minne imekuwa ikiipitishia Urusi taarifa kuhusu kinachoendelea katika halmashauri ya Umoja wa Ulaya.
Hivi leo waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban ameagiza uchunguzi ufanyike kuhusu kile alichokiita, kudukuliwa kwa waziri wake wa mambo ya nje, wakati serikali ya Budapest ikitafuta njia ya kushughulikia ripoti hizo za kuhusishwa na Urusi kabla ya uchaguzi wa mwezi Aprili.