1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2016 : Ureno mabingwa wa Ulaya

Admin.WagnerD11 Julai 2016

Eder wa Ureno aleta kilio kwa Ufaransa , kocha Fernando Santos asema hahitaji kucheza mchezo safi kushinda, alikuwa na lengo kamili baada ya kuchukua hatamu za kuifunza timu hiyo.

Portugal Lissabon Ankunft Nationalmannschaft EURO 2016 Cristiano Ronaldo
Nahodha wa Ureno CR7 Cristiano Ronaldo akinyanyua juu kombe la UlayaPicha: picture-alliance/dpa/P.Duarte

Mashindano makubwa kabisa ya soka barani Ulaya yamefikia mwisho jana Jumapili Julai 10, 2016 kwa mshangao wa mwisho katika mashindano hayo yaliyoleta mshangao kila mara katika muda wote wa mwezi mzima.

Mashindano hayo yalimalizika jana Jumapili kwa mshangao wa wengi ambapo Ureno iliwashangaza wenyeji wa mashindano hayo kwa kunyakua taji lao la kwanza katika historia la kombe la Ulaya - ikiwa ni mshangao wa mwisho katika mashindano hayo ambayo yamekuwa maafuru kwa timu ndogo kuviangusha vigogo, kuliko ubora wa mchezo wenyewe uwanjani.

Wachezaji wa Ureno wakiwasili nyumbani baada ya ushindi wao wa kombe la UlayaPicha: picture-alliance/dpa/M.Cruz

Pia mashindano hayo yalishuhudia ghasia nje ya uwanja na pia mashabiki walioleta furaha kwa watazamaji wa mchezo huo katika runinga, kujitokeza kwa baadhi ya wachezaji kuwa nyota wa kimataifa kama Antoine Griezmann, na mshambuliaji hatari Cristiano Ronaldo wa Ureno kuondolewa uwanjani kwa machela akibubujikwa na machozi lakini bado alifanikiwa hatimaye kunyanyua juu taji lake la kwanza akiwa na kikosi cha timu ya taifa.

Kwa ujumla hayo ndio yaliyojiri katika kinyang'anyiro hiki cha mwezi mzima kuwania taji la Ulaya.

Ureno imetawazwa kwa mara ya kwanza kuwa mabingwa wa Ulaya baada ya kuwasili katika fainali mbili, ambapo ya kwanza mwaka 2004 iliishia kwa Ureno kufungwa bao 1-0 nyumbani na Ugiriki na kupokwa taji hilo.

Wachezaji wa Ureno wakianika kombe lao hadharaniPicha: Reuters/R. Marchante

Kocha wa Ureno Ferdando Santos alipoulizwa kwamba aliwaambia nini wachezaji wake hadi kuweza kufanikiwa kulinyakua kombe hilo baada ya kutolewa nje nahodha wake Cristiano Ronaldo. Alikuwa na haya ya kusema.

"Sio tabia yangu kuficha kile ninachofikiri kwa hiyo niliwaambia wachezaji wangu kile ninachofikiri. Tuna vipaji , uwezo mkubwa na hiyo ndio italeta tofauti. Juun ya yote tuna timu imara. Tunapaswa kupambana kwa kiwango cha juu, kupambana kuliko wapinzani wetu, kukimbia zaidi kuliko wao, kucheza kwa uelewano zaidi, kuwa na malengo kuliko wao. Iwapo tutaweza kufanya hivyo , tunaweza kuwa na nafasi kuwa mabingwa. Itakuwa vigumu kwa mtu yeyote kuishinda Ureno.Huo ndio uliokuwa ujumbe wangu kila wakati na nina bahati kuwa na kundi hili la wachezaji."

Kuhusu nahodha wa Ureno Cristiano Ronaldo CR7 , kocha Santos alikuwa na haya ya kusema.

Cristiano Ronaldo aliumia na ilibidi nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mwingine katika dakika ya 25.Picha: picture-alliance/dpa/V. Pesnya

"Nahodha wetu alifanya juhudi kubwa. alikosolewa mara kadhaa. Lakini ana ari kubwa na leo amedhihirisha hivyo tena. Alijaribu kila uwezekano wa kibinadamu mara mbili kuendelea kucheza. Hakuweza kurejea lakini kuwapo kwake katika chumba cha kuvalia na katika benchi kulikuwa muhimu sana. Jinsi alivvyonisaidia kupeleka ujumbe kwa wachezaji wenzake. Jinsi alivyowapa moyo. Aliwaambia kwamba leo ilikuwa siku yetu. Aliamini mno kama mimi kwamba leo ilikuwa siku yetu."

Mfungaji bora

Antoine Griezmann alijitokeza kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo akiwa na mabao 6, mshambuliaji nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo alikuwa na hali ya kupanda na kushuka katika mashindano haya lakini alifunga mabao wakati muafaka na kuonesha uwezo wake binafsi pale alipohitajika sana.

Mashabiki wa Ureno wakifurahia ushindiPicha: Reuters/M. Dalder

Ureno ilitoka sare mara tatu katika michezo yake ya duru ya makundi na kuishia kuwa katika nafasi ya tatu hatimaye imeondoka na ushindi wa kombe hilo.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alipata taabu kuelezea kipigo hicho dhidi ya Ureno jana.

"Hakuna maneno ya kupunguza machungu, ni makubwa na magumu. Lakini hatuwezi kusahau njia tuliyopitia kufika hapa tulipofikia na hamasa ya kuungwa mkono na mamilioni ya watu wa Ufaransa. Ni vigumu pia kwa mashabiki wetu wote , tungependa kuwapa taji hili. Ni kweli kwamba wakati kuvunjika moyo kunakuwa kwa kiwango kikubwa , ni vigumu kuona mambo mazuri yaliyokuwapo. Ni wazi kabisa yalikuwapo, lakini hali iliyopo ni kuvunjika moyo. Ni vigumu, lakini ni katika kiwango cha juu, kwa hiyo ni lazima tuikubali."

Mfungaji bora wa mashindano hayo Antoine Griezmann akiwa na mabao 6Picha: Reuters/C. Hartmann

Ari ya timu na kuwa na mshikamano , kama kocha wa Wales Chris Coleman alivyosema , inaonekana kuwa ni maneno yaliyotumika sana, na wachezaji nyota wenyewe hawakuchoka kuelezea kwamba hawana lolote bila wachezaji wenzao.

"Ari ya timu" , halikuwa tu neno lililotumika sana. Lingine ni msemo wa zamani kwamba unaposhambulia unashinda mchezo , wakati unapolinda zaidi lango lako unashinda mataji.

hivyo ndivyo ilivyokuwa jana kama anavyoeleza kocha wa Ufaransa Didier Deschamps tena.

"Mshindi wakati wote anastahili ushindi. Nilishasema hayo kabla ya fainali, hawakufika hapa kwa bahati mbaya. Hii ni mara ya kwanza haya yanatokea, timu ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu katika awamu ya makundi inafikia kuwa mabingwa wa Ulaya.Kwa kweli, hawajashinda michezo mingi, lakini mwishoni wamekuwa mabingwa wa Ulaya. Wameshinda mchezo mmoja muhimu leo katika muda wa nyongeza. Siwezi kuondoa kitu chochote kutoka kwao, hawakufika hapa kwa bahati mbaya."

Cristiano Ronaldo akimkumbatia Ricardo Quaresma, karibu na kocha Santos(kushoto)Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Matarajio ya mashabiki

Mashindano haya ya Euro 2016 yalionekana kuwa mashindano ambayo wachezaji kama Paul Pogba, Cristiano Ronaldo na huenda Thomas Mueller wa Ujerumani wakitamba na kung'ara. Mueller , mfungaji bora katika kombe la dunia mwaka 2014 nchini Afrika kusini , hakupata bao wakati Ujerumani mabingwa wa dunia walipoachwa na bumbuazi na mshambuliaji wa Ufaransa Antoine Griezmann kwa kuwafunga mabao mawili mjini Marseille. Mueller alirejea nyumbani mikono mitupu akiwa hana lake katika michuano hii.

Slatan Ibrahimovic wa Sweden hakuonekana kuweza kuisaidia timu yake licha ya kuwa mshambuliaji hatari akiwa na Paris Saint-Germain.

Kocha wa Ufaransa Didier DeschampsPicha: Reuters/C. Platiau

England, Uhispania na Urusi zilionekana kushindwa kuonesha nini walichokitayarisha kuonesha uwanjani baada ya kuadhiriwa na timu ambazo zilionekana kuwa rahisi kuziweka kando.

Ghasia za mashabiki

Kiasi ya mashabiki 40 walikamatwa mjini Paris jana Jumapili baada ya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi na mabomba ya maji dhidi ya mashabiki waliokuwa wakirusha chupa kwa polisi katika eneo maarufu la mnara wa Eiffel wakati wa fainali hizo za Euro 2016.

Mashabiki wa Urusi wakifanya fujoPicha: Getty Images/C. Court

Makundi ya mashabiki , baadhi wakijifunika bendera za Ufaransa ama Ureno , walikusanyika chini ya mnara huo maarufu na baada ya Ureno kupachika bao lao la ushindi na kuzuiwa kuingia katika eneo hilo la mashabiki ambalo lilikuwa na karibu mashabiki 90,000 fujo zilianza.

Lakini katika mashindano haya kumekuwa na mambo kadha ya mashabiki kufanya fujo, ambapo tulishuhudia mashabiki wa England na Urusi wakipambana na kisha pia mashabiki wa Croatia kufanya fujo.

Pamoja na hayo yote, mashindano hayo yalimalizika salama licha ya kitisho cha mashambulizi ya kigaidi na baada ya jamvi kukunjwa Ureno wanasherehekea taji lao la kwanza la mashindano makubwa ya soka duniani.

Tennis

Kwa upande wa Tennis , Andy Murray amefanikiwa kupata taji lake la pili la mashindano ya Wimbledon kwa kumshinda bila taabu Milos raonic wa Canada kwa seti 3-0 kwa 6-4 . 7-6 na 7-6.

Mskochi Andy Murray , ambaye anashikilia nafasi ya pili nyuma ya Novak Djokovic katika orodha ya wachezaji bora wa mchezo huo, sasa anashikilia mataji matatu katika mashindano makubwa akimshinda Raonic kwa mara ya sita mfululizo. Ni taji lake la pili la Wimbledon katika majaribio manne ya Wimbledon.

Andy Murray akinyanyua kombe la tennis la WimbledonPicha: Reuters/T. O'Brien

Murray pia alishinda mashindano ya US Open mwaka 2012 na kuandika historia mwaka mmoja baadaye akiwa Muingereza wa kwanza katika muda wa miaka 77 kushinda mashindano hayo ya Wimbedon yanayofanyika nchini Uingereza.

Wanariadha na Doping

Na katika riadha , shirika la Uingereza la kupambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli kwa wanamichezo , limefungua uchunguzi kuhusiana na taarifa za gazeti moja zinazodai kwamba madaktari nchini Kenya waliwapatia wanariadha wa Uingereza dawa zilizopigwa marufuku za kuongeza nguvu misuli.

Picha zilizochukuliwa kwa siri na gazeti la Sunday Times zinaonesha madaktari wawili wa Kenya na mshirika wao wakidai kweamba waliwapa wanariadha wa Uingereza dawa zinazoimarisha wingi wa damu mwilini ambazo zilipigwa marufuku zijulikanazo kama EPO.

Gazeti la Sunday times pia limesema lina picha za maboksi ya EPO matupu ambayo yametupwa katika kituo cha mazowezi katika eneo la nyanda za juu nchini Kenya la Iten, magharibi mwa nchi hiyo , ambako wanariadha wa Uingereza walikuwa wanakaa.

Kwa taarifa hiyo ndio nafikia tamati ya habari hizi za michezo jioni ya leo. Jina langu ni Sekione Kitojo , kwa habari zaidi tembelea tovuti yetu www.dw.de Kiswahili michezo upate habari nyingine kem kem za michezo. Kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga