1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Facebook, Twitter zamlenga Trump 'kwa habari za kupotosha'

6 Agosti 2020

Kampuni ya mawasiliano ya mtandao ya Facebook imefuta chapisho la rais Donald Trump ambalo kampuni hiyo inasema lilikiuka sheria zake kuhusu habari za kupotosha kuhusiana na virus vya corona.

Symbolfoto für Fake News
Picha: imago images/ZUMA Wire

Kampuni hiyo imesema kuwa chapisho hilo lilijumuisha kanda ya video kutoka katika mahojiano ya kipindi cha televisheni cha Fox and Friends ambapo Trump alidai kuwa watoto wana 'kinga' dhidi ya ugonjwa wa COVID-19. Msemaji wa kampuni hiyo ya Facebook amesema kuwa kanda hiyo ya video inajumuisha madai ya uongo kwamba kundi la watu fulani lina kinga dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 hatua inayokiuka sera zao kuhusu habari za kupotosha kuhusiana na ugonjwa huo.

Wakati huo huo kampuni ya Twitter pia ilifunga akaunti rasmi ya kampeni ya rais huyo kuhusiana na ujumbe unaojumuisha video hiyo ambapo Trump alitangaza kuhusu kufunguliwa kwa shule mnamo mwezi Septemba. Msemaji wa kampuni hiyo katika tawi la San Fransisco, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba ujumbe huo ulikiuka sheria za kampuni hiyo kuhusu habari za kupotosha kuhusu ugonjwa wa COVID-19 na kwamba kundi hilo la kampeni litabidi kuondoa ujumbe huo kabla ya kuruhusiwa kutumia tena mtandao huo.

Rais wa Marekani- Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP Images/Star Max/D. V. Tine

Muda mfupi baadaye, akaunti hiyo ya kampeni ya Trump ilianza kutumika tena hii ikiashiria kuwa video hiyo ilikuwa imeondolewa. Kundi hilo la kampeini ya Trump limezishtumu kampuni hizo kwa ubaguzi na kusema Trump alisema ukweli.Msemaji wa kundi hilo Courtney Parella, amesema kuwa kampuni za mawasiliano ya mtandaoni sio watetezi wa ukweli.

Maafisa wa afya wayahimiza makundi ya watu wote kujilinda 

Maafisa wa afya wamewahimiza watu wa makundi yote kujilinda na hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. Trump alitetea ujumbe wake kuhusu athari ya virusi hivyo kwa watoto alipotakiwa kuzungumzia suala hilo wakati wa kikao na wanahabari mapema Jumatano.Trump alisema kuwa alikuwa anazungumzia kuhusu kuathirika vibaya zaidi na virusi hivyo na kuongeza kuwa watoto wana uwezo mkubwa wa kukabiliana navyo.

Katika miezi ya hivi karibuni, kampuni ya Facebook imekuwa chini ya shinikizo kali kutoka kwa wabunge na wafanyakazi wake kwa kutochukuwa hatua dhidi ya machapisho ya uchochezi kutoka kwa Trump. Awali kampuni hiyo iliondoa matangazo kutoka kampeni ya kuchaguliwa tena kwa Trump kwa kuvunja sheria za habari za kupotosha  katika tukio la karibu na sensa ya kitaifa.Pia iliondoa machapisho ya Trump na matangazo ya kampeni yake yalionesha pembe tatu nyekundu zinazoagalia chini, ishara iliyotolewa na wanazi kuwatambua wafungwa wa kisiasa kwa kukiuka sera dhidi ya chuki ya kupangwa.

Trump amekuwa akituhumiwa mara kwa mara kwa kueneza habari za kupotosha kuhusu janga la virusi vya corona ambalo limesababisha zaidi ya vifo vya raia 150,000 wa Marekani ikiwa ni pamoja na tetesi zisizo za kawaida kwamba waathiriwa wa virusi hivyo huenda wakachomwa sindano za dawa za kuuwa vimelea vya wadudu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW