Upungufu wa nishati wazusha hofu ya umaskini wa mafuta Ulaya
19 Oktoba 2021Kamishna wa masuala ya kazi wa Umoja wa Ulaya Nicolas Schmidt ameonya juu ya kuongezeka kwa kile kinachoitwa umaskini wa afuta barani Ulaya msimu huu wa baridi kutokana na kupanda kwa kasi kwa bei za nishati.
Idadi ya watu wanaoshindwa kupasha joto majumbani mwao inatarajiwa kuongezeka kutooakana na gharama kubwa za nishati.
Akizungumza na shirika la habari la DPA Schmidt amesema tayari kuna mamilioni ya watu Ulaya wanaoshindwa kupasha joto la kutosha majumbani mwao, na kuongeza kuwa idadi hii inaweza kuongezeka.
Wakati Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya inaweza kuyasaidia mataifa ya Umoja wa Ulaya kupunguza athari ya gharama kubwa za niashati kwa umma, Schmit alisema ni jukumu la msingi la serikali kuchukua hatua.
Familia inatajwa kuwa katika umaskini wa mafuta ua nishati pale wanachama wake wanaposhindwa kuipasha nyumba yao joto la kutosha kwa gahrama nafuu.
Mnamo Septemba Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Ulaya, ETUC, lilionya kwamba zaidi ya watu milioni 2.7 barani Ulaya hawamudu kupasha joto majumbani mwao kwa viwango vya kutosha licha ya kuwa na ajira.
Wiki iliyopita Ujerumani ilipunguza kodi yake kwa nishati jadidifu kwa theluthi moja. Kodi hiyo inachangia humusi moja ya bili za umeme kwa watumiaji nchini Ujerumani. Ufaransa kwa upande wake inatoa kiasi cha Euro 100 kwa familia zenye kipato cha chini kulipia gharama za ziada za upashaji majumba joto.
Ufufukaji wa uchumi wa dunia wapandisha gharama
Bei za gesi asilia na makaa ya mawe duniani zmefikia viwango vya juu kabisaa katika wiki za hivi karibuni, na bei ya mafuta imepanda hadi zaidi dola 80 kwa pipa.
Ongezeko hilo la bei limelaumiwa kwa ufufuaji wa kiuchumi kutokana janga la COVID-19 wakati mahitaji ya umeme katika uzalishaji yakisababisha uhaba wa ugavi kote duniani.
Baadhi ya wanasiasa wameilaumu Urusi, ambayo inasafirisha asilimia 50 ya gesi asilia katika Umoja Ulaya. Ugavi wa gesi ya Urusi ulizorota wakati wa janga la Corona na sasa imerudi katika viwango vya kawaida lakini haikidhi mahitaji ya ziada.
Uvumi unaendelea kwamba huenda Moscow inazuia usambazaji wa gesi ya ziada kuishinikiza Ujerumani izindue rasmi bomba la gesi la Nord Stream 2 kupitia Bahari ya Baltic, ambalo ujenzi wake ulikamilika mwezi uliopita.
Ujenzi wa bomba hilo ulikosolewa kwa madai kwamba kuna uwezekano wa kuifanya Ulaya kuitegemea sana gesi ya Urusi.
Umoja wa Ulaya hapo awali ulisema unaamini kuongezeka kwa bei ya nishati ni kwa muda mfupi na itapungua katika majira ya machipuko.
Chanzo: DW