1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yazindua operesheni ya ulinzi katika Bahari ya Shamu

20 Februari 2024

Umoja wa Ulaya umezindua rasmi operesheni ya wanamaji ya kuzilinda meli za Bahari ya Shamu dhidi ya waasi wa Huthi. Mashambulizi ya kundi hilo yaliwalazimu mabaharia wa meli moja kuitelekeza meli na kuiharibu nyingine.

Ndege za kijeshi za Marekani aina ya B1-Bomber
Umoja wa Ulaya utaungana na Marekani na Uingereza katika kuzilinda meli za Bahari ya ShamuPicha: Christopher Ruano/picture alliance/Planetpi/Planet Pix/ZUMA Press Wire

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Ulaya itahakikisha uhuru wa kusafiri katika Bahari ya Shamu, ikishirikiana na washirika wake wa kimataifa.

Afisa mmoja alisema operesheni hiyo ya Ulaya itapewa jina la Aspides katika kigiriki, kumaanisa ngao, na itajumuisha manowari nne. Marekani tayari inaongoza muungano wake wa jeshi la wanamaji katika eneo hilo na imefanya mashambulizi ya kulipiza kwenye maeneo ya Wahuthi nchini Yemen, ikishirikiana na Uingereza.

Mashambulizi kadhaa ya Wahuthi yamevuruga usafiri wa meli katika Bahari ya Shamu, na kuzilazimu baadhi ya kampuni kutumia njia mbadala ikiwemo kuzunguka upembe wa kusini mwa Afrika safari inayochukua wiki mbili.

Jana jioni, Wahuthi walisema walizilenga meli tatu katika saa 24 zilizopita, ikiwemo meli iliyosajiliwa Uingereza ya Rubymar, meli inayomilikiwa na Marekani Sea Champion na Navis Fortuna walioielezea kuwa ya “Kimarekani.“

Wahuthi ambao wanaungwa mkono na Iran, na kudhibiti sehemu kubwa ya Yemen, wamekuwa wakitatiza safari za meli tangu Novemba katika kampeni wanayosema ni ya mshirikamo na Wapalestina wa Gaza wakati wa vita vya Israel na Hamas.

AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW