1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yalihofia Dola la Kiislamu Barani Ulaya

18 Oktoba 2016

Wakati mashambulizi ya kuukomboa mji wa Mosul yakiingia siku yake ya pili, Kamishna wa usalama wa Umoja wa Ulaya, Julian King ameonya kuhusu kitisho cha kurejea Barani Ulaya kwa wapiganaji wa Dola la Kiislamu, IS.

Irak Mossul Offensive der Regierungstrupen gegen IS
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Jumanne hii kwenye mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la Die Welt la nchini Ujerumani, Kamishna huyo wa usalama wa Umoja wa Ulaya amesema "Kuchukuliwa kwa mji huo wa Mosul ulioko Kaskazini mwa Iraqi, kutasababisha kurejea kwa wapiganaji wa kundi hilo Barani Ulaya". Amesema, hata wakirejea wachache wataweka kitisho ambacho Ulaya inahitaji kujiandaa nacho.

Majeshi la Iraqi yanaendelea kufanya mashambulizi yanayolenga kuuomboa mji huo wa Mosul, hatua inayochukuliwa kama kuvunjwa kabisa kwa ngome hiyo ya IS, iliyokuwemo ndani ya mji huo, walioutangaza kama ngome yao miaka miwili iliyopita. 

Vikosi vyenye wanajeshi wapatao 30,000 vinaongoza mashambulizi hayo, yanayoungwa mkono na mashambulizi ya anga na ya ardhini kutoka kwa muungano wa majeshi ya mataifa 60 unaoongozwa na Marekani. 

Kamishna wa masuala a usalama wa Umoja wa Ulaya, Julian King, amesema Ulaya inahitaji kujiandaa na kitisho hicho.Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Ingawa mashambulizi hayo yangali yanatabiriwa kukabiliwa na ugumu, inaelezwa kuwa majeshi ya Iraqi yamefanikiwa kusonga mbele zaidi ya matarajio yao, taarifa ya wizara wa ulinzi ya Marekani, Pentagon Imesema. Mashambulizi hayo ambayo yalisubiriwa kwa muda mrefu yalizua wasiwasi mkubwa juu ya usalama wa mamia kwa maelfu ya raia waliozuiliwa kwenye mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Iraqi, huku makundi ya misaada wa kibaadamu yakionya kitisho cha janga la kibinaadamu.

Rais wa Marekani Barack Obama, amenukuliwa kwenye mahojiano na gazeti la nchini Italia la La Republica kwamba, kundi hilo la kigaidi la Dola la Kiislamu hatimaye linaweza kuangushwa baada ya mashambulizi haya magumu, ingawa ameonya kwamba bado kundi hilo linaweza pia kufanya shambulizi la kigaidi. Amesema kwenye mahojiano hayo yaliyochapishwa Jumanne hii kabla ya kushiriki kwenye chakula cha jioni, kilichoandaliwa na waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi kwamba Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani unaendelea kupambana na kundi hilo la IS. 
 
Pentagon imeonya kwenye taarifa yake iliyotolewa jioni ya Jumatatu hii kwamba pamoja na operesheni hiyo kuanza vyema, bado kuna wasiwasi wa kukumbana na ugumu na itachukua muda mrefu. Jenerali wa juu kabisa wa Marekani, amesema itachukua wiki kadhaa ama hata zaidi. Msemaji wa serikali wa Marekani, Peter Cook amesema, viashiria vya awali vinaonyesha kuwa Iraqi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kuliko hata ilivyokuwa imepangwa katika siku ya kwanza tu ya mashambulizi.

Na Jijini London Uingereza, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir ameitaka serikali ya Iraqi kutowatumia wapiganaji wa Kishia kuingia kwenye mji wa Mosul unaokaliwa na raia kutoka madhehebu ya walio wengi ya Sunni, ili kuzuia mauaji ya kikatili. Amesema, hatua hiyo inaweza kuchochea machafuko ya kimadhehebu, na kuongeza kwamba anaihofia  hatari hiyo.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/DPAE/.
Mhariri: Daniel Gakuba

   


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW