1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaAfrika

EU yazindua mkakati wa kibiashara na Afrika

7 Machi 2024

Katika hatua ya kuifanya biashara izingatie haki za binaadamu pamoja na kulinda mazingira, Umoja wa Ulaya umezindua mpango mpya wa ubia na mataifa 11 ya Afrika.

Uganda | Mkutano wa kuzindua Makakati wa kibiashara wa EU mjini Kampala
Umoja wa Ulaya unalenga kujenga ushirikiano endelevu na unaojumuisha pande zote za kibiashara na nchi 11 za KiafrikaPicha: Lubega Emmanuel/DW

Lakini Rais Yoweri Museveni wa Uganda anakosoa mpango huo kuchanganya masuala ya kisiasa na biashara akisema kuwa masharti yanayojitokeza chini ya mkakati huo yatakwaza shughuli za biashara.

Soma pia: EU kuekeza zaidi ya dola milioni 60 kwa umeme Uganda

Kulingana na mpango huo wa kuwa na jukwaa maalumu la kibiashara kati ya mataifa ya bara la Ulaya na mataifa 11 ya Afrika, lengo ni kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya bara hilo na nchi kama Uganda unazingatia masuala ya haki za binaadamu pamoja na uhifadhi endelevu wa mazingira. Kwa mfano, mnyororo wa uzalishaji mazao au bidhaa unatakiwa kuhakikisha kuwa haki za binaadamu hazikiukwi kama vile kuwatumikisha watu kwa mishahara na mazingira duni. Aidha, mazao ambayo yametokana na misitu kufyekwa kutoa nafasi kwa mashamba ya mazao hayo hayatakubaliwa. Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo, kiongozi wa wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Uganda, Jan Sadek, amesema: "Mkakati huu wa kuwa na jukwaa maalum la kibiashara na mataifa mengine unalenga kuwepo kwa ukuaji endelevu wa uchumi na biashara unahusisha wadau wote kuzingatia mazingira na haki za binadamu."

Ijapokuwa Rais Museveni ameipongeza Ulaya kwa mpango huo ambao pia unazingatia kuimarisha uwekezaji na misaada ya kifedha kwa sekta binafsi, amekosoa masharti yanayohusiana na haki za binaadamu, akisema kuwa hicho kitakuwa kikwazo kikubwa kwa Afrika kunufaika: "Tunatakiwa kujenga uchumi unaotajirisha kila mtu lakini bila masharti na vigezo ambavyo si rahisi kutekelezwa yanayokosesha fursa zaidi."

Museveni ameipongeza Ulaya kwa mpango huo wa kibiashara na Afrika utakaoifaidi pia sekta ya kibinafsiPicha: Darko Vojinovic/AP Photo/picture alliance

Katika uzinduzi wa mpango huo nchini Uganda, miradi kadhaa inayolenga kutoa mtaji wa kifedha kwa biashara za makundi maalum kama vile wanawake na vijana wajasiriamali imesainiwa. Mkuu wa ujumbe wa Ulaya, Jan Sadek, ameongezea hivi: "Tunalenga kushughulikia changamoto zinazokwaza makundi ya wanawake na vijana na pia jamii za vijijini kwani ndiyo njia muafaka na kuwezesha kila mtu kuhusika katika ukuaji wa uchumi."

Akisaini mikataba hiyo kwa niaba ya Uganda, Rais Museveni amehimiza wanasiasa wa bara la Ulaya kutenga masuala ya biashara na siasa, akisema hicho ndicho chanzo cha mizozo pale mataifa ya Ulaya yanapozingatia kutumia malighafi za Afrika na kuweka sera zinazozuia mnyororo wa uzalishaji kuanzia Afrika: "Wanasiasa wa Ulaya wafahamu kuwa ni makosa kutanguliza siasa badala ya biashara katika mfumo wa maendeleo ya kiuchumi duniani."

Itakumbukwa kuwa bunge la Ulaya limekuwa katika mstari wa mbele katika kukosoa mpango wa Uganda kuchimba mafuta. Hii hasa imetokana na wanaharakati wa mazingira na haki za binaadamu kudai kuwa sekta hiyo itasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Kongamano la siku tatu kati ya mataifa ya Ulaya na Uganda, lililowashirikisha pia wafanyabiashara wa nchi hizo lilimalizika jana Alhamisi hapa mjini Kampala.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW