EU yajadili mageuzi ya Palestina kusaidia kumaliza vita Gaza
21 Novemba 2025
Mkutano huo wa Kundi la Wahisani wa Palestina, ulioongozwa kwa ushirikiano na Ufaransa na Saudi Arabia, ulijikita katika mageuzi ya Mamlaka ya Palestina yaliyoainishwa katika mpango wa amani wa Marekani ambao uliidhinishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu.
Mamlaka ya Palestina, ambayo inasimamia baadhi ya maeneo yanayojitawala kwa kiasi fulani katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, inafanya juhudi mpya za kuwa mhusika katika Gaza ya baada ya vita.
Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Mustafa alitoa wito kwa Israel kugharamia pakubwa, kama sio kikamilifu, katika ukarabati wa uharibifu uliofanyika Gaza na kuchangia katika juhudi za kuijenga upya.
Umoja wa Ulaya, mfadhili mkubwa wa Mamlaka ya Palestina, unatumai inaweza kutawala Gaza kwa ufanisi baada ya mageuzi ya kina. Lakini Washington inadai kwamba Mamlaka ya Palestina ifanye mageuzi kwanza, na Israeli inakataa jukumu lolote la Palestina huko Gaza.
Eupol kutoa mafunzo huko Jericho
Mawaziri wa mambo ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya walijadili mipango ya kutanua kwa kiasi kikubwa operesheni za polisi ya umoja huo na usalama wa mipaka huko Gaza kama sehemu ya juhudi za kuunga mkono mpango wa amani wa Marekani.
Mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya Kaja Kallas alisema maafisa 3,000 wa usalama wa Kipalestina watapewa mafunzo na maafisa wa Ulaya.
EU inaweza kutumia ujumbe wake wa polisi wenye makao yake Ukingo wa Magharibi, Eupol Copps, kuongoza ujenzi wa kikosi kipya cha polisi kwa ajili ya Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita. Lengo ni kutoa mafunzo kwa maafisa wote 13,000 wanaotarajiwa kuhitajika, kwa kipindi kirefu.
Kwa kipindi kifupi, Eupol Copps itasaidia kujenga upya miundo ya mahakama na usalama huko Gaza na kuandaa programu za mafunzo kwa wakufunzi wa polisi wa Palestina katika chuo cha polisi huko Jericho kinachofadhiliwa kwa ushirikiano na Ujerumani.
Hadi sasa, polisi wa kiraia huko Gaza wamekuwa wakihudumu chini ya udhibiti wa kundi la wanamgambo wa Hamas, lililopigana vita vya miaka miwili na Israeli ambavyo vimeacha eneo kubwa likiwa magofu kutokana na mashambulizi ya anga ya Israeli na mashambulizi ya ardhini.