FA ya Ujerumani yasema kususia Kombe la Dunia si sahihi
28 Januari 2026
Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) limevunja ukimya wake kuhusu uwezekano wa kususia Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Marekani majira ya joto mwaka huu, huku baadhi ya mechi zikitarajiwa kuchezwa pia nchini Mexico na Kanada.
Akizungumza katika mkutano wa Ligi ya Soka ya Ujerumani (DFL) uliofanyika Jumatatu, Rais wa DFB Bernd Neuendorf alisema: "Sidhani kama huu ni mjadala mkubwa hata kidogo, kwa sababu naamini sisi ndani ya DFB tuna msimamo wa pamoja kwamba mjadala huu kwa sasa hauna mwelekeo sahihi kabisa.”
Rais wa DFL, Hans-Joachim Watzke, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alisema huu si wakati muafaka wa kujadili suala hilo.
"Wakati utakapofaa, tutalijadili, lakini kwa mtazamo wangu, kwa sasa mjadala huu hauna nafasi,” alisema Watzke.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich, Jan-Christian Dreesen, ambaye alirejea Kombe la Dunia la mwaka 2018 nchini Urusi, lililochezwa miaka minne baada ya nchi hiyo kuiteka Crimea kutoka Ukraine.
Dreesen aliongeza kuwa haoni sababu kwa nini Ujerumani isishiriki mashindano ya mwaka huu, akisisitiza kuwa masuala ya siasa za kimataifa yanapaswa kushughulikiwa kwingine.
Miito ya kususia yaongezeka
Wito wa kususia umeendelea kuongezeka nchini Ujerumani na Ulaya, kufuatia msimamo wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Greenland, na zaidi hivi karibuni baada ya shambulio la pili la risasi lililotokea Minneapolis na maafisa wa idara ya uhamiaji na forosha, ICE, ambalo limesababisha hasira na upinzani mpana dhidi ya utekelezaji mkali wa sheria za uhamiaji nchini humo.
Mtazamo wa jumla ni kwamba, kufuatia mgomo wao nchini Qatar na kutokana na hali ya kudhoofika kwa Umoja wa Ulaya, uwezekano wa kususia bado ni mdogo. Hata hivyo, hilo halijazuia baadhi ya sauti ndani ya Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) kutoa maoni yao waziwazi. Makamu wa Rais wa DFB na Mwenyekiti wa klabu ya St Pauli, Oke Göttlich, alisisitiza msimamo wake kuhusu suala hilo katika mkutano wa DFL.
"Kwa maoni yangu binafsi, ningeshauri kutoelekea huko kwa kuzingatia hali ilivyo sasa nchini Marekani,” Göttlich aliliambia shirika la habari la Sportschau.
"Huenda nikatofautiana na wenzangu wengi. Lakini mimi pia ni muumini wa demokrasia ninayeweza kuelewa endapo, mwishowe, wengi wataamua kwamba kususia huenda si ujumbe sahihi kwa soka la Ujerumani,” aliongeza.
Neuendorf alimkosoa Göttlich kwa kutowasilisha kwanza maoni yake ndani ya Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB).
"Hajakaa nasi kwa muda mrefu sana. Lakini kwa kawaida, masuala kama haya hujadiliwa kwanza ndani ya kamati husika, kisha ndipo tunaunda msimamo. Kwa bahati mbaya, safari hii amewahi kutoa msimamo wake kabla ya mjadala huo,” alisema Neuendorf.
Wakati huo huo, aliyekuwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter, hivi karibuni aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa naye anaunga mkono wazo la mashabiki kususia Kombe la Dunia. Baadhi ya mashabiki hawawezi kusafiri kufuatia marufuku ya safari iliyosasishwa hivi karibuni na utawala wa sasa wa Marekani.