1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro milioni 400 kusaidia wahanga wa mafuriko Ujerumani

21 Julai 2021

Baraza la Mawaziri nchini Ujerumani limeidhinisha kitita cha mamilioni ya Euro kuwasaidia wahanga wa maafa ya mafuriko na kuahidi kuwa kazi ya kuyajenga upya maeneo yaliyoathiriwa na janga hilo itaanza mara moja.

Deustchland Berlin | Kabinettssitzung Angela Merkel
Kansela Angela Merkel kabla ya kuongoza kikao cha Baraza la Mawaziri mjini BerlinPicha: Annegret Hilse/dpa/picture alliance

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf Scholz ametangaza kuwa kiasi Euro milioni 400 zimeidhinishwa leo kuwasaidia watu kukabiliana na madhara yaliyotokana na mafuriko makubwa yaliyolikumba eneo la magharibi mwa Ujerumani.

Majimbo mawili ya Rhineland Palatinate na North Rhine-Westphalia ndiyo yameshuhudia uharibifu usio na mfano wa mafuriko ya wiki iliyopita.

Scholz amesema nusu ya kiasi hicho cha fedha kitatolewa na serikali kuu mjini Berlin na nusu nyingine itatolewa na serikali za majimbo yaliyokumbwa na maafa hayo.

Mkuu huyo wa hazina ya taifa amearifu kuwa serikali kuu na za majimbo zitakuwa tayari kuongeza msaada zaidi wa kifedha iwapo mahitaji yatakuwa makubwa.

Msaada unafuatia ziara ya pili ya Kansela Merkel kwenye maeneo ya maafa

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Olaf Scholz Picha: Luca Bruno/AP Photo/picture alliance

Akizungumzia nia ya serikali ya kuhahakikisha msaada huo unawafikia haraka wahanga wa mafuriko Scholz amesema "Serikali za majimbo ndiyo zitaratibu msaada huu. Utatolewa haraka bila urasimu."

Pia ameahidi hawataweka mifumo ya serikali ya shirikisho katika kuidhinisha kutolewa kwa msaada huo na badala yake serikali kuu itahakikisha fedha zinakuwepo na zinawafikia haraka wale wenye wanaozihitaji

Msaada huo wa kifedha umetangazwa siku moja tangu Kansela Angela Merkel alipofanya ziara ya pili kwa kulitembelea jimbo la North Rhine-Westphalia ambalo ni miongoni mwa maeneo yaliyoshuhudia uharibifu mkubwa uliotokana na mafuriko.

Akiwa mjini Euskirchen jana, Bibi Merkel alisema serikali yake inatoa kipaumbele cha kupelekwa haraka kwa msaada wa dharura kwenye maeneo yote yaliyokubwa na maafa.

Kazi ya ujenzi na ukarabati inatarajiwa kuwa ngumu na ya gharama 

Uharibifu uliotokana na mafuriko ni mkubwaPicha: Christof Stache/AFP/Getty Images

Hadi leo Jumatano watu wasiopungua 171 wamekufa na mamia wengine badi hawajulikani waliko baada ya mvua kubwa ya Jumatano iliyopita kusababisha mafuriko ambayo hayashuhudiwa kwa miaka mingi nchini Ujerumani.

Miundombinu muhimu ikiwemo barabara, njia reli, madaraja, shule, hospitali na makaazi ya watu vimeharibiwa vibaya na janga hilo.

Ama kuhusu mipango ya ujenzi mpya na ukarabati wa miundombonu iliyoathiriwa na mafuriko viongozi wa serikali nchini Ujerumani wamesema wanatarajia kazi itaanza haraka iwezekanavyo  lakini wameutaka umma kuwa subira kwa sababu gharama zinatarajiwa kuwa kubwa na zoezi hilo huenda litachukua muda mrefu.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani  Horst Seehofer amesema anatumai tathmini ya awali ya uharibifu ulitokea  itakamilika mwishoni mwa mwezi Julai na wakuu wa serikali za majimbo watakutana kujadili hatua za kuchukua.

Kwa mujibu wa serikali, gharama za ujenzi na ukarabati wa maafa yaliyotokea wakati wa mafuriko ya mwaka 2013 ilifikia Euro bilioni 6 na inakadiriwa kazi kama hiyo itagharimu fedha nyingi zaidi kutokana na ukubwa wa maafa ya mwaka huu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW