1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro 2022: Uholanzi na Sweden zatoka sare

10 Julai 2022

Mabingwa watetezi wa michuano ya Euro ya wanawake Uholanzi wametoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Sweden katika mechi iliyochezwa uwanjani Bramall Lane, Sheffield.

UEFA Frauenfussball Euro 2022 I Niederlande gegen Schweden
Picha: Franck Fife/AFP

Sweden walikuwa wakitafuta kulipiza kisasi baada ya kubanduliwa nje na Uholanzi katika hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia miaka mitatu iliyopita.

Mechi hiyo imesajili rekodi ya mashabiki kwa mechi ya makundi ambayo haimuhusishi mwenyeji kwa mashabiki 21,342.

soma Euro 2022: England wapata ushindi mwembamba dhidi ya Austria

Matarajio ya mechi hii yalikuwa makubwa huku ikitazamiwa kama mechi kubwa katika hatua ya makundi, hata hivyo ilianza kwa kasi ndogo.

Mambo yalianza kuwa magumu wakati mlinda mlango na nahodha wa Uholanzi Sari Van Veenendaal kutolewa uwanjani kutokana na jeraha, lakini mchezaji aliyeingia na kuchukua nafasi yake Daphne Van Domselaar aling'ara katika mechi yake ya pili pekee ya kimataifa.

Kila mwamba ngozi huvutia kwake

Picha: Lee Smith/REUTERS

Katika kipindi cha kwanza Sweden ilidhihirisha kwanini inaorodheshwa ya pili  katika timu bora duniani na moja kati ya timu bora katika mashindano haya.

Mchezaji wa Sweden Kosovare Asllani pamoja na mshambuliaji wa Barcelona Firdolina Rolfo walijaribu kuvunja ngome ya Uholanzi lakini kipa Van Domselaar alikuwa imara langoni.

Shinikizo la Sweden hatimaye lilizaa matunda kunako dakika ya 35 wakati ujanja wa Asllani ulipofungua safu ya ulinzi ya Uholanzi na krosi yake ikaunganishwa na Andersson na kupachika wavuni bao la kwanza.

Kocha wa Uholanzi Mark Parsons amekosolewa kwa kushindwa kufikia viwango vilivyowekwa na kocha wa zamani Sarina Wiegman, tangu alipoondoka na kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya wanawake ya England.

Katika kipindi cha pili mshambuliaji wa klabu ya Arsenal Miedema alionyesha utashi wake wa kubadilisha mchezo na kunako dakika ya 52 mchezaji Jill Roord aliisawazishia Uholanzi.

Mechi nyengine za kundi C

Picha: Pro Sports Images/IMAGO

Katika mechi nyengine ya kundi C, Ureno imetoka sare ya 2-2 na Uswizi katika mechi yake ya kwanza ya michuano ya mabingwa wa Ulaya jana Jumamosi.

Uswizi walikuwa na mwanzo mzuri katika kipute hicho wakati mchezaji Coumba Sow alipomuacha hoi mlinda lango wa Ureno Ines Pereira kunako dakika ya pili ya mchezo na kufunga bao la kwanza. Dakika tatu baadaye Rahel Kiwic aliongeza la pili.

Hata hivyo katika kipindi cha pili Ureno ilipata bao la kwanza dakika ya 58 lilifungwa na Diana Gomes Na mchezaji Jessica Silva kupachika wavuni bao la pili na hatimaye mechi hiyo kukamilika kwa sare ya 2-2.

Matokeo hayo yanaziacha timu zote mbili zikiwa na pointi moja kila mmoja katika kundi C. Huku Sweden na Uholanzi zikipigiwa upato zaidi kutinga hatua ya mchujo.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi