1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro Billioni 50 kutumika kuupiga jeki uchumi wa Ujerumani

Miraji Othman14 Januari 2009

Serikali ya mseto ya vyama vikuu viwili hapa Ujerumani, CDU/CSU na SPD, imeupitisha mpango mkubwa kabisa wa kuupiga jeki uchumi kuwahi kuonekana hapa nchini. Kutokana na mpango huo, serekali itatoa Euro bilioni 50.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, na waziri wa maswala ya nje wa ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: AP


Jambo hilo lilikubaliwa katika mkutano wa viongozi wa vyama hivyo baada ya mashauriano yaliodumu saa sita. Jana Kansela Angela Merkel aliuwasilisha mpango huo hadharani, akiwa pamoja na makamo wa kansela, ambaye pia ni mtetezi wa ukansela katika uchaguzi ujao kwa tiketi ya Chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier, na pia kiongozi wa chama cha CSU, Horst Seehofer.


Ulikuwa mkutano wa watu hao watatu mbele ya waandishi wa habari wa mjini Berlin. Wanasiasa hao walionesha kukubaliana na kuridhika, lakini hawakuhepa kujisifu. Mtetezi wa ukansela kwa tiketi ya Chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier, alisema mpango huo ni mchanganyiko uliotungwa kwa umahiri. Kiongozi wa CSU, Horst Seehofer, hajachelea kuhakikisha jambo hilo. Naye Kansela Angela Merkel hajatafuna maneno. Alisema kwamba bila ya kuchukuwa hatua, ingekuwa sio mbadala.; serekali ya Ujerumani, kama vile nchi nyingine, lazima ichukuwe hatua kukabiliana na mzozo wa kiuchumi ulioko:


" Hatua kama hiyo ilio na nguvu, mtu anaamuwa kuichukuwa tu pale anapoamini kweli kwamba kuna mzozo mkubwa. Nami siwezi kuchukuwa dhamana kuacha kuona kwamba katika upande huu kunajengwa daraja, na kuangalia huenda maelfu au mamia kwa maelfu ya watu wanapoteza nafasi za kazi, bila ya sisi kuchukuwa hatua ifaayo."


Mtetezi wa ukansela wa Chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier, anaiona pia Ujerumani, licha ya mzozo wa kiuchumi ulioko, imesimama vizuri, kiuchumi, hasa ukilinganisha na nchi nyingine za Ulaya:


"Sisi hapa Ujerumani maisha tuna nguvu za kuchukuwa hatua, na katika mzozo kama huu tunaweza tukawa ni dira. Pale ninapoiangalia Ulaya hii, basi sioni nani na vipi kunaweza kufanywa uzuri zaidi kuliko tunavofanya sisi."


Licha ya kukubaliana huko kote, vyama viliomo katika serekali ya mseto vinajipigia debe venyewe. Katika mwaka huu wa 2009, ambapo kutafanywa chaguzi nyingi za mabunge ya mikoa na bunge la Shirikisho, kila upande utajipongeza kutokana na mashauri yaliofanyika, japokuwa kwa kiwango fulani. Chama cha SPD kimeweza kufanikwa kwamba familia na watu wenye vipato vya chini watapunguziwa mzigo. Kinafurahia, kwa mfano, kwamba sasa kila familia italipwa zawadi ya Euro 200 kwa kila mtoto, na wenye vipato vya chini watapunguziwa kodi.


Nao vyama vya Ki-Conservative vinaweza kuashiria mafanikio. Mpango wao umeweza kukubaliwa. Sasa ni baada ya kipato cha Euro alfu nane kwa mwaka ndipo kodi ya mapato itakapodaiwa, badala ya kima cha sasa cha mapato ya Euro 7,660 kwa mwaka. Kwa ujumla, serekali ya muungano inakisia kwamba familia yenye watoto wawili baadae itaweza kutia mfukoni Euro 500 kwa mwaka.


Kiini kingine cha mpango huo wa kuupiga jeki uchumi ni kwamba baina ya Euro bilioni 17 hadi 18 zitatumiwa na serekali katika kujenga miundo mbinu, shule, shule za chekechea na barabara. Hali hiyo itahakikisha kuweko nafasi za kazi. Pia motisha wa kifedha watapewa watu wenye magari yaliozeeka ili wabadilishe magari yao kwa magari mepya. Kila mmoja wao atapewa Euro 2,500 kutoka serekalini. Pia imekubaliwa kwamba serekali ibebe dhamana kwa mikopo ya gharama ya Euro bilioni 100 itakayotolewa kwa makampuni ya Kijerumani ambayo ni imara, lakini yako katika mkwamo wa kutopata mikopo.


Chama cha Kijani kimeuita mpango huo wa serekali ya mseto kuwa ni ujanja wa hapa na pale, na kiongozi wa chama cha kiliberali cha FDP, Guido Westerwelle, alisema mpango huo hautoi sura ya mafanikio kwa serekali ya mseto:


"Mwaka huu kodi zitapunguwa kwa kiwango cha Euro bilioni tatu. Ukitia hesabu, hiyo ina maana kila familia itapunguziwa kodi kwa Euro 3.10. Hiyo ni bei ya sausage, bila ya pili pili na bila ya chips. Hali hiyo itapelekea watu Ujerumani kukwepa kutumia fedha madukani."


Shirikisho la vyama vya wafanya kazi hapa Ujerumani linalalamika kwamba uwekezaji ulioelezewa na mpango huo wa serekali hautoshi. Pia Jumuiya ya wanaviwanda na wafanya biashara hazijaipigia vigelegele serekali. Jumuiya hizo zilisema uchumi ulihitaji serekali iwapunguzie sana wananchi kodi za mapato.

Miraji Othman


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW