1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCroatia

EU yapongeza mafanikio makubwa ya Croatia

2 Januari 2023

Mkuu wa Umoja wa Ulaya aliitembelea Croatia jana kusherehekea kile alichokiita "mafanikio makubwa" ya taifa hilo changa la Umoja wa Ulaya. Croatia ilijiunga na kanda ya sarafu ya euro na Eneo la Schengen

Kroatien ist jetzt Euro- und Schengen-Land
Picha: Denis Lovrovic/AFP

Katika Siku ya Mwaka mpya, Croatia ilianza kutumia sarafu ya euro na kuwa mwanachama wa 27 wa eneo kubwa kabisa ulimwenguni la kusafiri bila pasipoti la Schengen. 

Soma pia:Croatia kuanza kutumia sarafu ya euro kuanzia Januari 2023

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen alikutana na viongozi wa Croatia na Slovenia katika kivuko cha mpaka cha Bregana baina ya nchi hizo mbili za Balkan, ambacho kiliwekwa wazi katika dakika za mwanzo za mwaka wa 2023 wakati eneo la usafiri huria la Schengen lilipanuliwa na kuijumuisha Croatia. Von der Leyen alisema ilikuwa siku ya kuandikwa kwenye vitabu vya kumbukumbu. "Kizazi kijacho cha Wacroatia kitakulia katika eneo la Schengen. Watu wataweza kusafiri kwa uhuru, biashara haitaathiriwa na ukaguzi. Usafiri usio na vizuizi utaleta matokeo yanayoonekana kwa watu wanaoshi mpakani, wanaofanya kazi katika pande mbili za mpaka au kuwa na familia katika pande zote za mpaka. Jamii zitaungana pamoja tena." Alisema von der Leyen

Kivuko cha mpaka cha Bregana kati ya Croatia na SloveniaPicha: Luka Stanzl/PIXSELL/IMAGO

Mnamo usiku wa manane Jumamosi, Croatia pia iliiweka pembeni sarafu yake ya kitaifa kuna, na kuwa mwanachama wa 20 wa sarafu ya euro inayotumiwa na watu milioni 347 barani Ulaya. Watalaamu wanasema kuanza kutumia sarafu ya euro kutasaidia kuulinda uchumi wa Croatia katika wakati ambao mfumko wa bei unaongezeka duniani kote baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kusababisha kupanda kwa bei za chakula na mafuta.

Lakini hisia miongoni mwa Wacroatia ni za mchanganyiko. Wakati wanakaribisha kuondolewa kwa udhibiti wa mipakani, baadhi wanahohofia kuhamia kwenye sarafu ya euro kutasababisha kuongezeka kwa gharama ya Maisha kwa sababu wafanyabiashara wataongeza wakati wanapobadilisha sarafu.

Maafisa wanatetea uamuzi wa kujiunga na kanda ya euro na Schengen, wakisema kwa kufanya hivyo, Croatia imekamilisha ushirikiano wake kamili katika Umoja wa Ulaya.

Watalaamu wanasema matumizi ya euro yatapunguza masharti ya kukopa wakati huu mgumu wa kiuchumi. Croatia ambayo ina jumla ya watu milioni 3.9 ilijiunga na Umoja wa Ulaya mwaka wa 2013.

Utanuzi wa Umoja wa Ulaya umekwama katika miaka ya karibuni. Lakini tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari mwaka jana, maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kuwa kuimarisha ushirikiano wa jumuiya hiyo na mataifa ya magharibi mwa Balkan ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika kudumisha usalama wa Ulaya.

DPA, Reuters, AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW