Euro milioni 500 kusaidia kuhifadhi misitu iliyo hatarini
28 Mei 2008Kansela Angela Merkel amesema,Ujerumani imedhamiria kuweka shabaha maalum ili Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa kutaka kuzuia mimea na viumbe kutoweka duniani,yaweze kutekelezwa ifikapo mwaka 2010.
Serikali ya Ujerumani,kati ya mwaka 2009 na 2012 itatoa mchango wa hadi Euro milioni 500 kusaidia kuhifadhi misitu iliyo katika hatari ya kutoweka duniani.Na kuanzia 2013 Euro milioni 500 zingine zitawekwa kando kila mwaka.Pesa hizo zitatumiwa katika maeneo ambako misitu na mifumo mingine ya ekolojia ipo hatarini na vile vile kutafuta njia za kuhifadhi misitu hiyo na viumbe vinavyoishi huko.Lakini Ujerumani haiwezi kuubeba mzigo huo mkubwa peke yake.Merkel amezihimiza nchi zingine pia zichukue hatua za uasisi kuhifadhi mimea na viumbe mbali mbali vilivyo hatarini.Akaongezea:
"Katika miaka iliyopita tulipanga malengo muhimu,lakini sasa pia ni wakati wa kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatimizwa.Kwa hivyo mkutanoni Bonn tunahitaji kupitisha maamuzi ya mwongozo. "
Kansela Merkel akasisitiza kuwa lazima uwepo uwiano katika juhudi za nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda na nchi masikini zinazoendelea.Amesema,jitahada za kuokoa mimea na viumbe zinatoa nafasi ya kufanywa mageuzi ya kiuchumi na umasikini kupigwa vita.
Kwa upande mwingine,Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya,Jose Manuel Barroso amesisitiza uhusiano uliopo kati ya kutoweka kwa viumbe na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Ulimwengu unapaswa kutambua umuhimu wa kiuchumi katika kuhifadhi misitu pamoja na mimea na viumbe mbali mbali vinavyotegemeana.Amesema,uhai anuai ni msingi wa uchumi wetu kwa hivyo raslimali hiyo ya umma isiteketezwe.
Kiasi ya wajumbe 6,000 kutoka nchi 191 wanahudhuria mkutano wa uhai anuai uliofunguliwa siku 11 zilizopita mjini Bonn.Hii leo mawaziri 87 wameanza majadiliano ya kisiasa kwa azma ya kutayarisha mswada wa makubaliano mapya ya kimataifa juu ya njia za kuhifadhi misitu pamoja na viumbe vinavyoishi humo.Wanasayansi wanaonya kuwa baadhi ya mimea na viumbe vinatoweka kwa kasi.Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhai anuai ulizinduliwa wakati wa Mkutano wa kilele wa Mazingira mjini Rio de Janeiro mwaka 1992.