1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiPoland

EU yatenga bilioni 10 kwa nchi zilizoathiriwa na mafuriko

20 Septemba 2024

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema Umoja huo utatenga mabilioni ya fedha ili kuyasaidia mataifa ya Ulaya ya Kati yaliyokumbwa na mafuriko makubwa hivi karibuni.

Mitaa iliyofurika maji eneo la Glucholazy, kusini mwa Poland.
Mitaa iliyofurika maji eneo la Glucholazy, kusini mwa Poland.Picha: Sergei Gapon/AFP

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika mji wa Wroclaw nchini Poland, akiwa na viongozi wa nchi zilizoathirika na mafuriko hayo, von der Leyen amewahakikishia viongozi hao kuwa Ulaya itasimama nao wakati huu mgumu.

Amesema huu ni wakati wa uhitaji na kwamba ni lazima kwa viongozi wa Ulaya kuonyesha umoja ili kuikabili changamoto iliyowakumba.

Soma pia: Mafuriko Ulaya: Mji wa Dresden wa Ujerumani uko kwenye hali ya tahadhari

von der Leyen amesema kiasi euro bilioni 10 zitatolewa kwenye mfuko wa mshikamano wa Umoja wa Ulaya huku baadhi ya masharti yanayohusishwa na fedha hizo, kama vile ufadhili wa pamoja wa nchi wanachama, yataondolewa ili kurahisishwa mchakato huo.

Mafuriko mabaya zaidi kuwahi kuikumba Ulaya ya Kati katika muda wa miongo miwili yamesababisha uharibifu mkubwa kutoka Romania hadi Poland, huku watu wasiopungua 24 wakipoteza maisha.