1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUturuki

EURO 2024: Turkey na Netherlands zatinga robo fainali

Sylvia Mwehozi
3 Julai 2024

Uturuki itakutana na Uholanzi katika robo fainali ya michuano hii ya Ulaya baada ya kupata ushindi wa kusisimua wa mabao 2-1 dhidi ya Austria.

Wachezaji wa Uturuki wakishangilia kufuzu robo fainali
Wachezaji wa Uturuki wakishangilia kufuzu robo fainaliPicha: Darko Vojinovic/AP Photo/picture alliance

Nchi zote mbili za Uturuki na Uholanzi zimefuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2008. Merih Demiral alikuwa shujaa asiyetarajiwa wa Uturuki, baada ya kuifungia timu yake mabao yote mawili katika kipindi cha kwanza na cha pili.

Timu zote mbili zilipata nafasi ndani ya sekunde 30 za kwanza huku Demiral akifanikiwa kufunga bao la mapema mnamo dakika ya kwanza baada ya safu ya ulinzi ya Austria kushindwa kukabili mpira wa kona.Bellingham: Natumai nimewafunga mdomo wakosoaji

Austria ilifanya juhudi za kutafuta bao la kusawazisha lakini wachezaji wa Uturuki waliweka ulinzi mkali langoni na huenda wangefunga zaidi huku nyota wake Arda Guler akijaribu bahati yake kutoka mbali na Demiral kidogo afunge kutokea mpira wa kona.

Mchezaji wa akiba wa Austria aliyeingia kutokea benchi Michael Gregoritsch aliifungia timu yake bao pekee mnamo dakika ya 65 ya mchezo.

Kocha wa Austria Ralf Rangnick akimfariji Michael Gregoritsch baada ya kipenga cha mwishoPicha: Thanassis Stavrakis/AP Photo/picture alliance

Timu zote mbili zilicheza bila ya manahodha wao. Nahodha wa Uturuki Hakan Calhanoglu anatumikia adhabu ya kadi za njano huku David Alaba wa Austria, akiwa bado anauguza jeraha la goti lililomzuia kucheza michuano hiyo.

Beki wa Uturuki Kaan Ayhan ambaye alichukua mikoba ya unahodha alisema baada ya mechi kwamba "ulikuwa mchezo mgumu na Austria walikuwa wapinzani wakali zaidi."EURO 2024: Ujerumani yatinga robo fainali lakini hali bado ni tete

Kocha wa Uturuki Vincenzo Montella alisema kuwashinda Austria 2-1 na kutinga robo-fainali ya Euro 2024 ilikuwa ni zawadi maalum baada ya kuchapwa na wapinzani hao katika mechi ya kirafiki mnamo mwezi Machi walipofungwa mabao 6-1.

Katika mchezo wa awali baina ya Uholanzi na Romania, timu hiyo ya rangi ya machungwa imefuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka 16 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Romania.

Cody Gakpo ndiye alikuwa wa kwanza kufumania nyavu za Romania dakika ya 20 huku Donyell Malen aliyeingia kutoka benchi akifunga magoli mawili na kuipeleka timu hiyo katika hatua inayofuata.Mbappe ahofia wapinzani kuilenga pua yake

Kocha wa Uholanzi Ronald Koeman amesema mchezo wa leo ulikuwa bora na kwamba wanahitaji nafasi ili kuendelea katika michuano hii.

Wachezaji wa Uholanzi wakifurahia ushindi dhidi ya RomaniaPicha: Fiona Noever/REUTERS

Timu hiyo imeonyesha mchezo mzuri ukilinganisha na namna walivyoanza katika hatua ya makundi ambapo walichapwa na Austria mabao 3-2.

Romania wanaondoka katika michuano hiyo wakijivunia mafanikio yao baada ya kuwa kileleni mwa mechi zao za kufuzu kabla ya mchuano na kisha kuongoza kundi kuelekea hatua ya mtoano.

Robo fainali nyingine itakuwa kati ya wenyeji Ujerumani itakayocheza na Uhispania, Ufaransa wanakutana na Ureno siku ya Ijumaa huku England ikikipiga na Uswisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW