1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yapinga madai ya 'kutoweka ustaarabu' wa Ulaya

15 Februari 2026

Mkuu wa sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amepinga dhana kuwa Ulaya inakabiliwa na „kutoweka kwa ustaarabu wake". Ametoa kauli hiyo kupinga ukosoaji unaofanywa na utawala wa Trump kuhusu bara hilo.

Kaja Kallas akizungumza katika mkutano wa usalama Munich
Mkuu wa sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amepinga dhana kuwa utamaduni wa Ulaya unatowekaPicha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Kallas amezungumza katika siku ya mwisho ya mkutano wa usalama mjini Munich, siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kutoa kile kilichoonekana kama ujumbe wa kuwatia moyo washirika wa Ulaya.

Alitumia lugha ya upole kuliko alivyofanya Makamu wa Rais JD Vance wakati akiwahutubia viongozi wa Ulaya katika mkutano huo mwaka jana. Hata hivyo Rubio amesisitiza nia ya Washington ya kuunda upya muungano wa kijeshi wa NATO na kushinikiza vipaumbele vyake vya sera.

Kallas aligusia ukosoaji katika mkakati wa usalama wa taifa wa Marekani uliotolewa Desemba, ambao ulidai kwamba kudorora kwa uchumi barani Ulaya "kumefunikwa na matarajio halisi na dhahiri zaidi ya kufutwa kwa utamaduni." Ulipendekeza kwamba Ulaya inadhoofika kutokana na sera zake za uhamiaji, kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, "udhibiti wa uhuru wa kujieleza na ukandamizaji wa upinzani wa kisiasa" na "kupoteza utambulisho wa kitaifa na hali ya kujiamini."

Rais wa Ukraine Zelensky asema ana matumaini mazungumzo ya wiki ijayo ya kutafuta amani ya Ukraine yatakuwa mazuriPicha: Ukranian Presidency/Anadolu/picture alliance

"Kinyume na kile ambacho baadhi wanaweza kusema, Ulaya iliyoamka, au kuharibika haikabiliwi na kupotea kwa utamaduni," Kallas aliambia mkutano huo. "Ukweli ni kuwa, watu bado wanataka kujiunga na klabu yetu na sio Wazungu wenzetu tu," aliongeza, akisema aliambiwa alipotembelea Kanada mwaka jana kwamba watu wengi huko wana nia ya kujiunga na EU.

Kallas alikataa kile alichokiita "kuishambulia Ulaya."

"Unajua, tunauendeleza ubinaadamu, tunajaribu kutetea haki za binaadamu na haya yote, ambayo kwa kweli yanaleta ustawi pia kwa watu. Kwa hivyo ndiyo maana ni vigumu sana kwangu kuamini shutuma hizi."

Katika hotuba yake ya mkutano, Rubio alisema kwamba kumalizika kwa enzi ya ushirikiano wa Marekani na Ulaya "sio lengo letu wala matakwa yetu," akiongeza kwamba "nyumbani kwetu kunaweza kuwa katika ulimwengu wa Magharibi, lakini tutakuwa watoto wa Ulaya kila wakati."

Aliweka wazi kwamba utawala wa Trump unashikilia msimamo wake kuhusu masuala kama vile uhamiaji, biashara na hali ya hewa. Na maafisa wa Ulaya waliohutubia mkutano huo waliweka wazi kwamba wao pia watasimama na maadili yao, ikiwa ni pamoja na mbinu yao ya uhuru wa kujieleza, mabadiliko ya hali ya hewa na biashara huru.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Rubio auambia mkutano wa Munich kwamba Marekani na Ulaya zinahitajiana Picha: Alex Brandon/REUTERS

Mkakati mpya wa usalama wa Ulaya

Kallas amesema anaufanyia kazi mkakati mpya wa usalama wa UlayaPamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen.

Mkakati huo utashughulikia "maeneo yote ya usalama wa Ulaya" ili kukabiliana vyema na tishio la Urusi na enzi yenye uaudi zaidi ya siasa za kikanda.

Ulinzi ni kipaumbele muhimu. "Hili linaanzia Ukraine, lakini tunajua mwisho wa vita vya Urusi si Donbas," alisema, akizungumzia madai ya vita mseto vya Urusi na hujuma ya miundombinu muhimu ya Ulaya.

Mkuu huyo wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya ametoa wito kwa wanachama wa EU kuubadili mtizamo wao linapokuja suala la ulinzi wa kitaifa. Amewahimiza kuwa na mtizamo wa Ulaya zaidi na sio wa kitaifa.

"Fikirieni kikanda kwa sababu tishio ni la Ulaya, kwa hivyo jibu linapaswa kuwa la Ulaya," alisema.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW