1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2013 : Ujerumani bingwa

29 Julai 2013

Wanawake wa Ujerumani mabingwa wa kombe la mataifa ya Ulaya, Euro 2013 na wanalinyakua taji hilo kwa mara ya nane. Marekani bingwa wa kombe la shirikisho la soka la mataifa ya Amerika ya kati na kaskazini CONCACAF.

Nadine Angerer (front L) and Anja Miitag (front R) of Germany celebrate with her team he victory of the UEFA Women«s EURO 2013 final soccer match between Germany and Norway at the Friends Arena in Solna, Sweden, 28 July 2013. Photo: Carmen Jaspersen/dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++
Timu ya taifa ya Ujerumani ya wanawake mabingwa wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa

Mlinda mlango Nadine Angerer aliokoa mikwaju miwili ya penalti na mchezaji wa akiba Anja Mittag aliyeingia badala ya Lena Lotzen alipachika bao la ushindi wakati Ujerumani ikiishinda Norway kwa bao 1-0 katika fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2013 mjini Stockholm.

Huu ni ushindi wa sita mfululizo kwa mabinti hao wa Ujerumani na fainali ya nne dhidi ya Norway. Ulikuwa mchezo mgumu na ambao ushindi ungekwenda upande wowote jana kama anavyosema kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Silvia Neid , ambaye amepachikwa jina la "Malkia Silvia".

Kocha wa timu ya Ujerumani Silvia NeidPicha: picture-alliance/dpa

"Nafikiri , ulikuwa mchezo ulio katika kiwango sawa kwa timu zote, ilikuwa ni fainali ngumu sana kwetu. Kile ilichokifanya timu hii inayoundwa na vijana, bila shaka kinanifanya nifarijike sana. Nadine amecheza katika kiwango cha juu kabisa katika mashindano haya. Katika fainali ameonesha uwezo wake kwa mara nyingine tena."

Norway ilikuja juu

Norway iliwabana sana Wajerumani kuanzia mwanzo wa mchezo huo, na kukosa nafasi nzuri ya kupata bao la kuongoza baada ya Trine Ronning kukosa mkwaju wa penalti baada ya Celia Okoyino Da Mbabi kuadhibiwa kwa kumsukuma Catherine Dekkerhus.

Mpambano kati ya Celia Okoyino da Mbabi wa Ujerumani (mbele) na Marit Fiane wa NorwayPicha: picture-alliance/dpa

Ikiwa chini ya mbinyo mkali Ujerumani ilimbadilisha Lena Lotzen na kuingia Mittag na ilimchukua mchezaji huyo wa akiba dakika nne kuiweka Ujerumani katika njia ya ushindi. Kocha Silvia Neid amesema.

"Hatimaye nimekuwa mwenye furaha sana, kwamba tumeweza kufanikiwa na kikosi hiki cha vijana, ambapo kimeonesha hamasa, na wote tumeweza kushuhudia."

Maumivu

Maumivu zaidi yaliwapata Norway dakika nne baadaye wakati goli la Ada Hegerberg lilipokataliwa kwa kuwa alikuwa ameotea. Timu ya Ujerumani ilikosa mara hii hali yake ya moto wa mapambano, iliweka wavuni mabao sita tu katika michezo sita, na hatimaye ilibidi kutegemea tu uwezo wa hali ya juu wa mlinda mlango Nadine Angerer kuweza kupata mafanikio.

"Katika wakati muafaka wa mashindano haya tumeweza kupandisha kiwango cha uchezaji kwa pamoja na tunaamini kuwa tunapaswa kusherehekea kwa kiwango cha juu, lakini pia tunastahili kusherehekea mara mbili zaidi."

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema katika ujumbe aliyomtumia kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Silvia Neid kuwa " anampongeza kocha huyo binafsi na timu nzima kwa ushindi wa nane wa ubingwa wa Ulaya."

Mabingwa wa CONCACAF

Nayo timu ya taifa ya Marekani chini ya uongozi wake kocha wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann imefanikiwa kunyakua taji la ubingwa wa mataifa ya America ya kati na kaskazini ya CONCACAF ya kombe la dhahabu baada ya kuishinda Panama kwa bao 1-0 katika fainali iliyofanyika jana.

Pamoja na kufurahishwa na ushindi huo , Wamarekani wana matumaini kuwa utakuwa ni changamoto kwao kuweza kukata tikiti katika fainali za kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Sizitaki ni mbichi

Kocha wa mabingwa wa Ulaya Pep Guardiola amesema kuwa timu yake haikujali sana kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya Borussia Dortmund katika taji la Super Cup nchini Ujerumani siku ya Jumamosi(27.07.2013), ikiwa ni marudio ya fainali ya kombe la mabingwa wa Ulaya Champions League miezi miwili iliyopita.

Mpambano wa Super Cup, Kocha wa Bayern Guardiola(kushoto) na Klopp(kulia)Picha: Getty Images

Ni kipigo cha kwanza kwa Mhispania huyo tangu kuchukua wadhifa wa kuifunza Bayern Munich kutoka kwa kocha wa zamani Jupp Heynckes, ambaye msimu uliopita aliiongoza timu hiyo ya mjini Munich kuwa timu ya kwanza ya Ujerumani kushinda mataji matatu muhimu ya msimu, ubingwa wa Ulaya , ubingwa wa ligi na kombe la shirikisho.

Guardiola amesema makosa madogo madogo yatarekebishwa kabla ya kuanza ligi ya Bundesliga tarehe 9 mwezi ujao.

Kocha wa Bayern Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya kuwa tumeshindwa lakini sijahisi kuwa Borussia wamecheza vizuri kuliko sisi. Amesema Guardiola.

Kocha wa Dortmund , Jurgen Klopp alionesha kufurahishwa na ushindi huo, hususan wakati timu yake ikiwa haikuweza kumchezesha mchezaji mpya wa kiungo Henrikh Mkhitaryan ambaye ni majeruhi. Ulikuwa mchezo mzuri, wachezaji wa timu zote walikimbia kama vile hawataishi tena kesho, alijigamba kocha huyo wa Dortmund. Akaongeza ni vizuri kushinda Super Cup, wakati mshindi anajisikia furaha na aliyeshindwa amekatishwa tamaa.

Tumeshinda, kitu ambacho ni kizuri sana na wakati tutakapocheza nao mjini Munich , tutataka pia kupata ushindi kwao, Ameongeza Jurgen Klopp.

Bastian Schweinsteiger ndie mchezaji bora wa mwaka nchini Ujerumani kwa mujibu wa uchaguzi uliofanywa na waandishi wa habari za michezo ulioendeshwa na jarida la michezo la Kicker nchini Ujerumani. Schweinsteiger alipata kura 92 kati ya 527 zilizopigwa, akimpita mchezaji mwenzake wa Munich Frank Ribery na Thomas Muller. Robert Lewandowski wa Borussia Dortmund alishika nafasi ya nne.

Mchezaji bora wa mwaka nchini Ujerumani Bastian SchweinsteigerPicha: Getty Images

Burundi kwenda CHAN

Timu ya taifa ya Burundi imefanikiwa kukata tikiti ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa mara ya kwanza mwishoni mwa juma. Burundi ilitoka sare ya Sudan kwa kufungana bao 1-1 jana mjini Omdurman. Burundi kwa sare hiyo imefanikiwa kupita kwa jumla ya mabao 4-3.

Sudan ni mahali penye baraka kwa Burundi baada ya timu ya Vital'O kunyakua ubingwa wa vilabu vya Afrika mashariki na kati CECAFA mwezi uliopita. Ushindi huo wa Burundi umeipa nafasi ya kushiriki katika fainali zitakazohusisha timu 16 katika miji ya Bloemfontein, Cape Town na Polokwane Januari mwakani.

Timu nyingine zilizokwisha kufuzu ni pamoja na Burkina Faso, Congo, Ghana, Libya, Mali, mauritania, Morocco, Nigeria na Uganda.

Fumbo lililoshindwa kufumbuliwa kwa muda wa miaka 125 kuhusiana na mfungaji wa goli la kwanza la ligi duniani limefumbuliwa kwa kuchapishwa kitabu kipya kinachomtambulisha James Kenyon , "Kenny" Devenport wa Bolton Wanderers kuwa ndio aliyetia wavuni bao la kwanza la ligi duniani. Mchezo wa kwanza wa ligi ulifanyika Septemba 8, 1888 wakati ligi ya Uingereza ilipoanza kwa michezo mitano ikiwa ni pamoja na mchezo kati ya Bolton Wanderers dhidi ya Derby County.

Mabingwa wapya wa America ya kusini Atletico Mineiro ilipata kibano cha kufungwa mabao 4-1 jana dhidi ya mahasimu wao wakubwa na watani wa jadi Cruzeiro katika mpambano ambao Mineiro iliteremsha dimbani kikosi chake cha pili. Ushindi huo wa Cruzeiro unaiweka timu hiyo katika nafasi ya juu ya ubingwa wa Brazil ikiwa na point 18.

Mbio za magari , Formula One:

Lewis Hamilton ameondoa ukame wake wa mataji, jana baada ya kushinda mbio za Grand Prix nchini Hungary na kufikia sawa na ushindi wa Michael Schumacher wa mara nne katika nchi hiyo. Dereva huyo wa Mercedes hakutarajia kupata ushindi wake wa kwanza tangu alipooata ushindi nchini Marekani Nivemba mwaka jana, na kusema kabla ya mbio hizo kuwa atahitaji miujiza , licha ya kuanza mbio hizo akiwa katika nafasi ya kwanza kwa mara ya tatu mfululizo.

Lewis Hamilton bingwa wa Grand Prix , HungaryPicha: AFP/Getty Images

Hamilton alimshinda Kimi Raikkonen wa timu ya Lotus na Sebastian Vettel, ambaye amezogea karibu na ushindi wake wa nne mfululizo wa Formula one.

Riadha.

Bingwa wa mbio fupi katika mashindano ya Olimpiki Usain Bolt amekubali changamoto kutoka kwa mkimbiaji wa mbio za masafa ya kati Mo Farah kukimbia katika mbio za hisani , akisema atakuwa tayari kupambana nae katika mbio za mita 600. Farah ambaye amepata tuzo ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 na 10,000 katika michezo ya Olimpiki mjini London mwaka jana alikuwa nyota katika michezo hiyo pamoja na Mjamaica Bolt, ambaye alishinda mbio za mita 100 na 200.

Mo Farah(kushoto) na Usain Bolt(kulia)Picha: picture-alliance/dpa

Tennis.

Serena Williams ameendelea kuwa juu katika orodha ya wachezaji wa mchezo wa tennis kwa upande wa wanawake hadi leo Jumatatu, kwa mujibu wa shirika la mchezo huo duniani WTA. Wakati huo huo Novak Djokovic ameongoza orodha ya wachezaji wa tennis kwa upande wa wanaume , akifuatiawa na bingwa wa Wimbledon Andy Murray na David Ferrer.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW