1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2016: Ujerumani yashinda kwa penalti

3 Julai 2016

Ujerumani imetinga katika nusu fainali ya Euro 2016 jana Jumamosi(02.07.2016) lakini kutokuwa makini katika upigaji penalti dhidi ya Italia nusura iwagharimu kabla ya Jonas Hector kuiokoa Ujerumani.

UEFA EURO 2016 Deutschland vs. Italien Jubel nach Elfmeterschießen
Wachezaji wa Die Mannschaft wakishangiria ushindi dhidi ya ItaliaPicha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Ujerumani ilikosa penalti tatu kabla ya kushinda kwa mikwaju 6-5 katika mikwaju 18 ya penalti wakati Hector alipoweza kufunga mpwaju wake mpira ukimpita mlinda mlango Gianluigi Buffon wa Italia na kukimbia kwa wachezaji wenzake waliokuwa wakimshangiria.

Katika nusu fainali itakayofanyika siku ya Alhamis, Ujerumani itakwaana na mshindi wa pambano la leo Jumapili baina ya wenyeji wa mashindano hayo Ufaransa na timu iliyowashangaza wengi katika mashindano haya ya Iceland .

Joshua Kimmich akishangiria baoa lake la penalti dhidi ya ItaliaPicha: picture alliance/GES/M. Gilliar

"Ni vigumu kuelezea, lakini nina furaha ya kupita kiasi kwamba mkwaju wangu uliingia wavuni," amesema Hector. "Hakuna watu wengi waliobakia. Nilitambua kwamba ni lazima nipige katika wakati fulani na moyo wangu ulikuwa unadundia mdomoni."

Ujerumani pia ilijivua uteja kwa mahasimu wao Italia, kwa kushinda kwa mara ya kwanza katika majaribio tisa.

"Ndio,ndio, ndio, jinamizi dhidi ya Italia limekufa," Gazeti la Bild la Ujerumani limeandika.

Jonas Hector akishangiria bao la ushindi kwa Ujerumani dhidi ya ItaliaPicha: picture alliance/dpa/C. Charisius

Rekodi ya mafanikio

Wajerumani wameendelea kushikilia rekodi ya mafanikio katika mikwaju ya penalti. Unahitaji kwenda nyuma hadi 1976, kwa mara ya kwanza waliposhindwa katika mikwaju ya penalti katika mashindano makubwa.

Kikosi cha kocha Joachim Loew kilionekana kuelekea katika ushindi baada ya Mesut Ozil kuufumania wavu wa Italia na kupata bao la kuongoza katika dakika ya 65, lakini katika wakati usioeleweka Jerome Boateng aliunawa mpira katika eneo la hatari.

Leonardo Bonucci kwa utulivu kabisa aliumimina mpira huo wavuni, dakika 12 kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika na mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 dakika 90 zilipowadia.

Mlinzi wa Italia Giorgio Chiellini akimlinda mario Gomez wa UjerumaniPicha: Reuters/C. Hartmann

Wakati hakukuwa na bao katika dakika za nyongeza , Ozil, Thomas Mueller na Bastian Schweinsteiger wote walishindwa kutumbukiza mpira kimiani kwa upande wa Ujerumani , ambao kwa kawaida wanategemewa sana katika umbali huo wa hatua 12 za mtu mzima.

Lakini baada ya Simone Zaza na Graziano Pelle kukosa kwa upande wa Italia na mkwaju wa Bonucci kupanguliwa na mlinda mlango wa Ujerumani Manuel Neuer, Matteo Darmian naye alishindwa kuutumbukiza mkwaju wake wavuni mwa Ujerumani na mkwaju huo wa tisa wa kikosi cha Azzurri ulisafisha njia kwa Hector kuwa shujaa wa Ujerumani.

Kijana mdogo mwenye sura ya kitoto Kimmich mwenye umri wa miaka 21, pia alifunga mkwaju wake wakati majina makubwa yalishindwa.

Wachezaji wenye uzoefu walishindwa na vijana wadogo walifanikiwa, kwa hiyo inawezekana kabisa," amesema kocha wa Ujerumani Loew.

Wenyeji wa mashindano

Wenyeji wa mashindano hayo Ufaransa macho yao yameelekezwa katika nafasi ya kuingia katika nusu fainali ya Euro 2016 lakini wanapaswa kuwa na wasi wasi wa kuangukia pua pale watakapotiana kifuani na wauaji wa vigogo Iceland wakati timu hizo zitakapokutana leo Jumapili (03.07.2016).

Mashabiki wa Iceland wakifurahia mashindano ya Euro 2016Picha: Getty Images/AFP/H. Kolbeins

Kikosi cha Didier Deschamps kinaingia katika robo fainali katika uwanja wa Stade de France wakipigiwa upatu kuvuka kikwazo hiki dhidi ya timu inayotoka katika nchi yenye wakaazi 330,000, na pia itapambana na Ujerumani katika nusu fainali ikiwa itashinda pambano la leo.

Lakini Iceland imeingia katika mashindano haya kama tufani na kuthibitisha uwezo wake kwa kuishangaza England katika duru ya timu 16, ikitoka nyuma na kushinda kwa mabao 2-1 mjini Nice.

"Sio kibahati Iceland kufika hapa," mlinda mlango wa kikosi cha Ufaransa "Les Bleus" Hugo Lloris amesema jana Jumamosi.

Kocha wa Ufaransa Didier DeschampsPicha: Reuters/P. Rossignol

Wachezaji kadhaa hawatashuka dimbani kuitetea Ufaransa leo. Wakati mlinzi Adil Rami anaadhabu ya kadi mbili za njano, kocha Deschamps anatarajiwa kumpa nafasi Samuel Umtiti mwenye umri wa miaka 22 ambaye anahamia Barcelona msimu ujao kucheza kwa mara ya kwanza mashindano ya kimataifa akishirikiana na Laurent Koscielny katika ulinzi.

Mbinyo inaongezeka kwa wenyeji wa mashindano wakati wakilenga kurudia mafanikio ya mwaka 1984 katika mashindano kama haya ya Euro na mwaka 1998 katika kombe la dunia kwa kushinda mashindano makubwa katika ardhi yao, wakati Iceland inaingia katika mchezo huo wakitaka tu kufurahia wakati wao mashindanoni.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid